Profesa Alwiya anavyoking'arisha kiswahili duniani

Muktasari:

  • Lugha ya Kiswahili imeendelea kufanya vyema nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Mmoja wa wadau wakubwa wa Kiswahili wanaofanikisha kuenea kwake ni pamoja na Profesa Alwiya Omar, ambaye ni mtaalamu wa lugha hiyo anayefundisha chuo kikuu Marekani tangu mwaka 1987 ambaye anaeleza mengi kuhusiana na Kiswahili.

Kiswahili kinazidi kuchanja mbuga. Ni lugha inayokua kwa kasi nje ya mipaka ya Tanzania.

Maendeleo hayo yanachangiwa na baadhi ya wadau wa Kiswahili, akiwamo Profesa Alwiya Omar; mwalimu wa muda mrefu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Indiana kilichopo nchini Marekani.

Indiana ni moja ya vyuo lukuki vilivyopo nchi mbalimbali vinavyotoa kozi za lugha ya Kiswahili.

Katika mahojiano na Mwananchi, Profesa Alwiya ambaye hivi Aprili mwaka huu alipokea tuzo ya ufanisi na utafiti wa ufundishaji wa lugha za kigeni nchini Marekani, anaeleza nafasi ya lugha ya Kiswahili na mustakabali wake.

Swali: Ulianza lini kufundisha Kiswahili?

Jibu: Nilianza kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni mwaka 1987 nilipopata nafasi ya kuja Marekani kusoma masomo ya shahada ya uzamivu ya fani ya Lughawiya (sayansi ya lugha) katika Chuo Kikuu cha Indiana, Bloomington. Nilipata ufadhili wa kusomesha Kiswahili. Ufadhili huo ulinisaidia kulipa ada za chuo na gharama nyengine.

Swali: Umekuwa ukifundisha Kiswahili kwa zadi ya miaka 30 sasa, umejifunza nini kuhusu Kiswahili nje ya Tanzania?

Jibu: Nimejifunza kuwa Kiswahili kina umuhimu sana. Kuna vyuo vikuu vingi vya Marekani na nchi nyengine duniani ambavyo vinafundisha Kiswahili. Kiswahili kinaonekana kwenye mitandao ya jamii kama Facebook.

Unaweza kupata tafsiri kama Kiswahili kwenda Kiingereza au Kingereza kwenda Kiswahili kwenye Facebook, Google na kadhalika. Kuna jamii za Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wana sherehe inayoitwa Kwanzaa. Kwanzaa ina siku saba na kila siku imepewa jina la Kiswahili.

Swali: Unadhani kwa nini Kiswahili kinawavutia wageni?

Jibu Ukiwauliza wanafunzi waliojiandikisha kusoma Kiswahili, wengi hujibu kuwa wanataka kusoma lugha ambayo ni tofauti na lugha yao.

Pia wangependa kwenda Afrika ya Mashariki kufanya utafiti, kufanya kazi kwenye programu za serikali au programu zisizo za kiserikali, na pia kujitolea au kutalii. Wanapenda sana kujua utamaduni wa wazungumzaji wa Kiswahili. Wengi waliosoma Kiswahili na kusafiri nchi za Afrika ya Mashariki, huwa wanaendelea kuwasiliana na watu waliokutana nao na hurejea tena na tena kuwatembelea.

Swali: Unafikiri Kiswahili kitakuja kuwa lugha kubwa duniani?

Jibu: Kiswahili kinakua na kinasambaa kote diniani. Ni lugha inayotumiwa katika Umoja wa Afrika. Hivi karibuni, Kiswahili kimechaguliwa kuwa lugha rasmi ya nchi ya Rwanda, na Afrika Kusini imetangaza kuwa Kiswahili kitafundishwa katika shule. Kuna makongamano yanayofanywa kwa Kiswahili Marekani, Uingereza na Ujerumani. Kwa mfano Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), huwa na makongamano Marekani kila mwaka kwenye mkutano wa chama cha walimu wa lugha za Kiafrika.

