Shule za ufundi suluhisho la ombwe la ajira nchini

Muktasari:

  • Hili ni moja ya mambo ambayo huonesha upande wa pili wa Edward Lowassa na uimara wake kwenye masuala ya uongozi na usimamizi. Wakati wa kampeni hiyo mara kadhaa nilijitokeza hadharani, si kuipinga, bali kushauri kuwa ingeliendana na ujenzi wa shule moja ya ufundi katika kila kata.

Kuanzia miaka ya 2006 – 2008, Serikali ya Tanzania iliyokuwa chini ya Jakaya Kikwete na Edward Lowassa ilifanya kazi kubwa ya kujenga shule za sekondari za kata na kampeni ya ujenzi wa shule hizo ilikuwa ni ya nchi nzima.

Hili ni moja ya mambo ambayo huonesha upande wa pili wa Edward Lowassa na uimara wake kwenye masuala ya uongozi na usimamizi. Wakati wa kampeni hiyo mara kadhaa nilijitokeza hadharani, si kuipinga, bali kushauri kuwa ingeliendana na ujenzi wa shule moja ya ufundi katika kila kata.

Hata hivyo, na kama ilivyo ada ya taifa letu, wakati wa kampeni za wakubwa, sauti za wadogo hazisikilizwi kabisa.

Hoja nilizozitoa wakati ule, za kupigia upatu shule za ufundi za kila kata kuliko shule za sekondari katika kila kata au hitaji la kuwepo kwa usambamba wa sekondari za kata na shule za ufundi za kata, ziko hai na hazijafa na ninachoona zinazidi kuchomoza na kuwa na nguvu zaidi.

Wakati ule (miaka 13 iliyopita) nilieleza kuwa, msingi wa ujenzi wa shule za ufundi za kata unatokana na uzoefu wangu wa mwaka mmoja niliokuwa nao katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo nilishuhudia maelfu ya wanafunzi wakitumia muda wao wote kukaririshwa dhana mbalimbali za kimasomo na kitaaluma kuliko kuzielewa, na jambo hilo likionekana ni kitu cha kawaida sana.

Lakini, nilianza kukutana na watu wengi wenye ndugu zao waliohitimu vyuo vikuu wakaishia kukaa mitaani kwa miaka mingi bila kupata kazi, hapo ndipo nikagundua kuwa mfumo wetu wa elimu una matatizo makubwa na tunapaswa kuuboresha au kuwekeza katika mfumo wa ziada wenye tija.

Shule ya ufundi kila kata

Kama tangu mwaka 2005 tungeliwekeza kwenye ujenzi wa shule moja ya ufundi katika kila kata ya Tanzania tungeliweza kuwa na vyuo 4,000 na ushee nchi nzima. Tungeliweka utaratibu vyuo hivi vipokee wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kushindwa kuendelea na sekondari kwa sababu mbalimbali pamoja na wale waliohitimu kidato cha nne wanaporudi kwenye likizo ndefu ya kuamua kama wangelienda kidato cha tano au la.

Shabaha ya taifa letu ingelikuwa kila kijana anayehitimu shule ya msingi na kukosa nafasi au kushindwa kuendelea na sekondari, lazima ajiunge kwenye shule ya ufundi ya kata.

Na shabaha nyingine ingelikuwa vijana wote wanaohitimu darasa la saba na kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari sharti waende kusoma kwenye shule hizi za ufundi za kata mara wanapohitimu kidato cha nne wakisubiri mustakabali wa majibu ya mitihani yao.

Madarasa 10 – 14 pamoja na ofisi 2 – 4 za walimu ambazo tumejenga kwenye kila kata ya nchi hii ili kutoa elimu ya sekondari, vingeliweza kabisa kuwekezwa kwenye shule za ufundi nchi nzima, au shule hizohizo za sekondari tungezitumia kama shule za ufundi, wanafunzi wa sekondari wanasoma asubuhi hadi mchana na wanafunzi wa ufundi wanaingia majira ya jioni.

Kupanga ni kuchagua na mfumo huo ungelikuwa rahisi sana, kwa hiyo tungelikuwa na shule za sekondari na shule za ufundi kwa wakati huohuo au kwa lugha rahisi tungelikuwa na shule za sekondari mpya 4,000 na wakati huohuo tunazo shule za ufundi 4,000 pia katika majengo hayohayo.

