Mwanajeshi aeleza Nyerere alivyohenyesha walinzi shambani

Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda kushiriki shughuli za uzalishaji mali wakat wa uongozi wake na hata baada ya kustaafu kama anavyoonekana hapa.Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Tabia ya Mwalimu Nyerere ya kupenda kushiriki kazi za mikono kama kilimo na kuwa karibu na majirani zake, hakupenda sana kulindwa na kuna wakati aliwahenyesha walinzi wake kwa kuwatoroka hasa alipokuwa akienda shambani kulima.

“Sifa za Mwalimu ni nyingi, lakini kubwa zaidi alikuwa mtu wa watu”.

Hiyo ni kauli ya mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Butiama wilayani Butiama, Mkoa wa Mara. Pia ni kauli inayofanana na zilizotolewa na wengi kijijini hapo ambako Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 na kuzikwa Oktoba 23, 1999.

Hakuna hata mmoja kati ya wote nilioongea nao kuhusu “maisha baada ya miaka 19 bila Mwalimu” katika kijiji hicho aliyesema baya lolote lililowahi kufanywa na Baba wa Taifa wakati alipokuwa hai na mkazi wa Butiama.

Taji Masengwa, mwanajeshi mstaafu aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Rwamkoma, kiasi cha mwendo wa dakika tano hivi kwa gari kutoka hapo hadi Butiama ni miongoni mwa watu waliobahatika kuishi nyumbani kwa Mwalimu katika kijiji hicho.

Wakati mmoja, Masengwa aliyestaafu jeshi Juni 30, 2017 kuna wakati aliteuliwa na wakuu wake wa kazi kikosini kwake kwenda kuwa mmoja kati ya wasaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere, anasema alipata nafasi ya kumfahamu vizuri Rais huyo wa Kwanza wa Tanzania.

“Hata wakati anaondoka (Butiama) katika safari ile ya kwenda London, Uingereza kwa ajili ya matibabu nilisafiri pamoja naye kwenye ndege kutoka Musoma mpaka Dar es Salaam,” anasema mwanajeshi huyo mstaafu.

Wakati Mwalimu alikuwa akitoka Musoma kuelekea Dar es Salaam katika safari yake hiyo ya mwisho kutokana na ukweli kwamba hakurudi tena Butiama akiwa hai, Masengwa alikuwa akienda nyumbani kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanganyika na baadaye Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Tanzania marehemu, Rashid Kawawa huko Kiluvya, nje kidogo ya jiji hilo kujifunza kilimo cha uyoga.

Anasema alikwenda Kiluvya kujifunza elimu hiyo ili akirudi akafanye kazi ya kusimamia kilimo hicho katika mashamba ya Mwalimu Nyerere, lakini bahati mbaya Baba wa Taifa akafariki dunia alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza Oktoba 14, 1999 na huo ukawa ndiyo mwisho wa kozi yake hiyo.

“Kutokana na kifo hicho hata kozi yangu ya kilimo cha uyoga ikaishia hapo. Nikahamishiwa katika kikosi cha JKT Ruvu (kilichopo Kibaha, Mkoa wa Pwani),” anasema, lakini miezi michache baadaye alirejeshwa Rwamkoma alikoanzia kazi Agosti, 1983 baada ya kuhitimu mafunzo yake ya awali ya kijeshi katika iliyokuwa kambi ya JKT Masange, Tabora, wakati huo.

“Kwa kweli nilikuwa namfahamu vizuri sana Mwalimu kwa sababu niliishi naye nyumbani kwake hapahapa Butiama na mara kadhaa tulikuwa tukikaa wawili tu tunapiga stori, kusema kweli alikuwa hana mfano,” anabainisha.

Mathalani, Sajini Masengwa anasema wakati Baba wa Taifa alipokuwa hai, idadi ya watu waliokuwa wakiishi nyumbani kwake ilikuwa kubwa na ikiongezeka mara kwa mara, lakini baada ya kifo chake hakuna aliyebaki.

“Wote waliondoka,” anasema na kuongeza: “Kipindi hicho watu walikuwepo wengi sana pale nyumbani kwake. Walikuwapo mpaka watoto yatima na watu wazima mpaka wazee na walikuwa mchanganyiko (akimaanisha wanaume na wanawake)”.

Pamoja na kuwapenda sana watu na bila ubaguzi wa aina yoyote, anasema Baba wa Taifa alikuwa akimheshimu na kumthamini kila mmoja, hatua ambayo pia ilisababisha naye apendwe na kila mmoja katika upande mwingine.

Maelezo hayo ya Masengwa yanashabihiana na yaliyotolewa na Mzee James Sorongai (73), mkazi wa kitongoji cha Busegwe.

Sorongai anasema Mwalimu alikuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi mbalimbali kwa sababu alikuwa akiwasaidia kwa hali na mali ikiwamo kusikiliza matatizo yao na kuwapa ushauri unaotakiwa.

Akizidi kubainisha anasema tabia hiyo ilikuwa faraja kubwa kwao “na siku zote alikuwa zaidi ya baba wa familia”.

