Pitana, mcheza filamu aliyegeuka adui Croatia

Muktasari:

  • Pitana anatajwa na mashabiki wa Croatia ni adui namba moja kwa kuwa wana amini ndiye aliyewanyonga katika mchezo wa fainali dhidi ya Ufaransa.

Kama kuna mtu ambaye anachukiwa zaidi nchini Croatia ni Nestor Pitana.

Pitana anatajwa na mashabiki wa Croatia ni adui namba moja kwa kuwa wana amini ndiye aliyewanyonga katika mchezo wa fainali dhidi ya Ufaransa.

Mwamuzi huyo ambaye kabla ya kugeukia soka, alikuwa muigizaji, amepata umaarufu kutokana na umbo lake la miraba minne na msimamo katika mechi zote alizochezesha.

Kama alivyotambulika Mtaliano, Pierluigi Collina kwa msimamo na macho yake makubwa, Pitana amebeba sifa ya umbo lililojengeka vyema kwa mazoezi.

Bao la kutatanisha la mkwaju wa penalti lililofungwa na Antoine Griezmann limemuweka pabaya mwamuzi huyo raia wa Argentina mwenye umbo la miraba minne.

Miongoni mwa wachambuzi wa soka waliopinga mkwaju huo ni Roy Keane ambaye bila kificho amemnyooshea kidole Pitana akimtuhumu kutofanya uamuzi sahihi.

Ivan Perisic alishika mpira ndani ya eneo la hatari na Pitana alisita kutoa adhabu kabla ya wachezaji wa Ufaransa kumzonga hatua iliyomfanya aende kujiridhisha kupitia msaada wa matumizi ya teknolojia ya video (VAR).

Pitana ameingia katika rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza kutumia VAR kwenye Fainali za Kombe la Dunia tangu mfumo huo ulipotambulishwa rasmi mwaka huu.

Licha ya umbo kubwa, Nestor Fabian Pitana alizaliwa Juni 17, 1975 Argentina na kabla ya kuwa mwamuzi wa Fifa mwaka 2014, alikuwa muigizaji.

Pitana alichezesha mchezo wa ufunguzi wa fainali hizo baina ya Saudi Arabia na Russia. Ni mwamuzi wa pili kutoka Argentina kuchezesha mchezo wa fainali za Kombe la Dunia akitanguliwa na Horacio Elizondo aliyepuliza filimbi mwaka 2006 nchini Italia.