Mwangwi wa sauti ajali ya MV Nyerere una mafunzo lukuki

Muktasari:

  • Hii ni ajali ya pili kubwa katika Ziwa Victoria baada ya ajali Mei 21, 1996 iliyohusisha meli ya Mv Bukoba iliyozama na watu zaidi ya 800 walifariki dunia. Je, hakuna funzo lililotokea baada ya ajali ya Mv Bukoba, kuna tatizo gani katika suala la uokoaji. Hayo ni maswali ya kujiuliza.

Wanasaikolojia na wanasosholojia wamekuwa wakieleza mbinu mbalimbali za kijamii na kisaikolojia, namna ya kuendana vizuri na watu watata. Hata hivyo, napenda andiko la mwandishi, Celestine Chau, lililochapwa na jarida la mtandao, Dumb Little Man, na kuwekwa kwenye tovuti ya biashara na fedha Marekani, Business Insider, Januari 22, 2011.

Chau, raia wa Singapore, aliandika, “9 Useful Strategies to Dealing with Difficult People at Work”, yaani mikakati mizuri tisa ya kuchukuana na watu wagumu kukaa nao kazini.

Jinsi alivyoainisha mikakati hiyo tisa na uchambuzi wake, inatosha kuwa somo la watu kujua namna ya kujenga uhusiano na kuelewana na watu watata kijamii. Ni mikakati inayotosha kuwajenga viongozi wa nchi ili kuwa na namna bora ya kuwaelewa na kuwaongoza wananchi ambao kwa namna moja au nyingine wanaowaona ni watata.

Mkakati wa kwanza, anasema ‘uwe mtulivu’, usiwe na haraka ya kupandisha jazba. Jazba hazitaleta maelewano zaidi ya kuukuza utata. Pili, ‘elewa dhamira yake’. Kuhusu hili la uelewa, anafafanua kwamba hakuna mtu mtata bila sababu. Jishughulishe kujua kiini na dhamira ya utata wake.

Mkakati wa tatu, anashauri ‘pokea mtazamo wa watu wengine’. Naam, unaweza kumwona mtu mtata kumbe wengine hawamwoni hivyo. Ukizungumza na watu na kukupa maoni yao, utaweza kujua wapi umesimamia. Inawezekana tatizo si mtu, bali wewe kwa namna unavyomchukulia.

Imeandikwa mikakati tisa, ila katika kujenga maudhui ya makala haya, naomba nizungumzie hiyo mitatu. Shabaha ni kupita katikati ya hoja hasi na chanya juu ya ajali ya kivuko cha MV Nyerere, kilichozama katika Ziwa Victoria, Septemba 20, mwaka huu.

MV Nyerere, ilizama ikiwa inatokea kisiwa cha Bugolora kwenda Ukara. Makisio ya eneo ambalo kivuko hicho kilizama ni umbali wa kati ya mita 50 na chini ya mita 100, kabla ya kufika kwenye gati la bandari ndogo ya Ukara.

Zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha. Wananchi wa kawaida hasa wavuvi walifanya kazi kubwa kuokoa watu. Idadi kubwa ya manusura iliokolewa na wananchi wa kawaida. Hili ni eneo ambalo linasababisha mwangwi mkali wa sauti. Upande mmoja unakera, lakini pia unafundisha.

Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alitoa agizo la kusitishwa kwa shughuli za uokoaji usiku wa Alhamisi (Septemba 20), kwa maelezo kuwa giza lilikuwa totoro, akaagiza kazi ya kuokoa iendelee alfajiri ya siku iliyofuata, yaani Septemba 21 (Ijumaa). Agizo hili pia limesababisha manung’uniko mengi, japokuwa yeye amesema ilikuwa ni ushauri wa wataalamu.

