UCHAMBUZI: Ni muungano wa Zitto na Chadema kuliko ACT Wazalendo vs Chadema

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Uturuki, uliofanyika Juni 24, mwaka huu, vyama vya upinzani vya Iyi na Saadet vilisema kuwa vimeungana na chama kikuu cha upinzani cha CHP kwa ajili ya uchaguzi, hivyo baada ya uchaguzi, hawakuona sababu ya kuendelea kushirikiana.

CHP, Iyi na Saadet, viliungana kutengeneza umoja waliouita, The People’s Alliance (muungano wa watu), ili kuongeza nguvu katika kukikabili chama tawala, AK na mshirika wake, MHP.

Hata hivyo, wapinzani hawakufua dafu. AK na MHP walipata wabunge wengi na Rais Tayyip Erdogan alifanikiwa kutetea kiti chake kwa muhula mwingine.

Julai 4, mwaka huu, mtandao wa Shirika la habari la Uingereza, Reuters, ulimnukuu msemaji wa chama cha Iyi, Aytun Ciray na Kiongozi wa Saadet, Temel Karamollaoglu wakisema kuwa muungano wao haukuwa umoja wa vyama, bali ushirika wa uchaguzi.

Kilichotokea Uturuki kinakumbusha vyama vilivyounda Ukawa, kwa maana ya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi vilivyoungana mwaka 2014. Ukawa ulihusu ushirikiano wa kutetea maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba Mpya.

Masilahi ya Katiba ndiyo yaliwaunganisha Ukawa. Wao wakanogewa na kushawishika kuingia pamoja kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 kabla ya kuvurugana.

Mgogoro wa uongozi CUF, chanzo chake ni Ukawa. Mgawanyiko ulitokea kuhusu uamuzi wa Chadema kumpokea Edward Lowassa kutoka CCM na kumsimamisha kugombea.

Upande mmoja wa CUF ulikataa, mwingine uliridhia. Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba akajiuzulu. Baada ya uchaguzi, akarejea kuudai uenyekiti wake. Sehemu ya uongozi ikamkubali, wengine wakakataa. Sasa wapo mahakamani.

Siyo hilo tu. Utaratibu wa kuachiana majimbo na kata za uchaguzi, uliibua migogoro. Yapo maeneo wagombea wa vyama vyote walisimama, kwingine malalamiko ya kuhujumiana yaliibuka.

Kuelekea uchaguzi mdogo jimbo la Buyungu, Kigoma, vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vilitangaza kushirikiana. Ushirikiano ulihusu jimbo hilo na kata 79, katika uchaguzi uliofanyika Agosti 12, mwaka huu. Buyungu walifanya uchaguzi baada ya aliyekuwa mbunge, Kasuku Bilago (Chadema) kufariki dunia.

Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe ana nguvu kubwa ya ushawishi Kigoma. Ni hapo ndipo kuna swali; Chadema walishirikiana na ACT kama chama au Zitto kama mtu binafsi mwenye ushawishi wa kitaasisi?

Hata baada au kabla ya uchaguzi mdogo wa Buyungu, Zitto amekuwa akionekana kushirikiana na Chadema kuliko viongozi wengine wa ACT. Je, Zitto ndiye anautaka ushirikiano na Chadema kuliko wenzake au Chadema wanamhitaji Zitto kuliko ACT nzima kama chama?

Zitto alikuwa bega kwa bega na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotajwa kwenye orodha ya watuhumiwa kutumia na kuuza dawa za kulevya, iliyotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Februari mwaka jana.

Zitto alikuwa mstari wa mbele kuusema ukatili aliofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alipopigwa risasi Septemba 7, mwaka jana. Aliandika twitter, Facebook na Instagram. Aliandika makala kuelezea ubaya wa unyama aliotendewa Lissu. Si hivyo tu, Zitto alikwenda Nairobi Hospitali na baadaye Ubelgiji kumtembelea.

Zitto amekuwa akipanda majukwaa ya Chadema kuzungumza na wananchi. Agosti mwaka huu, mkutano wake Esther Matiko na John Heche Tarime ulisambaratishwa na polisi.

Hivi karibuni, Zitto alilazwa mahabusu siku mbili. Viongozi wa juu wa Chadema walitoa matamko ya kutaka aachiwe huru na kumfariji. Haitoshi, wabunge Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Heche, walikwenda Kituo cha Polisi Mburahati, Dar es Salaam, kumtembelea.

Ni sawa na ambavyo Zitto amekuwa akijitoa kwa ajili ya viongozi wa Chadema. Mfano kumuunga mkono Lissu aliyekuwa anashikiliwa na polisi, Sugu, Lema na Lijualikali wakiwa mahabusu. Kama ni kuelekea 2020 mapambano ya demokrasia na utawala bora, malengo yawekwe wazi na yaheshimiwe kama wapinzani Uturuki walivyoyaishi makubaliano yao.