UCHAMBUZI: Mwinyi Zahera: Vazi Limewapendeza Yanga

Sasa waulize kuhusu Yasuf Manji, watakuwa wastaarabu kipindi hiki na mnaweza kujadili na kuelewana kuhusiana na yeye kurejea ama kutokurejea kama mwenyekiti.

Ni suala ambalo halihitaji hoja kubwa ya kulielezea na hata uchaguzi uliopangwa kufanyika unaweza kuendelea bila vurumai ya wanachama na mashabiki, kwa sababu kubwa moja tu, Mwinyi Zahera.

Wakati Mo Dewji anatangaza kuingia rasmi kwenye ‘siasa’ za soka la Tanzania kupitia klabu ya Simba, walioathirika kwa kiasi kikubwa ni mashabiki na wapenzi wa Yanga.

Maisha hayakuwa rahisi kwao kwa sababu ya usajili wa bilioni moja wa Mo, lakini hayakuwa rahisi zaidi kwa kambi za kijanja ambazo Simba walikuwa wanakwenda kwenye maandalizi ya msimu mpya.

Maisha ambayo Manji aliwapa pale walipotaka ndiyo ambayo yalikuwa nakshi ya kipindi hiki kwa Mo.

Wakiwa katika kipindi hicho kigumu, Yanga walihitaji malaika mmoja tu ambaye angeweza kushika sikio la kila mmoja wao na kupenyeza sauti yenye mvumo wa radi ambayo ingewastua wote na kuwaambia fedha siyo kila kitu.

Ndicho kilichotokea kwa Mwinyi Zahera, naam tunakishuhudia kwenye uso wa soka la Tanzania kwa sasa.

Ajabu na kweli kwamba maisha yamekuwa rahisi na matamu kwa Yanga kuliko ambavyo wengi walidhani na kutegemea.

Yanga imekuwa timu yenye muunganiko bora zaidi kwa sasa kweye Ligi Kuu Tanzania Bara lakini pia hata nidhamu ya wachezaji inaonekana imeimarika kuliko wakati mwingine wote uliopita.

Zahera anaonekana amepata tiba, amewafahamu wachezaji wake na sasa kila akitoa amri wanatii. Nilitazama wakati akimpa moyo na kupuuza maneno yaliyoelekezwa kwa kipa wa Klaus Kindoki na presha anayopata kutoka kwa mashabiki baada ya kuanza vibaya langoni.

ninaamini kuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuna upendo mshikamano na amani imetawala kwenye mioyo ya wachezaji.

Usajili kwenye soka ni jambo moja, kupatia saikolojia, aina ya uchezaji na kupata kikosi imara ni mambo mengine ambayo yanaamua mafanikio au kuanguka kwa timu husika. Pamoja na ubora ambao Simba imekuwa nao, usajili mkubwa waliofanya bado Yanga imeduwaza kwa kuwa na matokeo bora kuliko wao, hakuna aliyehisi hili litatokea. Kuanzia mfumo mpaka wachezaji wanaoamua matokeo yao unaona kabisa kuna kitu ambacho kimepulizwa kwenye akili yao na kocha Zahera kinachowafanya kuwa tofauti.

Kuna nyakati ambazo mchezaji aliye kwenye kiwango bora alikuwa Ibrahim Ajibu, lakini bado haikumwekea kinga ya kukaa benchi pale ilipobidi.

Kuna kipindi Haritier Makambo alikuwa kama amesahau viatu vyake lakini sasa amevikumbuka, bila kusahau hata akina Mrisho Ngassa, Raphael Daud na Feisal Salum ‘Feitoto’ wamekuwa na moto uliosaidia uokaji wa keki hii inayoliwa taratibu na mashabiki wa Yanga kwa sasa.

Inawezekana kabisa kuwa muda bado na wanaweza kupoteza kasi waliyoanza nayo lakini kama ni kweli mvua hainyeshi bila mawingu kuwepo dalili, nao wameonyesha dalili.

Nimeamini, kukiri na kuamini katika Mwinyi Zahera, moyo unaniambia atawafikisha Yanga mbali, akili yangu inasema hii ni taarifa kwa klabu nyingine Tanzania.

Kwa mafanikio ya klabu, kabla ya fedha unahitaji usimamizi sahihi wa rasilimali, uongozi imara na nidhamu. Hivi kwa pamoja huepusha migongano na hubeba uhalisia wa timu.

Yanga inavutia, imependeza na imevaa vazi la heshima kwa sasa kileleni mwa msimamo wa ligi hata ile kofia ya ufalme wanastahili kuivaa mpaka pale atapopatikana wa kuwapindua.

Bahati nzuri ni kuwa hawabahatishi na mlinganyo kati ya safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji kimahesabu ukokotoaji wake ni rahisi.

Natamani kuona chachu ya baraka hizi za Zahera inakwenda mpaka kwenye uchaguzi wao.