Salha: Mwanamke aliyeanza siasa akiwa na umri wa miaka 18

Unapozungumzia wanasiasa vijana waliomo kwenye Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) bila shaka Salha Mohamed Mwinjuma ni miongoni mwao.

Salha Mohamed Mwinjuma ni mwakilishi wa Viti Maalumu wa anayewakilisha vijana kwenye Baraza hilo.

Safari yake ya siasa aliianza akiwa na umri wa miaka 18, na mwaka 2014 alimaliza masomo yake ya diploma ya Uhusiano wa Kimataifa na mwaka 2015 akawania viti maalumu na hatimaye kufanikiwa kuingia kwenye Baraza hilo akiwakilisha vijana kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Mama huyo mwenye mtoto mmoja anasema kuwa alianzia harakati zake kwenye umoja wa vijana wa CCM mwaka 2012 kabla ya kujitosa rasmi mwaka 2015 baada ya kuona anaweza kusimama na kutetea vijana na wanawake.

Anasema alipata wakati mgumu kueleweka na jamii, lakini vijana na wanawake baadhi walimuelewa na sasa wanamuelewa zaidi.

“Haikuwa kazi rahisi kwa wakati ule nilikuwa mdogo nina miaka 18 tu, nimejikita kwenye siasa nikiwa sina utani hata kidogo, kwa kweli wengi hawakunielewa wachache waliielewa kazi ninayofanya ambao walizidi kunipa moyo wa kusonga mbele, ”anasema Salha.

Anazitaja changamoto alizokutana nazo katika hatua za awali kama mbunge mwanamke ni pamoja na kukatishwa tamaa hususani na wanaume ambao wamekuwa wakifanya siasa kwa muda mrefu.“Sikupata shida kukabiliana nazo kwa sababu zinaanzia ngazi ya chini na tangu nawania Ubunge nilijua nitakutana nazo.

“Ninachofanya ni kuhakikisha najifunza kila siku, kwa wanaosema ya kujenga na kubomoa lengo ni kuwajua wote na kwenda nao sambasamba ka sababu mimi ni kiongozi sasa siwezi kukwepa changamoto, ”anasema.

Anasema wanawake wengi wanafeli kwa sababu wanaume wameshawapima na kujua udhaifu wao kwa miaka mingi wakikatishwa tamaa kidogo wanarudi nyuma.

Mwinjuma anasema hatarajii kugombea jimbo kwenye uchaguzi wa 2020 kwa sababu anataka kujifunza zaidi.

“Nitagombea tena nafasi hii niliyonayo sasa, nataka kujifunza zaidi kabla sijaingia kwenye mikikimikiki ya kuwania jimbo, ”anasema.

Anasema anataka amalize masomo yake ambapo anachukua shahada ya uhusiano wa kimataifa, hivyo anaepuka kuchanganya mikiki ya jimboni na masomo.

Anayataja malengo kuwa ni kuhakikisha anaowaongoza au aliochukua dhamana yao wanamuelewa na kujenga imani nao, ikiwa ni pamoja na kutekeleza anachowaahidi kwa kuyapeleka bungeni malalamiko yao ya kiserikali.

“Sababu kubwa ya mimi kuwa Barazani ni wao, hivyo nafanya kazi yao, ”anasema ka kujiamini Salha.

Salha anasema majukumu yake ya kazi hayaingiliani na familia kwa sababu wanafahamu anafanya nini na atakuwa wapi kwa wakati gani.

“Mume wangu na familia yangu yenye mtoto mmoja wanafahamu ratiba ya kazi zangu, kuna wakati nachelewa kurudi nyumbani kutokana na majukumu na wapo wananielewa, ”anasema.

Anafafanua kuwa licha ya uwakilishi wake kuorodhesha anawakilisha vijana, lakini hajawaacha nyuma wanawake pia.

Anasema huwa anakutana nao na kuangalia namna ya kuwapa mafunzo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na wapo waliofanikiwa kupitia vikundi hivyo.

“Nasimamia kuhakikisha wanapata mitaji, kama mapema wiki hii nimekuwa na wafugaji wa nyuki wa eneo la Jambiani na Makunduchi nikiangalia miradi hiyo ambayo tuliapa mafunzo na wamefanikiwa sana kupata asalia ya kutosha, ”anasema.

Anasema mafanikio ya vikundi ndiyo kitu anachojivunia kwa sababu watu waliokupa dhamana wanapofanikiwa unapata nguvu ya kusonga mbele.

Salha anajinasibu kuwa bado yupo sana kwenye siasa, “Ninaweza kusema ndiyo kwanza naanza, wananchi watarajie makubwa kutoka kwangu.