Safari ya Ufaransa Kombe la Dunia Russia ilianzia hapa

Muktasari:

  • Safari ya Ufaransa kujiandaa na fainali hizo ilianza miaka miwili iliyopita kabla ya Julai 15, mwaka huu kuhitimisha kwa kutwaa ubingwa katika mchezo mkali wa fainali dhidi ya Croatia.

Ufaransa imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, lakini haikuwa kazi rahisi kupata mafanikio hayo kama baadhi ya wadau wa michezo wanavyodhani.

Safari ya Ufaransa kujiandaa na fainali hizo ilianza miaka miwili iliyopita kabla ya Julai 15, mwaka huu kuhitimisha kwa kutwaa ubingwa katika mchezo mkali wa fainali dhidi ya Croatia.

Timu hiyo ilipata ushindi wa kishindo katika mchezo huo baada ya Croatia kulala mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, Russia.

Ufaransa ilianza kujiandaa na fainali hizo mwaka 2016, baada ya kumalizika fainali za Euro 2016, ambapo ilitolewa kwa penalti na Ureno.

Hii ilikuwa ni miaka miwili tangu kocha Didier Deschamps na vijana wake waliposhindwa kutimiza ndoto ya kutwaa ubingwa wa Euro 2016 wakiwa wenyeji wa fainali hizo zilizofanyika jijini Paris.

Baada ya mchezo huo wa fainali ya Euro 2016 uliopigwa Uwanja wa Stade de France, Deschamps, alibadili mtazamo na kuelekeza akili yake katika maandalizi ya kutwaa Kombe la Dunia 2018.

Ilikuwa ni safari ya miaka miwili ambayo hakuna anayeweza kuanza isipokuwa mwenye malengo na dhamira ya kweli.

Deschamps alibadili wachezaji kadhaa wakati wa mechi za kufuzu, hii inaonyesha alijiandaa kwa safari ndefu ndio maana hatimaye aliikamilisha jijini Moscow, Russia kwa kutwaa Kombe la Dunia ikiwa imepita miaka 20 baada ya mwaka 1998 kutwaa taji hilo kwa mara ya mwisho.

Katika fainali hizo, silaha za Deschamps zilikuwa kwa kipa na nahodha Hugo Lloris, ambaye licha ya kufanya makosa machache, lakini alijitahidi kufanya vyema katika mechi zote saba ilizocheza Ufaransa.

Lloris alilinda vyema lango la Ufaransa, akishirikiana na mabeki wa kati Raphael Verane na Samuel Umtiti.

Mbali na wachezaji hao, kocha huyo anajivunia utendaji kazi mzuri baina ya N’Golo Kante na Paul Pogba katika safu ya kiungo ambao walipenyeza mbele mipira kwa akina Antoine Griezmann.

Ingizo jipya katika kikosi hicho, mshambuliaji chipukizi Kylian Mbappe (19), kuliifanya Ufaransa kuwa tishio akiungana na wachezaji Florian Thauvin, Olivier Giroud, Nabil Fakir na Ousman Dembele.

Giroud licha ya kucheza dakika 546 hakufunga bao tofauti na Mbappe ambaye licha ya kucheza kwa mara ya kwanza fainali hizo alifunga mabao manne.

Mbappe alianza kuonyesha umahiri katika mechi kati ya Ufaransa na Argentina alipoisambaratisha ngome ya Argentina akifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-3.

Katika mchezo wa fainali, Mbappe aliendelea kuwa tishio na chachu ya ushindi wa Ufaransa na kumpa wakati mgumu kipa Danijel Subasic wa Croatia.

Shughuli pevu ya Mbappe, chipukizi ambaye wakati mechi hiyo inachezwa alikuwa anatimiza miaka 19 na siku 207 ilikuwa mwiba kwa mabeki wa Croatia ambao walishindwa kudhibiti makali yake.

Makocha na wachambuzi wengi wa soka wanaamini Mbappe atakuwa Pele mpya kama ataendeleza umahiri alioonyesha kwenye fainali za mwaka huu za Komne la Dunia.