NDANI YA BOKSI: Kipaji ni moja, usimamizi ni jambo lingine...

Muktasari:

  • Ni kama Alikiba. Bila kuwa na watu makini nyuma yake. Ambao kwa makusudi waliamua kumsimamia angeishia huko walikoishia wengi sana. Tukubali kuwa bila Diamond asingekuwa King Kiba huyu tuliyenaye hivi sasa. Mafanikio ya Diamond ‘yalimbusti’ Kiba au kumuamsha.

Michael Jackson. Binadamu ambaye ni nembo halisi ya burudani ya muziki duniani. Alianza kuzungukwa na walinzi chini ya miaka kumi. Tayari dunia ilimjua akiwa staa mkubwa mwenye umri mdogo. Kwa umri wake siyo tu alistahili kulindwa bali na kuongozwa kwa kila kitu.

Unashangaa ukubwani kushinda na kucheza na watoto mpaka kupata kesi ya udhalilishaji? Usishangae. Ni kwa sababu Michael hakuwahi kupata muda wa kucheza na wenzake utotoni. Yeye tayari alikuwa anaishi kwa ratiba. ‘Supa staa’ mkubwa. Anayelindwa na kuongozwa.

Hakucheza marede wala mdako. Hakuijua komborela, ‘baishoo ailavyu bebi’ wala kibaba baba. Aliruka hatua ya makuzi na kuanza kuzeeka bila kufanya vitu ambavyo binadamu lazima ufanye. Akajikuta uzeeni anafanya mambo ya kitoto. Kosa la kutofanya jambo kwa muda sahihi.

Muda. Hapana, haujawahi kuwa rafiki na kitu chochote. Ukiachwa na muda basi ndo imetoka hiyo. Huwezi kukata rufaa kuurudisha nyuma. Kitu pekee utakachokifanya kwa ufanisi zaidi baada ya hapo ni kuanza kujutia.

Kuna washikaji wengi ambao walishindwa kutumia muda vizuri. Leo wanajuta. Maisha yamebadilika, wanashindwa washike lipi waache lipi. Tatizo ni pale walipopata pesa badala ya mafanikio wakaanza kuvimba. Pesa bila usimamizi bora ina maisha mafupi kama funza.

Farid Kubanda ‘Fid Q’ ‘taikuuni’ la mashairi na vina. Ni kielelezo cha vipaji halisi visivyo na karama ya kuweza kujisimamia yeye na kazi zake. Tatizo hata kujua nani anafaa kumsimamia yeye na kazi zake ameshindwa. Ngosha anaelea katikati ya kipaji na maisha yake.

Anabaki kwenye kundi la wanamuziki ambao mwili unaishi dunia ya sasa lakini fikra za dunia iliyopita. Bado wana mizuka ya ‘intavyuu’ za vipindi vya mchana redioni. Wakati ukweli ni kwamba watangazaji walipaswa kuota ndoto za kufanya ‘intavyuu’ na kina Fid.

Ndiyo maana leo unasikia Wema Sepetu kafungua sehemu duka la nguo na vitu vya watoto. Ni jambo zuri sana, lakini lingekuwa zuri na lenye manufaa kwake zaidi kama angefungua miaka saba nyuma. Muda wa kufanya hili kwa ‘kurelax’ aliacha upite, sasa anafanya kwa ‘presha’ ya watu.

Huenda leo angefanya jambo kubwa zaidi. Muda ulivyo na roho mbaya pamoja na kasauti na hips zake zile amazing flan, haujamsubiri. Muda siyo ‘romantic’ kabisa hata kwa warembo. Leo yupo daraja moja na Mobetto ambaye miaka mingi alimsikia Wema na kumsoma gazetini.

Leo wanagawana muda na kina Nandy na Young Killer. Huu ni ulimwengu wa mitandao siyo wakati wa ‘Kim &The Boys’ au Khadija Mwanamboka. Na mwisho wa siku ni kuweka ‘bifu’ na muda.

Wengi hawajui kwamba mitandaoni ndo

kila kitu. Wao wanatumia kusemana, ujuaji mwingi. Majivuno ya kibwege na kuishia kujisifu kwa kumiliki nyumba na gari.

Hatuwezi kulaumu wasanii, kama wasimamizi wa kazi zao wanaamini mafanikio ni gari. Hapa ujiulize Babu Tale na Chibu yupi ni meneja wa mwenzake? Tale ndo yule anayeamini Fid Q kakosa mafanikio kisa hana gari. Na Chibu ndo yule ambaye anawekeza pesa kwenye miradi ‘deile’.

Akili za uwekezaji za Chibu hazitokani na kichwa kinachoamini mafanikio ni gari. Kaanza kununulia ‘ndinga vicheche’ vya mjini kabla ya utawala huu. Kama angekuwa na akili za meneja wake asingekuwa Chibu huyu tunayemuona. Nadhani sasa mnaelewa kwanini wasanii wengi wamekata ringi.

Kuna wakati nilijiuliza kwa nini Diamond ana wasimamizi wengi wa kazi zake? Baadaye nikagundua kuwa hata wale hawatoshi. Na naamini kuwa tunaowaona kila siku mitandaoni na majukwaani siyo. Kuna watu nyuma ya pazia wanaocheza mchezo wa akili zaidi. Muda utasema.