INAENDELEA UK 18

Utulivu na uelewa

Serikali kwa nafasi yake, inaweza kuwa kwenye upande mmoja ikiwatazama wakosoaji kwamba ni watu watata. Hapo sasa nakurejesha kwenye mikakati mitatu niliyoichagua ya kuishi na watu watata. Kwanza lazima Serikali iwe na utulivu. Isichanganyikiwe na maneno mengi yenye kutolewa.

Mitandaoni kuna mashambulizi ya kila aina. Mengine kutoka kwa viongozi wa kisiasa na wengine wananchi wa kawaida. Kila mmoja anawasilisha hisia zake kuhusu namna alivyoguswa na vifo vya Watanzania wenzake. Hivyo, baada ya utulivu, kinachotakiwa ni kuelewa dhamira zao.

Watu wanaipenda nchi yao. Wanawapenda ndugu zao. Dhamira zao ni kuona ajali kama ya Mv Nyerere ilivyotokea, basi uokoaji unafanyika kwa nguvu kubwa na idadi kubwa zaidi ya watu wanapata nusura ya maisha. Kitendo cha watu waliokufa kuwa mara nne zaidi ya waliookolewa hakifurahishi.

Kama kadirio la umbali ni kati ya mita 50 na 100, maana yake kwa kuchukua ukubwa wa kiwanja cha soka, watu waliosimama kwenye milingoti ya goli la upande mmoja, wanashuhudia watu wakifa katikati ya uwanja au mbele kidogo, kabla ya kufika lilipo goli la pili. Na kwa umbali huo, watu waliopoteza maisha ni wengi mno.

Ni wajibu wa Serikali kuvaa utulivu na kuelewa wananchi wanazungumza nini. Ni kweli kwamba malalamiko mengine yanakera. Wapo Watanzania wanadhani nchi yao imebobea katika teknolojia ya uokoaji majini kama nchi za Magharibi. Hivyo, wanalaumu bila kujua kwamba mengine husababishwa na uwezo mdogo wa nchi.

Hata hivyo, jinsi viongozi wa Serikali wanavyoona kero kwa maneno ya wakosoaji na wapondaji, wajielekeze kusoma dhamira ni kwa kiasi gani Watanzania wanataka nchi yao iwe. Zaidi wanataka utu na kujali kulikozidi kipimo linapoibuka janga kama hilo la Mv Nyerere.

Mathalan, shughuli ya uokoaji ilisitishwa usiku mpaka alfajiri kupisha giza. Hili limewaumiza sana wananchi. Kuna wengine wamezungumza maneno makali mno. Hizo ni hisia, viongozi wachukue maumivu yao na siku nyingine wasifanye uamuzi kama wa Ukara.

Kuahirisha uokoaji mpaka asubuhi kilikuwa ni kitendo ambacho kimetafsiriwa na wengine kuwa roho za Watanzania wenzao zilikatiwa tamaa sababu ya giza. Wanaamini kwamba giza lingekuwa totoro kiasi gani, kulikuwa na namna tofauti ya kufanya ili mapambano ya uokoaji yaendelee. Injinia wa kivuko, Alphonse Charahani alikutwa hai baada ya siku mbili. Tafakari!

Ajali ilitokea saa 8 mchana. Mamlaka za nchi zilipumbazwa kiasi gani, hata kushindwa kukumbuka kwamba uokoaji ungefanyika mpaka usiku, hivyo maandalizi ya taa, tochi na vifaa vingine vya uokoaji usiku majini kuandaliwa? Kwa saa 8 mchana, hata Tanzania yote kusingekuwa na vifaa, ingewezekana kuomba msaada haraka nchi jirani na ungepatikana.

Lawama za Watanzania zinakumbusha mambo mawili; mosi, ni kwamba kuliko kuahirisha bora watu wangekesha kutafuta njia tofauti ya uokoaji. Kauli kwamba ilishindikana kuokoa mtu yeyote kwa sababu ya giza licha ya jitihada za usiku mzima, ina faraja kuliko kuwaambia watu wakalale mpaka alfajiri uokoaji uendelee.

