Redsan : Miaka 24 kwenye gemu

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yaliyotrend baada ya kutoa albamu yake ni madai kuwa alimpiga mtayarishaji wa albamu hiyo.

Redsan ni mmoja wa wanamuziki wa Kenya waliopenya katika nyakati nyingi za muziki Afrika Mashariki. Mwishoni mwa wiki aliachia albamu yake ya tano tangu alipoanza muziki miaka 24 iliyopita.

Miongoni mwa mambo yaliyotrend baada ya kutoa albamu yake ni madai kuwa alimpiga mtayarishaji wa albamu hiyo.

Mwishoni mwa wiki alipamba vichwa vya habari baada ya kudaiwa kumpiga makofi mtayarishaji wa albamu yake Dk Sappy. Tukio la mwanamuziki wa Nigeria, Tiwa Savage kuachwa kwenye mataa na waandaaji baada ya kuhudhuria uzinduzi wake lilichukua vichwa vya habari huku akiahidi kumsaka promota na kujiapiza kumshikisha adabu.

Kwa nini umeamua kuiita albamu yako The Baddest?

Ni kutokana na kukubalika kwangu. Nimeona nastahili kuiita hivyo kwa kuwa wanaoniunga mkono wameongezeka kadri miaka ilivyosogea. Mapenzi yao kwangu ndio nguvu yangu.

Wakati upo kimya ulikuwa unafanya nini?

Nalisoma gemu na kuangalia nani anaweza kuwa tishio kwangu. Hata ninapofanya kazi macho yangu huwa kwenye gemu. Lengo langu siku zote ni kutoa kazi inayokubalika duniani kote lakini nyumbani kwanza.

Unajionaje baada ya kuwa kwenye gemu kwa miaka 24?

Nilianza na makundi kama Kalamashakas na Five Alives, lakini niliendelea kujiongeza. Nina furaha kwamba wasanii wanaochipukia awnapita kirahisi katika njia tulizotengeneza. Najivunia hilo.

Siri ya mafanikio yako katika kubaki maarufu kipindi chote hiki?

Kujipanga vizuri. Kuwekeza katika kipaji chako na kufanya kila kitu katika wakati sahihi ni muhimu. Watu wengi hutolea maoni wenzao wanapotoa nyimbo iwe kwa kukosoa au kusifia. Tunasahau kila mtu ana maono yake. Inabidi tuache kufikira ndani ya boksi. Afrika Magharibi wanakuja na kutawala anga letu la muziki inabidi na sisi tuende kwao. Kwa kufanya kazi nzuri ndio tunaweza kufika huko.

Umeoa, familia yako inaishi wapi?

(Anacheka) Nimeoa lakini huwezi kuiona familia yangu, kwanza hawapo hata kwenye mitandao ya kijamii. Wanafurahi maisha ya kutokuwa maarufu. Napenda kutumia muda wangu mwingi kuwa na familia kwa sababu ziara za muziki huniweka mbali nao. Napenda wabaki na maisha binafsi ili watu wenye hasira na mimi wasije kuwatumia wao kuniadhibu kupitia lugha za kuudhi mitandaoni.

Unaweza kutuambia chochote kuhusu wao?

(Anacheka tena) Mke wangu ni Mkenya na mrembo sana. Tumebarikiwa watoto watatu; mmoja wa kiume na wawili wakike. Tunatarajia mtoto mwingine wanne.

Je hao ndio wanakusababisha usionekane mtaani?

Hapana, ninafanya hivyo pia kuilinda brand yangu. Nani atakuja katika matamasha yangu wakati wananiona kila mahali?