Njia sahihi ya kuepuka saratani

Unapozungumzia maradhi yasiyoambukiza, basi huwezi kuacha kutaja maradhi ya saratani.    

Nayo ni miongoni mwa maradhi yanayowatesa wananchi wengi kutokana na kushindwa kuzitambua dalili zake za awali.

Hali hiyo inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa huchangia kwa kiwango kikubwa wagonjwa wengi kufika katika vituo vya afya wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne ya ugonjwa, ambazo huleta ugumu katika matibabu.

Wanasema iwapo mgonjwa wa saratani atatambua dalili za awali za ugonjwa huo, mara nyingi ni rahisi kwake kutibiwa na kupona kabisa.

Mratibu wa Programu ya Via vya Uzazi kutoka Wizara ya Afya, Dk Safina Yuma aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema; watu wengi nchini huchelewa kupata ugunduzi na tiba kwa haraka, jambo linalochangia kuleta ugumu katika matibabu.

Kwa hapa nchini, zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mbele zaidi.

Lakini hivi karibuni serikali imeongeza juhudi katika kuhakikisha inapigana vikali na maambukizi mapya ya saratani na kuitokomeza hususani zile zinazoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Mpaka sasa saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi iliyo na asilimia 32.8 ya wagonjwa, ikifuatiwa na saratani ya matiti yenye asilimia 12.9 ambayo ni karibu asilimia 50 ya wagonjwa wote kwa mujibu wa takwimu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali iliongeza bajeti ya dawa za saratani kutoka Sh700 milioni hadi Sh7 bilioni mwaka huu, huku idadi ya vituo vya afya vinavyoweza kubaini saratani ya mlango wa kizazi na matiti ambazo zinaongoza hapa nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kufikia 600.

“Tunaamini kuwa endapo vituo hivi vitaanza kutoa huduma za uchunguzi, idadi ya wagonjwa itaongezeka zaidi kuliko wale 50,000 wanaogunduliwa hivi sasa kila mwaka,” anasema Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. “Ndiyo maana tuliamua kuanza kutoa chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 ili kuhakikisha kuwa tunawalinda kama taifa la kesho, nipende kuwahakikishia kuwa chanjo hiyo haina madhara kama inavyotangazwa,” anasema Waziri Ummy.

Hata hivyo, waziri huyu anasema binafsi anaamini katika kipindi cha miaka 10 ijayo, saratani ya mlango wa kizazi itakuwa ni historia kwa sababu nchi ya Australia imeweza kupunguza saratani hiyo kwa asilimia 86. Katika mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kufanyika jijini Dar es Salaam, mada ilizungumzia maradhi yasiyoambukiza. Mjadala huo ulioitwa ‘Mwananchi Jukwaa la Fikraa’, wataalamu wa afya na wadau wao walijadili kwa kina tatizo la maradhi ya saratani yanayoingia katika kundi la maradhi yasiyoambukiza na baadhi ya wataalamu walitaja njia rahisi zinazoweza kutumika na mtu mmoja mmoja kuzuia saratani kama kama zitafuatiliwa kwa makini na kila mmoja.

Mkurugenzi Mkuu NIMR, Profesa Yunus Mgaya alisema kuna haja kubwa kwa watu kuanza kuepuka mazoea ya kutumia vitu vilivyopigwa marufuku na wataalamu kwa kisingizio kuwa madhara yake hayaonekani. “Kuna vitu vingine havihitaji fedha kubadilika, tumewahi kupewa elimu mara kadhaa kuwa kuweka chakula cha moto katika vitu vya plastiki au mifuko kuna hatari ya mtumiaji kuugua saratani kutokana na rangi ya vyombo au plastiki yenyewe kuyeyuka. Sasa kama tunazungumza haya, kwanini tuendelee kuvitumia,” alihoji Profesa Mgaya.

Mwanafunzi wa udaktari kutoka Chuo cha Afya Muhimbili, Yusra Hamza alisema wazazi wanapaswa kubadilisha mwenendo mzima katika kuwalea watoto wao ili kuhakikisha wanawakinga na maradhi yanayoweza kuwapata baadaye. “Zamani mzazi alikuwa akimfungashia mwanawe vitu vya kubeba shuleni, atamuwekea vitu vilivyopikwa kiasili kama viazi, muhogo, lakini siku hizi mzazi anamuwekea mtoto soseji, chokleti nyama za beef, vitu vimesindikwa si salama sana kwa afya,” anasema Yusra.

Anasema ulaji wa vyakula hivyo unaweza kumletea mtoto madhara kama hakutakuwa na mabadiliko au kama atakuwa mvivu wa kufanya mazoezi. “Tusije kutafuta wachawi wa watoto wetu baadaye, wakati wachawi wao wa sasa ni sisi wazazi tuwafanye wapende kutumia vitu vya asili na wakue katika misingi hiyo,” anasema Yusra.

Ufanyaji wa mazoezi pia umetajwa kuwa ni moja ya mambo yanayoweza kusaidia kupunguza wagonjwa wapya wa saratani.

“Siku hizi watu wavivu sana, hawawezi hata kutembea hata mwendo wa kilomita mbili bila kupanda bodaboda au daladala tofauti na zamani watu walipokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma,” anasema Dk Chrispin Kahesa, Daktari Bingwa wa Maradhi ya Saratani Ocean Road. Anasema suluhisho la matatizo haya ni pamoja na ulaji mzuri wa vyakula vyenye kujenga mwili na kujiepusha na vitu vinavyoweza kukuweka katika hatari ya kupata maambukizi mapya ya saratani. “Unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara, matumizi mabaya ya vidonge vya uzazi wa mpango hususani katika umri mdogo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya ya saratani,” anasema Dk Kahesa.

Elimu stahiki pia juu ya masuala yanayochangia kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani inatakiwa itolewe zaidi katika maeneo ya vijiji kuliko na uhitaji mkubwa zaidi kuliko mijini, anafafanua daktari huyo bingwa. “Wataalamu ni vema nao wakaangalia maeneo yenye uhitaji mkubwa kwa kufanya uchunguzi ili kujua mahitaji ya watu kabla ya kuwapatia elimu,” anasema Dk Faraja Chiwanga, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata).

“Tuangalie ni eneo gani lina uhitaji sana ili kujiaminisha kuwa kile tunachokitoa kinawafikia watu sahihi, hakipotei bure, inaweza kusaidia kuwabadilisha watu na tukafanikiwa kugundua wagonjwa wengi walio katika hatua za awali,” anasema daktari huyo.

Alimalizi kusema; “Wananchi wanapaswa kuelimishwa kusudi waweze kuondokana na imani potofu juu ya ugonjwa wa saratani na imani za kishirikina.