Swali: Tueleze sababu ya kupewa tuzo uliyoipokea mapema mwaka huu?

Jibu: Nilipata tuzo inayoitwa ‘Ronald Walton award’. Marehemu Walton alikuwa Mmarekani aliyehamasisha watu kuendeleza lugha ambazo hazifundishwi kwenye shule za msingi hadi sekondari na pia kwenye baadhi ya vyuo.

Mimi ni mwanachama wa chama wa National Council of Less Commonly Taught Languages (NCOLCTL) kinachohamasisha lugha zisizofundishwa. . Nilikuwa makamu wa rais kutoka 2010 hadi 2012 na rais kutoka 2012 hadi 2014. Pia ni mwanachama wa Chama cha walimu wa Kiafrika (ALTA).

Nimepata tuzo hii kwa sababu ya kuongoza vyama hivi viwili kwa muda mrefu na pia kuendelea kushiriki katika shughuli tofauti za kuendeleza ufundishaji wa lugha.

Swali:Unahisi fahari kufundisha Kiswahili nje ya nchi?

Jibu: Ndiyo. Huwa na furaha kubwa ninapowaona wanafunzi wangu wanavyoendelea na masomo yao ya Kiswahili kutoka wakati wanapoanza kusoma kwa mara ya kwanza mpaka wanapoweza kuwasiliana kwa Kiswahili kwa uzoefu na umahiri mkubwa. Baadhi ya wanafunzi niliowafundisha tunaendelea kuwasiliana na kukutana inapowezekana. Ni fahari kubwa kuwa wanathamini lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili.

Swali: Kuna wasemao Kiswahili ni lugha changa, hivyo haiwezi kutumika kufundishia. Unakubaliana kauli hii?

Jibu: Kiswahili si lugha changa. Ni lugha muhimu yenye asili na historia kubwa. Inaweza kutumiwa kama lugha ya kufundishia kutoka shule za msingi hadi vyuo vikuu. Ningependa kuwahamasisha Watanzania wote kuwa lugha ya Kiswahili inahitaji kupata kipaumbele na kupewa thamani inayohitajika. Hii, siyo kusema kuwa Kiingereza kiondolowe kabisa. Ni muhimu kujua lugha ya Kiingereza na inaweza kufundishwa kama lugha ya pili kwa kutumia mbinu bora ili wanafunzi wapate ujuzi mkubwa wa kuweza kuwasiliana kwa umahiri na watu wengine wasiojua Kiswahili.

Swali: Nini kifanyike ili Watanzania wanufaike zaidi na fursa za Kiswahili duniani?

Jibu: Watanzania wanaweza kunufaika kwa kushiriki kwenye programu mbali mbali ambazo zitawawezesha kwenda ughaibuni kufundisha Kiswahili na kuona vipi Kiswahili kinafundishwa kama lugha ya kigeni.

Kuna programu moja kutoka Marekani inayoitwa ‘Fulbright Foreign Language Teaching Assistant (FLTA) inayowapatia nafasi walimu wenye shahada ya kwanza kutoka nchi nyengine kuja Marekani kusaidia kufundisha Kiswahili kwa muda wa mwaka mmoja kwenye vyuo tafauti. Baadaye wanaweza kutuma maombi ya kusoma masomo ya shahada ya pili kwa kupitia udhamini wa kufundisha

Swali: Waeleze wasomaji kuhusu wasifu wako

Jibu: Mimi nimezaliwa na kukulia Zanzibar. Nilipomaliza kusoma shule ya sekondari Unguja, nilifundisha kwenye shule mbali mbali za msingi na sekondari na baadaye nilipata udhamini wa kwenda kusoma shahada ya kwanza ya Lughawiya na Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Kuwait. Niliendelea na shahada ya pili katika fani ya Lughawiya, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na shahada ya tatu Chuo kikuu cha Indiana.