Njia sahihi ya kumbaini mwanaume mgumba

Muktasari:

  • Kipimo hiki hufanyika kwa lengo la kuchambua kwa kina sampuli ya mbegu za kiume zilizotolewa katika kiwanda cha mbegu za kiume na lengo ni kubaini na kuwasaidia waathirika tatizo la ugumba.

Kipimo muhimu kinachotumika kumchunguza mwanaume mwenye tatizo la ugumba ni cha upembuzi yakinifu wa mbegu zake za kiume ambazo kitabibu zinaitwa ‘Semen analysis au sperms count test’.

Kipimo hiki hufanyika kwa lengo la kuchambua kwa kina sampuli ya mbegu za kiume zilizotolewa katika kiwanda cha mbegu za kiume na lengo ni kubaini na kuwasaidia waathirika tatizo la ugumba.

Mwenza wa kiume mwenye tatizo la kutotungisha mimba hushauriwa na wataalamu wa tiba kufanya kipimo hicho kwa nia ya kubaini kama tatizo hilo lipo upande wake au la.

Kipimo hiki huweza kumpa daktari taswira ya ndani ya ubora wa mbegu za mwanaume na hivyo kubaini kama tatizo ni mbegu au laa.

Vile vile, humwezesha daktari kujua kama uchache wa mbegu au udhaifu wake ni sababu ya mwenza huyo kuwa mgumba.

Kwa kawaida manii (semen) ni majimaji yaliyobeba shahawa (mbegu za kiume, sukari na protini) ambayo kwa pamoja hutolewa wakati mwanaume anapofikia mshindo.

Kipimo hiki huweza kutazama mambo makuu matatu ambayo ndiyo msingi wakuweza kubaini matatizo ya mbegu au kubaini mwanaume aliyefungwa kizazi kama njia hiyo imefanikiwa.

Mambo hayo ni pamoja na kutambua idadi, maumbile na mwendokasi wa mbegu hizo.

Njia hii hufanywa kwa umakini mkubwa ikiwamo muhusika, huitajika kuchukuliwa sampuli mara tatu zinazofanywa kwa nyakati tofauti lengo ni kubaini afya ya mbegu hizo kwa usahihi.

Upimaji wa sampuli hizo huachanishwa kwa muda wa siku saba na kufanywa ndani ya miezi miwili hadi mitatu. Hii ni kwasababu idadi ya mbegu huwa tofauti kwa kila siku inayopita.

Ili kupata sampuli yenye kukidhi kiwango, mwanaume hutakiwa kuepuka kujamiana na kufika mshindo saa 24 hadi72 kabla ya kuchukua sampuli.

Anatakiwa kuepuka kutumia pombe, kahawa na dawa za kulevya ndani ya siku 2-5 kabla ya kupimwa.

Anatakiwa kuepuka kutumia dawa yoyote ya kienyeji na vile vile kutotumia dawa zozote zenye vichochezi (hormones).

Atahitajika kuwa na utulivu wa kimwili na kiakili, kuepuka kazi ngumu, mazoezi magumu na msongo wa mawazo. Anatakiwa kupumzika na kulala angalau saa 6 hadi 8 kwa usiku mmoja.

Mambo haya ni ya msingi ili kupata majibu sahihi na kama hayatazingatiwa huweza kuathiri matokeo ya kipimo.

Sampuli ya mbegu hupatikana kwa njia ya kujichua (masturbation), kujamiana na mwenza kwa mpira wa kiume, kujamiana na mwenza na kumwaga nje mbegu katika chombo maalumu.

Kwa nchi zilizopiga hatua ipo njia ya kufikia mshindo na kuchukua sampuli kwa usisimuliwaji kwa kutumia umeme.

Kwa nchi zetu za uchumi mdogo mpaka wa kati, njia nzuri yakupata sampuli bora ni kwa njia ya kujichua. Ikumbukwe kuwa baada tu ya sampuli kuchukuliwa katika chombo maalumu itatakiwa kuhifadhiwa katika jotoridi sawa na lile la mwili, mazingira ya joto au baridi kali matokea yanaweza kuwa na dosari.

Jambo lingine ni kuhakikisha kuwa sampuli ya manii inafikishwa katika huduma za afya ndani ya dakika 30 hadi 60.

Ikumbukwe pia viko vitu vingine vinavyoweza kuleta athari hasi katika kipimo navyo ni pamoja na manii kukugusana na dawa yakuulia wadudu, kuwa na msongo wa mawazo na sampuli kuchukuliwa kwa muathirika akiwa anaumwa.

Pia, makosa ya mchunguzaji ikiwamo kugusanisha sampuli hiyo na zingine.