Rakitic, Modric mapacha waliotia fora Russia

Muktasari:

  • Licha ya kutopewa nafasi ya kufanya vyema kutokana na Taifa hilo kuwa dogo likikadiriwa kuwa na watu wasiozidi milioni nne, Croatia imeacha historia katika ardhi ya Russia.

Croatia imeweka historia mpya katika medani ya soka duniani, baada ya kucheza mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Licha ya kutopewa nafasi ya kufanya vyema kutokana na Taifa hilo kuwa dogo likikadiriwa kuwa na watu wasiozidi milioni nne, Croatia imeacha historia katika ardhi ya Russia.

Baada kufuzu fainali, idadi kubwa ya mashabiki waliipa nafasi Croatia kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kutokana na ubora wa kikosi chake na aina ya mchezo dhidi ya wapinzani wake.

Katika mchezo wa fainali, Croatia ilifungwa mabao 4-2 na Ufaransa licha ya kuongoza kwa kumiliki mpira dakika zote tisini.

Huwezi kutaja mafanikio ya Croatia bila kuwataja wachezaji wawili Ivan Rakitic na Luka Modric ambao walikuwa injini ya timu hiyo katika fainali hizo mwaka huu.

Rakitic (Barcelona) na Modric (Real Madrid), wametajwa ndio wachezaji bora wa kiungo waliotikisa katika fainali hizo, baada ya kucheza kwa kiwango bora katika mechi zote.

Modric ambaye ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa fainali hizo, alicheza pacha na Rakitic katika eneo la katikati.

Licha ya kucheza timu pinzani katika ngazi ya klabu, lakini nyota hao kila mmoja amemtaja mwenzake kwamba alikuwa roho ya timu katika fainali hizo.

“Kaka, Luka Modric wewe ni mchezaji wa aina yake unastahili. Najivunia sana kucheza na wewe, ni fahari kwa familia na wanacroatia wote,” anasema Rakitic.

Modric aliiongoza Croatia kuvuka hatua ya makundi ikiwemo ushindi wa kushangaza wa mabao 3-0 dhidi ya Argentina kabla ya kusonga mbele kwa mikwaju ya penalti katika mechi mbili.

Croatia imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kucheza mechi tatu kwa dakika 120 katika fainali moja.