Russia: Tumeng’olewa kishujaa Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Crotia iliing’oa Russia kwa penalti 4-3, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2, katika mchezo uliopigwa dakika 120.

Russia ambayo awali haikupewa nafasi ya kutamba katika Fainali za Kombe la Dunia imeondolewa kwa penalti, lakini kocha Stanislav Cherchesov, amesema wameng’olewa kishujaa.

Crotia iliing’oa Russia kwa penalti 4-3, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2, katika mchezo uliopigwa dakika 120.

Russia haikupewa nafasi ya kufika robo fainali kwa kuwa haikuwa na rekodi nzuri katika medani ya soka duniani.

Mwaka 2010 Russia ilitupwa nje na Hispania katika hatua ya 16 bora, katika Fainali za Kombe la Dunia zilizochezwa nchini Afrika Kusini.

Cherchesov alisema licha ya ndoto yao kushindwa kutimia, lakini walipambana hadi dakika ya mwisho kuhakikisha Russia inafuzu nusu fainali.

“Tunaondoka tukiwa na furaha ya kufika mbali katika fainali, tunajivunia. Hatukuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, tumesikitika lakini tumepambana,” alisema kocha huyo.

Cherchesov alisema kitendo cha wenyeji (Russia) kushika nafasi ya 70 katika viwango vya ubora wa soka duniani kabla ya kucheza fainali hizo na kupata mafanikio ni jambo la fahari.

Alisema wanaangalia mbele baada ya kuondolewa kwenye fainali hizo, lakini amesifu juhudi za wachezaji wake aliodai walionyesha kiwango bora tangu mchezo wa kwanza.

Cherchesov alisema Rais wa Russia, Vladimir Putin aliwatakia kila la kheri kabla ya mchezo huo na alipongeza baada ya mechi kumalizika.

“Vladimir Putin alizungumza na mimi kabla ya mchezo na baadaye alinipongeza kwa mechi nzuri sana. Tulimueleza tulivyoumia, lakini alituambia tufumbue macho tusonge mbele,” alisema kocha huyo.

Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Vitaly Mutko, alisikitika kwa matokeo hayo, lakini alisifu kazi nzuri ya wachezaji.

“Tulijaribu. Nadhani timu nzima ilicheza kwa asilimia 100, lakini penalti zimetuangusha. Tunarudi nyumbani,” alisema Cheryshev.

Pia kocha huyo alisema mashabiki wa nchi hiyo hawakuwaunga mkono katika maandalizi ya fainali hizo wakiwa na matarajio kuwa timu hiyo ingefungashwa virago mapema.