Najisikia amani kuwa CCM-Gekul

Oktoba 13 mwaka huu aliyekuwa mbunge wa jimbo la Babati Mjini Mkoani Manyara, Pauline Gekul aliandika barua kwa spika wa Bunge, Job Ndugai ya kujiuzulu nafasi hiyo, akajivua uanachama wa Chadema na nafasi zote alizokuwa nazo na kuomba kujiunga na CCM.

Katika mahojiano na Mwananchi, Gekul anasema, “Huku CCM kuna amani, upendo, mshikamano na umoja.” Endelea.

Swali: Unajisikiaje kuwa ndani ya chama ambacho hukukizoea?

Jibu: Ni kweli sikukizoea, katika maisha yangu ya siasa sijawahi kujiunga na CCM kwani siasa niliianza nikiwa Chadema. Kwa sasa nina amani ya kutosha kuwa kwenye chama ambacho sikukizoea kwani wanachama na viongozi wamenipokea kwa mikono miwili na kunipa ushirikiano na upendo wa kutosha.

Swali: Jambo gani unadhani utashindwa kufanya ukiwa CCM ambalo ukiwa Chadema uliweza kulifanya.

Jibu: Nikiwa Chadema nilishindwa kuwa huru kukutana na viongozi wa Serikali na wa CCM ili kufanikisha maendeleo kwani nikifanya hivyo nilikuwa naonekana kama msaliti ila kwa sasa nikiwa CCM nitafanikisha zaidi lengo la wananchi wa Babati Mjini kupata maendeleo.

Hakuna kitu nitashindwa kufanya nikiwa CCM ambacho nilikuwa nafanya nikiwa Chadema kwani Serikali ya CCM inasikiliza zaidi, tofauti na awali nikiwa mbunge kupitia Chadema.

Swali: Unaizungumziaje hoja kuwa madiwani na wabunge wa upinzani wanaojiunga na CCM wananunuliwa?

Jibu: Hoja ya wanaohama upinzani kwenda CCM kuwa wananunuliwa haina mashiko kwani kuna baadhi ya viongozi wa CCM waliwahi kutoka huko na kujiunga na vyama vya upinzani.

Wanaoshabikia hoja hiyo wangeeleza hao waliokuwa viongozi wa CCM wakajiunga na vyama vya upinzani kina Lazaro Nyalandu walinunuliwa kwa shilingi ngapi?

Swali: Unajisikiaje kuwa mwanamke wa kwanza kujiuzulu ubunge?

Jibu: Nimekuwa mwakilishi wa wananchi kupitia Chadema miaka minane iliyopita kwa kuanza na ubunge wa viti maalumu mwaka 2010-2015 baada ya kugombea jimbo la Babati Mjini na kuambulia kura 7,000 nikimfuatia mgombea wa CCM aliyepata kura 10,000 kati ya wapiga kura 19,000.

Mwaka 2015 nikitambua nafasi ya viti maalumu ni fursa ya kujengewa uwezo nilijitoa na kugombea ubunge na kushinda ambapo nilipata kura zaidi ya 21,000 mgombea wa CCM kura 16,000 na mgombea wa ACT-Wazalendo takribani kura 500.

Nilipata ubunge huo na kuwa miongoni mwa wanawake sita walioshinda kwenye majimbo na najisikia huru mwenye amani moyoni kuwa mwanamke wa kwanza kujiuzulu ubunge.

Swali: Mbali na kuunga mkono utendaji wa Rais John Magufuli, unazo sababu nyingine za kujiuzulu, ni zipi?

Jibu: Ndio ninazo. Sababu nyingine ni kuwa mzigo wa kuendesha chama uliachwa mabegani mwa wabunge. Kwenye chaguzi ndogo hakuna msaada kutoka makao makuu ilhali chama kinapata ruzuku ya zaidi ya Sh300 milioni na wanawakata zaidi ya Sh500,000 kila mwezi.

Nimevumilia kunyanyaswa na kutengwa, kazi ya chama cha siasa ni ulezi na usimamizi wa maslahi ya wale waliotupa dhamana lakini silioni hilo likifanyika vyema.

Mimi ni mwanamke, mama wa watoto wawili najua uchungu wa kulea na nafahamu uchungu walionao wananchi wa Babati Mjini, hivyo niliamua kushirikiana na serikali ya CCM ili kukamilisha miradi ya maendeleo.

Swali: Una mikakati gani baada ya kurudishwa tena bungeni bila kuopingwa?

Jibu: Mimi ni kiongozi makini ninaweza kujenga hoja na kuitetea hivyo nitaendelea moto wangu wa kuwatetea wananchi wa jimbo la Babati Mjini ili kuhakikisha wanapatiwa maendeleo.