Ronaldo aendelea kutikisa Real Madrid

Monday October 1 2018

Kiungo wa Real Madrid, Marco Asensio (kushoto)

Kiungo wa Real Madrid, Marco Asensio (kushoto) akiwania mpira na beki wa Atletico Madrid, Jose Gimenez wakati wa mechi ya ‘Madrid Derby’ juzi kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu. Picha ya AFP 

Inawezekana mashabiki wa Real Madrid hawajakubali kabisa kuondoka kwa straika wao matata, Cristiano Ronaldo.

Mara zote mambo yanapokuwa magumu, humkumbuka kwa kuwa alikuwa mtu wa kuamua matokeo. Real Madrid kwa sasa haina huyu mtu.

Pale mbele kwa sasa yupo Gareth Bale lakini hajafikia mavitu ya Ronaldo. Hata akiwa pamoja na Karim Benzema lakini mambo bado.

Unaambiwa katika mchezo wa juzi wa ‘Madrid Derby’ kati ya Athetico Madrid na Real Madrid, hakukuwa na mbabe kwani baada ya dakika 90, matokeo yalikuwa 0-0.

Lakini mashabiki walimkumbuka sana Cristiano Ronaldo, walikuwa wakiimba “Ronaldo, Ronaldo” ambaye hayuko tena kwenye klabu hiyo baada ya kutua kikosini Juventus dirisha lililopita.

Kelele za Ronaldo ni baada ya Real Madrid kushindwa kushinda mechi mbili mfululizo ambazo kama ingefanya hivyo, ingeupeleka kileleni mwa La Liga. Suluhu ya Atletico Madrid ndiyo iliyowatia hasira.

Real, ilifungwa na Sevilla katikati ya wiki, na ingeweza kuiengua kileleni Barcelona, ambayo nayo ilitoka sare na Athletic Bilbao mapema kabisa.

Straika Gareth Bale aliyekuwa akitarajia kucheka na nyavu, alilazimika kutoka baada ya kuumia.

Atletico ilikosa nafasi na yenyewe baada ya Antoine Griezmann, kutandika shuti kali lililodakwa na Thibaut Courtois.

Diego Costa alipambana kupata bao lakini alishindwa kufunga ikiwa ni mechi yake ya 16 bila bao.

Mabingwa hao wa Ulaya watakuwa na kazi kesho dhidi ya CSKA Moscow wakati Atletico ambao ni mabingwa wa Europa, wataialika Club Brugge siku itakayofuata.

Advertisement