Ninapomuuliza kama ana kumbukumbu ya jambo lolote baya lililofanywa na Baba wa Taifa iwe kwake mwenyewe au kwa watu wengine, Sorongai anasema bila kuchelewa kwamba “hakuna”.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa Butiama na maeneo mengi yaliyopo jirani na kijiji hicho ambacho kipo umbali wa kilomita 45 mashariki mwa mji wa Musoma, makao makuu ya Mkoa wa Mara, wanakiri kuondokewa na “lulu” iliyokuwa na thamani kubwa katika maisha yao.

Kama anavyosema Sajini Masengwa, Mwalimu Nyerere alikuwa rafiki na msaada mkubwa kwa kila mtu na tegemeo la aina yake kwa wanakijiji wa Butiama na vijiji vingine.

Licha ya kuishi kwake Ikulu kwa miaka 23 mfululizo akiwa Rais kuanzia Desemba 9, 1962 hadi Novemba 5, 1985 alipong’atuka kwa matakwa yake mwenyewe, Mwalimu Nyerere hakutaka hata siku moja aonekane kuwa ni mtu wa daraja tofauti la maisha na watu wengine.

Mavazi yake siku zote yalikuwa ya kawaida na daima alikuwa na tabia ya kudumu ya kuwatembelea majirani zake ili kuwajulia hali na kuongea nao.

Aliwashangaza wengi alipong’atuka urais na kurejea kijijini kwake Butiama kuwa mkulima na mwanakijiji wa kawaida sawa na wengine, na pia alikuwa akichukua jembe lake la mkono na kwenda kulima katika mashamba yake.

Aidha, Masengwa anasema anapokuwa kijijini au nyumbani kwake hata walinzi wake alikuwa akiwatoroka mara nyingi na kuondoka peke yake akiwa anatembea kwa miguu, hasa anapotaka kwenda shambani na alikuwa hapendi sana kupanda gari.

“Alikuwa hapendi kabisa kulindwa anapokuwa kijijini kwake”, anasema mwanajeshi huyo mstaafu aliyefanya kazi hiyo kwa miaka 34, miezi mitatu na siku 20 kuanzia Machi 10, 1983 hadi Juni 30, 2017 na kuongeza:

“Walinzi wake wanapomkosa akiwa ametoroka na kutembea kwa miguu badala ya kwenda shambani kwa gari walikuwa wakihaha sana kumtafuta, baadaye wakipita njia za mkato kumfuatilia shambani kwake wanamkuta anatembea kwenda huko.”

Ikitokea hivyo, Masengwa anasema walinzi hao walikuwa hawana cha kufanya zaidi ya kumfuata kule anakokwenda ili kuhakikisha usalama wake na kurudi naye baadaye.

Naye Wambura Nyamhanga anamwelezea Mwalimu Nyerere kwamba alikuwa Rais mstaafu na kiongozi wa kimataifa anayeishi maisha kama wanakijiji wengine.

Mara nyingi anapokuwa akipumzika nyumbani kwake hasa nyakati za jioni alikuwa akipenda kucheza bao na wazee wenzake, mchezo wa jadi aliokuwa akiupenda na kuucheza mara kwa mara.

“Hivi sasa wananchi wanapokuwa na shida wanakwenda kwa mwenyekiti wa kijiji, ofisa mtendaji au kwa Joseph Butiku anapokuja kutoka Dar es Salaam,” anasema Mzee Nyamhanga.

Kana kwamba haitoshi, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Ghati ambaye anaishi kijiji jirani cha Bisarye alikoolewa mwaka 2008, anasema ingawa alikuwa na umri wa miaka 12 wakati Baba wa Taifa anafariki, lakini anamfahamu na bado anakumbuka mengi aliyofanya.

Mathalani, Ghati anasema idadi kubwa ya watu waliokuwa wakiishi nyumbani kwa Mwalimu kipindi hicho anaikumbuka vizuri, na pia hajasahau jinsi alivyokuwa mkulima hodari na mzee mwenye upendo mkubwa kwa kila mtu hata wale anaokutana nao kwa mara ya kwanza.

Anakumbuka namna watu walivyokuwa wakienda kulima kwenye mashamba ya Baba wa Taifa katika kile kinachoitwa “vipande” ambapo mtu hukatiwa eneo la kulima au kupalilia na kulipwa fedha taslimu, lakini ajabu aliyoiona ni kwamba watu hao siku zote walikuwa wakipelekwa shambani na kurudishwa na gari bila malipo yoyote.

Mbali na usafiri, watu hao pia walikuwa wakipikiwa na kupelekewa chai asubuhi na baadaye chakula cha mchana, jambo ambalo hakuna anayeweza kulifanya na hadi sasa hajawahi kuliona tena Butiama wala katika kijiji cha Bisarye alikoolewa.

Hakika, Baba wa Taifa alikuwa ni kiongozi wa watu miongoni mwa watu. Alikuwa ni kiongozi aliyeishi karibu na watu, alizielewa shida za watu na alishughulika kuzitatua shida hizo za watu.

Hapo ndipo inapodhihirika kuwa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa ni darasa muhimu la uongozi kwa viongozi wa sasa na wajao.