Ng’ombe kanasa mtego wa panya!

Muktasari:

“Bwana mkubwa ule ni mtego wa panya. Wanaingia waliomo na wasiomo. Ebu fanya maarifa uupige dochi ufyatuke ili nami nipate riziki mantashah… Maana ni mchana huu…”

Panya aliuona mtego aliotegewa baada ya kuguguna suti ya mwenye nyumba. Alikitazama kwa uchu mkubwa kipande cha samaki alichotegewa, lakini kabla hajadondosha udelele akamwona jogoo akikatiza kwa nje. Alimkimbilia akiwa na uhakika kuwa tatizo lake litapata ufumbuzi.

“Bwana mkubwa ule ni mtego wa panya. Wanaingia waliomo na wasiomo. Ebu fanya maarifa uupige dochi ufyatuke ili nami nipate riziki mantashah… Maana ni mchana huu…”

Jogoo alikataa akisema, “mimi nakula pumba halali, si sawa na wewe unayepiga chabo visivyokuhusu vyumbani mwa watu. Nenda kadonoe pale mtegoni ukamuliwe haja!”

Panya akaondoka kinyonge. Lakini hamadi… beberu akaibuka karibu naye. “Bwana mkubwa, ule mtego umekaa vibaya. Hebu kaupige pembe tutapata mlo na sote tutajihakikishia usalama.”

Beberu lilicheka na kumzogoa panya: “Aliyekwambia mtego unanihusu ni nani?”

Basi panya aliamua kwenda kwa kubwa lao; fahali. Akamweleza hadithi nzima juu ya mazungumzo yake na jogoo na beberu. Akamsisitizia kauli yake ya kwamba mtego umekaa tenge maana mtego wa panya hupiga hata wasio na hatia. Hunasa waliomo na wasiomo.

Fahali akasema, “nimekuelewa bwana mdogo. Lakini huyu mwenye nyumba ndiye anayenilisha na kunitunza. Nikikusaidia wewe nitakuwa nimemkiuka yeye. Siku moja utakula pesa ambazo angezitumia kunipatia chakula na matibabu”.

Panya alinywea na kwenda kulala nyuma ya kabati.

Usiku wa manane kitu kikajibu: “kacha!” Mwenye nyumba akashtuka na kuitikia “Kanasa huyo!” Alitoka kitandani na kushika kiatu mkononi kama silaha. Akatafuta kiberiti cha kuwashia taa lakini akakikosa. Mkewe alimwambia “kwani ukimwacha hadi kukuche atatoroka?” Lakini akamjibu kuwa ana hasira naye.

Yule bwana alikwenda akiupapasa mtego, lakini mara aliguna “Akh! Ati kaning’ata!”

Mkewe alipapasa huku na kule hadi akabahatika kupata kiberiti. Alipowasha kandili ndipo alipogundua kuwa aliyenasa kwenye mtego ni nyoka, na kwamba mumewe ameng’atwa naye!

Alipiga uyowe na kuitikiwa na majirani. Walimhangaikia yule bwana bila mafanikio maana alifariki usiku huo. Asubuhi zilipelekwa taarifa kwa ndugu wa karibu na wa mbali, na kwa sababu pale nyumbani palikuwepo na majirani wachache, walichinjiwa jogoo kwa kitoweo.

Panya alimpungia mkono jogoo huku akimwambia beberu, “wakati mwenzio ananyolewa wewe tia maji…” Na kweli walikuja ndugu na jamaa, wakamzika ndugu yao na siku ya tatu wakaanua tanga. Maisha ya beberu yaliishia siku hiyo.

Mwezi mzima ulipita. Kwa mila na desturi siku ya arobaini wafiwa walisoma hitima, yaani walimaliza msiba. Siku hiyo ndugu, jamaa na marafiki wengi walipata nafasi ya kuhudhuria. Alfajiri ya siku hiyo panya alimwamsha fahali: “Je, unakumbuka nini juu ya mtego wa panya?”

Fahali alimkosa panya teke kubwa huku akimtaka amwondolee uchuro. Lakini muda mfupi baadaye parapanda ikamlilia kubwa lao; fahali la ng’ombe.

Kama ingelikuwa akili ni nywele watu wote tungekuwa wajinga. Asilimia kubwa ya wanaotupa elimu ya darasani na hata elimu ya maisha wana mgogoro mkubwa na nywele; sijui inatokana na nini hasa, umri au kufikiria sana, au yote mawili.

Wao ndio waliotufundisha kuwa aliye juu usimpandie, msubirie hapo chini. Atakapomaliza haja zake huko ni lazima atateremka. Hakuna kiendacho juu moja kwa moja kwani hata moshi hushuka kama maji.

Lakini kuna watu waliojiona kuwa na akili zaidi, wakafanya kinyume chake. Mfalme Juha alipolalamikiwa kuwa kila kitu kinapandishwa bei bila kushushwa, aliamua kupanga bei elekezi ili wanaopandisha wakwame. Aliagiza kila kitu kiuzwe hela moja; sukari, nyumba, tumbaku na kila kilichouzwa basi kiuzwe kwa bei hiyo.

Matokeo yake wajanja na wenye fursa walifanikiwa, lakini wenzangu na mie wakazidi kuumia. Kuna walionunua ratili ya dhahabu kwa hela moja, wakasafiri kwenda kuuza mbali kwa mamilioni ya hela. Na waliporudi nchini mwao wakanunua mamilioni ya nyumba.

Lakini kuna bwana mmoja aliyependa kula, alinunua na kula mbuzi mmoja kila siku kwa hela moja. Akawa mnene kiasi cha kusababisha mauaji ya mafundi ujenzi. Mtia maji udongo alishtuka kuona kipande ya mtu ikikatiza, akaongeza maji bila kukusudia na nyumba ikawaporomokea.

Mbaya zaidi ilimuangukia mfalme mwenyewe. Alimhukumu bonge la mtu kunyongwa. Lakini mjanja mmoja aliomba kunyongwa badala ya bonge kwa sababu “atakayekufa siku hiyo atapokelewa peponi”.

Juha akaja juu: “Yaani ukale bata kiulaini hivyo? Kwa nini nisinyongwe mimi?”

Uzuri wa watu wenye akili waliunena na kuutenda ukweli. Wengi walikutana na mazingira magumu wakaitwa waongo au wachochezi, na wengine walitukanwa hata baada ya kufikwa na mauti (kama aristotole). Lakini ukweli ulithibitika na kuwaweka huru.

Kizazi hiki kisidhani kuwa wahenga wetu walikuwa wachoyo au waroho walipopiga marufuku matumizi ya mayai kwa kinamama wajawazito. Ilikuwa ngumu kuwaeleza kuwa watoto watanenepa na kuzaliwa kwa taabu. Na enzi zile matokeo yalikuwa ni vifo kwani hakukuwa na uzazi wa kisu.

Kwa lugha nyepesi walitishia kuwa mwiko huo ukivunjwa, mtoto atazaliwa akiwa na bichwa kama yai lisilokubali nywele.

Lakini uongo wao uliokoa wengi.