Pili, inakumbusha wakati mwingine yakitokea majanga, watu wawaze nje ya boksi. Lazima kamati zijigawe. Laiti kungekuwa na kamati ya uokoaji usiku, ingetambua mahitaji ya usiku ni yapi. Ni hapo vitendea kazi vya gizani vingetafutwa ndani na nje ya nchi. Bila shaka kusingekuwa na uahirishaji kama uliofanyika.

Vema kupokea mitazamo

Mei 21, 1996 Meli ya Mv Bukoba ilizama ikiwa inakaribia Bandari ya Mwanza. Watu zaidi ya 800 walifariki dunia. Malalamiko ni kuwa uwezo wa uokoaji na uamuzi wa kuitoboa meli kwa juu, ni sababu ya kupoteza watu wengi ambao inadhaniwa walikuwa bado wazima ndani ya meli.

Malalamiko ya wengi yalibeba hisia kuwa mahali ambako Mv Bukoba ilizama, palikuwa karibu na bandari, kiasi kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuokoa watu wengi, kama uamuzi na vitendo vya uokoaji, vingeshabihiana na mazingira ya wakati husika. Huwezi kuzuia watu kulaumu. Na walilaumu kwamba uzembe na umakini mdogo ni chanzo cha vifo vingi.

Septemba 20, 2018, yaani miaka 20 na miezi minne baadaye, ndani ya ziwa lilelile, mkoa uleule (Mwanza), ajali inatokea mchana kweupe, takriban mita 50 kufika nchi kavu, wanaokolewa watu wachache, wengi wanaopolewa wakiwa wameshaaga dunia.

Kwa mazingira hayo huwezi kuzuiwa watu kuhoji ni kipi ambacho Serikali ilijifunza baada ya ajali ya Mv Bukoba? Umbali kutoka nchi kavu na idadi ya watu waliopoteza maisha, ni wazi kwamba Mv Nyerere ina mshangao mkubwa kuliko Mv Bukoba. Mshangao huo pia unajumuisha na muda wa ajali. Mv Bukoba ilizama alfajiri. Mv Nyerere mchana watu wakishuhudia.

Septemba 10, 2011, meli ya Mv Spice Islander, ilizama Bahari ya Hindi, eneo la Nungwi, Zanzibar na watu zaidi ya 200 walipoteza maisha. Ukitazama Nungwi na kina chake kirefu, umbali na changamoto ya mkondo wa bahari, kama Mv Nyerere ingezama umbali na eneo lenye changamoto kama Nungwi, pengine maafa zaidi yangetokea.

Ukipita mitandaoni kila tamko la Serikali halikosi mwangwi. Mathalan, tangazo la Serikali kuhusu akaunti maalumu ya michango ya rambirambi, limeibua maoni mengi, mengine yakiwa kama kejeli, lakini Serikali ina kitu cha kujifunza.

Watoa maoni wanakumbusha kilichotokea wakati tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Fedha nyingi kiasi cha mabilioni ya shilingi zilipatikana. Ikadhaniwa kwamba pengine waathirika wangepewa fedha ili kukarabati makazi yao. Wengine walijitolea mpaka vifaa vya ujenzi kama mifuko ya saruji na mabati.

Kilichotokea umma ulitangaziwa kwamba michango iliyokusanywa, isingekabidhiwa kwa waathirika, badala yake ingetumika kukarabati miundombinu. Kipindi hiki wito baadhi ya watoa maoni wanahoji; je, fedha hizi hazitabadilishiwa matumizi?

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemaliza utata, ameeleza kuwa michango inayokusanywa kwa ajili ya waathirika wa ajali ya Mv Nyerere, haitatumika vinginevyo zaidi ya kuwasaidia familia za marehemu na majeruhi.

Hii kuonyesha kuwa amesikia sauti zenye mwangwi kuhusu michango. Huo ndiyo uwe mwelekeo, kila sauti ipokelewe kwa hasi na chanya. Serikali ina mengi ya kujifunza badala ya kukereka