Rais Uhuru aitikisa kambi ya makamu wake Ruto

Matamshi ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wiki jana kwamba chaguo lake la mwanasiasa atakayemchagua kumrithi baada ya kustaafu 2022 litawashangaza wengi, yametetemesha kambi ya Makamu wa Rais William Ruto.

Taarifa ya Rais Uhuru imeongeza hofu katika kambi hiyo na wanasiasa wanaompigia debe Ruto kama kiongozi atakayechukua hatamu za uongozi kuanzia 2022.

Wanasiasa hao sasa wanasema tangazo hilo ni ishara kwamba Uhuru hataki kutimiza ahadi yake kwa Ruto kama wawili hao walivyokubaliana 2013 na 2017.

“Mmoja wa wanasiasa kutoka Rift Valley anakotoka Ruto alinukuliwa na vyombo vya habari akisema; Kamwe hamtaendelea kupuuza matamshi ya Uhuru kwa sababu yanabeba uzito mkubwa katika siasa za 2022.

Matamshi yake yamekuja wakati Wakenya wanafahamu kwamba kuna mkataba kati ya Uhuru na Ruto kuhusu urais 2022.

Ruto hana budi kujua kwamba bosi wake hajamfurahia,” anasema Mbunge wa Cheran’gany, Joshua Kuttuny.

Akizungumza katika Jimbo la Nyeri wiki jana ambapo aliwazomea wabunge na maseneta kutoka eneo la Mlima Kenya ambapo yeye pia anatoka, Rais alisema wanasiasa hawafai kufikiria siasa za urithi za 2022 ilhali wananchi wanaowawakilisha wanahitaji maendeleo.

Mnamo Mei mwaka huu, Uhuru alimsuta Makamu wa Rais hadharani akisema ana tabia mbaya ya kutangatanga nchini kwa minajili ya kufanya siasa badala ya kushughulikia miradi ya maendeleo.

Wadadisi wa siasa wanasema matamshi ya hivi majuzi ya Uhuru yanamlenga Ruto na wafuasi wake ambao wamekuwa wakizunguka kila pembe ya nchi wakifanya siasa za 2022, ilhali ni mwaka mmoja tangu Kenya ifanye uchaguzi mkuu.

Uhuru na Ruto wakati mmoja walikuwa wanapendana kama chanda na pete lakini sasa kitumbua chao kimeingia mchanga na hakiliki tena.

Hii ni baada ya Raila kuingilia kati na kuharibu ndoa yao ya kisiasa baada ya kufanya mkataba wa kushirikiana na Uhuru kujenga madaraja ya amani na utengamano.

Wafuasi wa Ruto wanaendelea kutilia shaka mkataba uliofanya na Raila na Uhuru Machi 9 mwaka huu. Wanadai kuwa lengo kuu la mkataba huo ni kukigawanya chama tawala cha Jubilee.

Kuttuny anasisitiza kuwa matamshi ya Uhuru ni mazito mno na yanaonyesha wazi kwamba Ruto si mrihi wa kiti cha urais wa chama cha Jubilee kama ilivyotarajiwa hapo awali.

Maneno ya Rais pia yaonyesha kwamba amekuwa anaficha hisia zake kuhusu anayetarajia kumwachia nafasi ya urais. Hili ni jambo ambalo lazima limwamshe Ruto kutoka usingizini. Lazima aamke na afahamu kwamba mambo yamebadilika kabisa na sasa anafaa kujitafutia riziki bila Uhuru.

Wadadisi wa siasa wanasema huenda kuna mambo ambayo Ruto amefanya na kumkasirisha mdosi wake kiwango cha kutaka kumzuia asikuwe rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.

Uchaguzi mkuu ujao ni miaka minne kuanzia sasa. Tangazo lolote kuhusu nani atakayemrithi Rais laweza kusababisha mizozo mikali ya kisiasa.

Ruto sasa anahitajika kutafakari hatma yake baada ya matukio haya ambayo yanaweza kumzuia na kuzima ndoto zake kuu.

Kila wakati Rais anasukumwa pembeni na wanasiasa atangaze msimamo wake kuhusu Makamu wake wa Rais kuhusiana na siasa za 2022 na pia aseme walichokubaliana na Raila Machi 9.

Wiki mbili zilizopita, Uhuru alikwepa msukumo kutoka kwa wanasiasa jamii ya Kalenjin ambayo ni kabila la Ruto waliomtaka atangaze hadharani kwamba atamuunga mkono Ruto kuwa rais wa Kenya baada ya kustaafu kwake.

Siku chache baadaye, wabunge wengine Wakalenjin kutoka Jimbo la Bomet waliondoka kutoka sherehe ya Rais Uhuru baada ya kukosa kupewa nafasi ya kuwahutubia wananchi. Wasimamizi wa Ikulu hawakutaka Rais asumbuliwe na wanasiasa hao kuhusu suala hilo la urithi.

Wanasiasa wa mrengo wa Ruto wanafaa kufahamu msemo kwamba, akufukuzaye, hakwambii ondoka. Matendo ya Rais kwa miezi michache iliyopita yanaonyesha hataki siasa za Ruto.

Mazungumzo yoyote bila shaka yataathiri vibaya ajenda ya maendeleo ya Rais na kwa hivyo Uhuru amefanya vyema kupuuza mijadala kuhusu siasa za 2022 hadi wakati unaofaa uwadie.

Uchaguzi mkuu ujao ni miaka minne kuanzia sasa. Tangazo lolote kuhusu nani atakayemrithi Rais laweza kusababisha mizozo mikali ya kisiasa.

Rais ametazama kwa umakini mkubwa jukwaa la siasa nchini, mkataba wake na Raila na haja ya kuwaleta Wakenya pamoja na hamna shaka kwamba kuna jambo ambalo anataka kufanya bila kusukumwasukumwa kama lori lililokwamba.