Nini sababu za mahusiano ya wengi kuishia kuvunjika?

Dr chriss mauki

Muktasari:

  • Sababu hizi zinaweza kupelekea moja kwa moja wanandoa kutengana au zinaweza pia kuchangia pamoja na sababu za kundi la pili kuongeza msukumo wa kutengana.

Baadhi ya tafiti zilizofanywa kwenye jamii na maeneo tofauti zinaonyesha sababu zilizo katika makundi mawili zinazoweza kusababisha ndoa nyingi kuvunjika. Kundi la kwanza ni sababu zinazo anzia kabla ya kuanza kuishi pamoja na zinazohusika na mchakato mzima wa maisha ya mtu.

Sababu hizi zinaweza kupelekea moja kwa moja wanandoa kutengana au zinaweza pia kuchangia pamoja na sababu za kundi la pili kuongeza msukumo wa kutengana.

Sababu za kundi la pili

Sababu kundi la pili ni yale matatizo ya kila siku ambayo wanandoa husuguana nayo baina yao. Matatizo haya mengine ni tabia za mtu alizokuja nazo ndani ya mahusiano yenu na anaziendeleza, na mengine yameibuka mkiwa tayari kwenye mahusiano (aidha unajua chanzo chake au hukijui). Matatizo au sababu hizi zaweza kusababisha mtengane, lakini huchukua uzito zaidi pale zinapochanganyika na zile za kundi la kwanza. Sababu hizi ni kama vile;

Katika sababu zote hizi, wanandoa wengi waliokwisha kutalikiana wametaja ‘mapenzi nje ya ndoa’ kuwa sababu kubwa iliyowapelekwa kuamua kutengana.

Hasira kali

Kuwa na hasira sio kitu cha ajabu, wengi wetu tuna hasira. Hasira inayozungumzwa hapa ni ile ya haraka, (short temper) isiyomruhusu mtu kufikiria mantiki ya kitu anachokasirikia, na kuamua tu kuchukua maamuzi ambayo mara kwa mara ni ya uharibifu au kusababisha maumivu kwa mwili au hisia za mwingine. Mara nyingi watu wa jinsi hii hukimbilia kuomba msamaha mara wakishapoa lakini msamaha huo hata pale unapotolewa hauwezi kufuta makovu yaliyozalishwa na hasira zile. Inakuwa ngumu kwa wapenzi kuendelea na mahusiano hasa pale ambapo hasira na matukio haya yanajirudia mara kwa mara. Hata kama mpenzi mmoja ni mwingi wa rehema sana anajikuta anafikia ukomo wa uvumilivu.

Tatizo lingine la tabia hizi ni kwamba, mara nyingi kila zinapotokea kupunguza kiwango cha penzi na imani kwa mwingine na taratibu unajisikia kumhofia mwenzako zaidi ya kumheshimu na kumpenda.

Hisia za maumivu na machungu

Wako watu wenye tabia au haiba ya kujisikia maumivu na machungu ya moyo na nafsi kila wakati. Machungu haya sio asili au yakuzaliwa nayo bali yanatokana na maisha ya kila siku. Kwa mfano, makuzi yetu, au mahusiano yetu ya awali yanaacha majeraha mioyoni mwetu na mara tunapoanza mahusiano mapya bado zile hisia za nyuma “negative reflections” zinatukumbusha machungu na maumivu.

Hali hii ikizidi kwa muda mrefu inakufanya uonekane kama ndiyo kawaida yako. Hali ya kutokuwa na furaha muda mwingi, kuto kuonyesha unapenzi kwa mwenzako au kuonyesha unalikubali penzi unalopewa kunafanya uwe ‘butu’ kihisia.

Taratibu ombwe inaanza kutokea kati yenu na kama msipo shituka mapema na kuamua kuishughulikia hali hii kwa haraka basi mnajikuta zile hisia za ukaribu “intimacy” na ule mvuto baina yenu “chemist” inakufa kabisa. Kinachofuatia ni mmoja kutafuta kuliwazwa kwingine au kutaka mtengane ili kila mmoja atafute hamsini zake.

Kutofautiana kwenye matumizi ya pesa

Utakubaliana na ukweli kwamba wako wengi ambao wamejikuta wanafikia tamati ya mahusiano yao kwasababu tu hawakuweza kuendana katika kasuala yanayohusu pesa.

Hapa namaanisha utafutaji wa pesa na matumizi ya pesa. Mara nyingi fedha imekuwa ikileta maumivu makubwa kwenye mahusiano kwasababu fedha ina uhusiano mkubwa na hisia za mwanadamu kwahiyo kutofautiana kokote katika eneo la fedha kunaleta maumivu makali ya moyo na hisia.

Kwa mfano, mpenzi wako ana matumizi makubwa ya pesa tofauti na mnavyoingiza, mpenzi wako ana madeni yasio ya lazima, mpenzi wako sio muwazi kwenye mambo ya pesa na hujui mapato wala matumizi yake, mpenzi wako anaugumu mkubwa katika kutumia pesa yake kwenye mambo yako, mbahili na hayuko tayari kupoteza hela yoyote kwako.

Inatokea pia wapenzi kutofautiana kwenye vipaumbele katika matumizi ya pesa, mmoja anataka wafanye hivi wakati mwingine anatamani watumie peza kufanya vingine, hapa msuguano unaibuka. Ni vema kujua kwamba tofauti hizi katika mambo yahusuyo fedha husababishwa na mazingira mengi ikiwemo malezi na makuzi yetu na namna wazazi wetu walivyo pandikiza mtazamo wa fedha aidha kwa wao kujua au hata pasipo kujua.

Hii itawasaidia wazazi leo kuwasaidia watoto wetu kuwa na mtazamo chanya kuhusu masuala ya pesa na matumizi yake.

Kwa hisani ya matokeo ya utafiti uliofanywa na Amato na Rodgers