Rais Uhuru, wabunge wavutana nyongeza ya mishahara

Wabunge na maseneta wa Kenya ni miongoni mwa wanasiasa wachache kote ulimwenguni wanaolipwa marupurupu na mishahara minono.

Mbali na hayo, wabunge hao hawajatosheka; ubinafsi na ulafi wao unaowapeleka kwa kasi na sasa wamesahau kwamba kuna Wakenya wengine ambao hawana lolote huku maisha magumu yakiwakodolea macho.

Walafi hao ambao Wakenya wanawafananisha na nguruwe kwa sababu ya tabia zao za kutotosheka na pia kujiingiza katika ufisadi, wanajitayarisha kupitisha muswada wa kuwawezesha kuongeza mishahara na marupurupu mengine.

Wanapanga kufanya hayo kwa kulenga kumtatiza Rais Uhuru Kenyatta ambaye ametangaza kwamba kamwe hawezi kuweka sahihi yake kwenye muswada huo.

Wabunge hao wanaweza kupata kura ya kutosha ya theluthi mbili kutupilia mbali uamuzi wa Uhuru wa kutosaini muswada huo. Wanajigamba kuwa, wana idadi tosha ya wabunge itakayowawezesha kupitisha muswada huo zaidi ya mara moja kama watahitajika kufanya hivyo.

Wiki iliyopita wabunge waliahirisha kupitishwa kwa muswada huo tata maarufu kama Parliamentary Service Bill , 2018 ambao ungepanua nafasi ya marupurupu siku moja baada ya Rais Uhuru kuapa kwamba hatauweka sahihi.

Muswada huo ungepitishwa wiki jana kabla wabunge hao kuanza likizo yao ya Krismasi.

Hata hivyo, haukuorodheshwa kwenye shughuli za siku katika Jengo la Bunge.

Watakapofanikiwa kusukuma matakwa yao kwa nguvu na kupitisha muswada huo, wabunge watajipatia marupurupu si haba ya usafiri wa gari lingine rasmi, marupurupu ya nyumba na ya bima ya hospitali ya wake/waume zao na jamaa.

Fauka ya hayo, wakifaulu kupindua hatua ya Rais ya kukataa kuweka sahihi kwa muswada kwa kupiga kura bungeni ya theluthi mbili, walafi hao watakuwa na uwezo na nafasi zaidi ya kujipa na kujiongezea pesa huku wananchi wakifa njaa kwa ukosefu wa chakula na dawa hospitalini.

Huku Wakenya wakiwa wameghadhabishwa na tabia hii ya kutojali miongoni mwa wabunge na maseneta, ni jambo la kusikitisha kwamba licha ya kushutumiwa na Rais Uhuru, wanaendelea kusukuma ajenda yao.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia amepinga hatua hiyo ya wabunge.

Wabunge wameapa kupitisha muswada huo kwa kuwashawishi wenzao wapige kura kwa fujo kwa mara ya pili ikiwa Rais Uhuru ataikataa kwa mara ya pili.

Iwapo utapitishwa kwa mara ya pili, kwa theluthi mbili , muswada huo utakuwa sheria bila Rais Uhuru kuuweka saini.

Wabunge hao wanataka bima yao ya matibabu wafaidi wake zao wengine (wake zaidi ya mmoja).

Bima ya sasa ni ya Ksh10 milioni; Ksh300,000 zimetengewa matibabu ya kuona daktari na kurudi nyumbani, Ksh150,000 ni za kujifungua na Ksh75,000 za matibabu ya meno.