Kabla ya Kiba kutangaza kurudi kwenye kiti chake. Na kwamba hakuna aliyekikalia bali anafuta vumbi na kukalia upya. Tayari Diamond alikuwa mbali maili nyingi sana. Na ‘intavyuu’ za mwanzo za Kiba ndizo zilizozua ‘bato’ lililopo mpaka leo. Bila shaka timu yake ya Kiba ilijua kucheza karata vizuri.

King Kiba alikuwa kama kaususa muziki. Ngoma kali kama Dushelele aliitolea video mbovu sana kama zile za ‘komunio’ au ‘kicheni pati’ za uswahilini. Ilikuwa ngoma kubwa pengine kuliko zote zilizofuata. Lakini hakuwekeza kwenye video kali ndo maana hatuna kumbukumbu nayo nzuri.

Kipindi hicho tayari Diamond toka anaanza na “Nenda Kamwambie”, anadondosha ngoma zenye video kali tupu. Hajawahi kubahatisha kwenye video dogo. Na anabaki kuwa mwanamuziki pekee ambaye hajawahi kuuchezea muda hata kwa bahati mbaya. Kila upenyo anakandamiza.

Watu wa Kiba baada ya hapo walijua wanachofanya. Bila kuzungukwa na akili kubwa tungemuhifadhi kwenye makabrasha ya “Jamaa alikuwa mkali sana.” Tungeishia kusema: “Wee muangalie hivyo hivyo huyo jamaa, alikuwa anaimbaa... ndiye aliyeimba Sinderela.”

Ukitaka kuamini hilo tazama mafanikio makubwa ya Kiba yameanza wakati upi. Kuanzia ubora wa video na usambazaji wa kazi zake. Hapo kabla Kiba aliacha kazi zake zisambae zenyewe mitaa ya Kibera Nairobi na Mombasa. Hakuwa na timu ya kusambaza kazi zake vya kutosha.

Ndo maana Diamond alikusanya kama wote. Kamata Fella, teka Babu Tale, na kumficha Sallam. Fella na Tale waliacha kundi la wanamuziki (TMK Wanaume, Ya Moto Band na TipTop Connection) na kwenda kutengeneza kundi la mameneja kwa Diamond.

Fella na Tale huenda wametengeneza zaidi wakiwa kundi la mameneja wa Diamond, kuliko waliposimamia makundi ya muziki. Wao waliunda makundi ya muziki, Diamond amejenga kundi la mameneja. Muda wa sasa wa Jibebe siyo kama ule wa Dar Mpaka Moro.

Kuna vipaji vingi sana ambavyo vimetoweka kwa kukosa usimamizi. Mandojo na Domokaya ni sehemu ya vipaji yatima. Ama kwa uzembe wao au fitna za ‘gemu’. Kuna wale ambao waliamini pesa ndo mafanikio kamili. Walipopata senti wakaacha muda userereke kama gari bovu mtaroni.

Mafanikio siyo gari na nyumba. Hivyo ni vitu tu vya msingi na lazima kwa binadamu. Mafanikio ni zaidi ya nyumba na gari. Marehemu Remmy Ongala mafanikio yake hayatazamwi kwa nyumba zake za Sinza na Mbezi tu. Hizi fikra lazima ziteketezwe kwenye vichwa vya madogo hawa.

Leo tunataja jina la Bob Marley kwa idadi na ubora wa nyimbo zake na siyo ukubwa na wingi wa nyumba zake. Michael Jackson siyo kwamba tunamkumbuka kwa mijengo na magari yake. Hata familia zao zinaendelea kuneemeka kwa kazi zao siyo magari na mikufu waliyotanulia mitaani.

Tunapoacha vijana waamini hivyo matokeo yake ndo kina Ferouz. Baada ya kupata Jeep Cherokee tu, mizuka ya kazi ikaishia hapo. Akaona kishamaliza kila kitu. Ndivyo ilivyo hata kwa Juma Nature baada ya gari na kibanda cha kuhifadhi mwili wake kupatikana.

Waandishi wakaanza kutangaza kama gari na nyumba ni mafanikio halisi kwa msanii. Nao wakavimba kichwa. Wakaanza kujitenga na marafiki waliowafikisha pale walipo. Kubadili kila kitu kuanzia madem, utembeaji, vyakula, viwanja vya kula bata, nywele rangi mpaka vilevi.

Ndo maana wengi wakaishia kwenye dawa za kulevya. Kwa kuamini hakuna la kufanya zaidi kwenye maisha yake. Unapoona Blue anaendelea kufanya kile alichofanya 2004 kwa ubora uleule. Mpe heshima yake maana ni kama kuvuka bahari bila kuloa korodani.

Afande Sele na Fid Q kulundikana kwenye ‘kosta’ ya Wasafi Festival na Fiesta. Ni matokeo yale yale kama ya Michael Jackson kutocheza marede utotoni na kutamani kucheza uzeeni. Muda wa kulundikana kwenye ‘kosta’ ulishapita. Leo wangeweza kuwa mawakala wazuri wa hizo shoo Kanda ya Ziwa na Morogoro.