Tatizo la walimu

Wakati fulani mwaka 2006 nilijadiliana wazo hili na mwalimu wangu mmoja wa UDSM ambaye alilitupilia mbali, hoja yake ilikuwa ya kwamba, hakutakuwa na uwezekano wa kupata walimu wa shule za ufundi ikiwa walimu wa shule za sekondari peke yake hawatoshi, na serikali imeshindwa kuwaajiri kwa idadi inayohitajika.

Nilimwambia kwamba, shule za ufundi za kila kata hazitaajiri wakufunzi wala kuhitaji bajeti ya Serikali kufanya jambo hilo.

Mawazo yangu yalikuwa kwamba, shule hizi zinahitaji kutumia wakufunzi watakaopewa semina ya muda mfupi kutoka miongoni mwa mafundi waashi, ushonaji, umeme, uezekaji, magari, baiskeli na wa zana mbalimbali za kilimo, ufugaji, uvuvi na kila aina ya ufundi, ujuzi au stadi – mafundi wenye stadi, taaluma, ujuzi na uwezo huo wametapakaa kila kona ya nchi yetu na hasa kwenye hizohizo kata.

Kwa mtazamo wangu wakati huo, na kwa mfano halisi wa kijijini kwangu, tulikuwa na mafundi ushonaji ambao walikuwa wanajitolea muda wao kufundisha vijana wapya namna ya kushona na tena kwa kutumia zana zao bila kupokea malipo yoyote.

Wazalendo hao wangelisakwa kila kitongoji, kijiji na kata kungelikuwa na idadi kubwa ya wakufunzi ambao wangelihudumu kwenye shule za ufundi za kila kata.

Kila kata ingelitakiwa kutoa sehemu ya mapato yake ya kila mwezi kuajiri Mkufunzi mkuu mmoja wa shule husika ya ufundi ya kata na mkufunzi huyo angelifanya kazi pamoja na wengine wanaojitolea ambao wangelikubali kulipwa posho kidogo ya kila mwezi ambayo ingelitokana na mchango wa wanafunzi wanaosomea kwenye shule hizi za ufundi.

Mahitaji ya vifaa, uendeshaji

Kiuzoefu, wilaya nyingi za Tanzania zinamiliki kata takribani 10 – 30, kama ndivyo basi, mabaraza ya madiwani ya halmashauri zote nchi zima yangelitakiwa kutenga asilimia kadhaa ya bajeti yao ya kila mwaka kununua mahitaji maalum kwa ajili ya shule hizi za ufundi, mfano wa vyerehani, vifaa vya mafundi waashi, ufundi wa magari, umeme, mota na kila aina ya ufundi – jambo hili lingeliwezekana.

Leo mwaka 2018 tungelikuwa na shule za ufundi zaidi ya zilizotapakaa kwenye kila kata na huenda zingelikuwa na walimu waliobobea zaidi kwa sababu mpango huo ungelikuwa umekua sana. Kama kila shule moja ya ufundi ingelitoa wahitimu takribani 200 kila mwaka, shule 4,000 za ufundi nchi nzima zingelikuwa zimetoa mafundi wenye ujuzi wa kuweza kujiajiri wapatao milioni 10.4. Mradi huu peke yake ungeliwapa ujuzi na ajira vijana zaidi ya milioni 10 na ungelikuwa ni mpango mkubwa sana wa kitaifa kuliko mipango yote iliyowahi kubuniwa tangu enzi za uhuru.

Leo, tunashuhudia mamilioni ya vijana wa Kitanzania wanahitimu masomo yao juu ya masuala mbalimbali kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu na mamilioni ya vijana hao wanakaa bila ajira kwa kipindi kirefu, wengine hata zaidi ya muongo mmoja kwa sababu tu tumekataa kufikiri juu ya uhalisia unaolikabili taifa letu.

Kila mwaka, vijana milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira nchibni, serikali yetu na sekta binafsi zinaweza kutoa ajira za uhakika kwa nguvu kazi ya vijana 50,000 – 100,000 tu kwa mwaka.

Zaidi ya asilimia 90 ya vijana wanakosa ajira rasmi na wanaanza kutangatanga. Kumbe, mkakati huu wa shule za ufundi ungeliweza kuzalisha ajira milioni moja kila mwaka na kukata tatizo la ajira nchini.

Mawazo ya wazungu

Wengi wetu tukisoma mawazo na maandishi na uchambuzi wa namna hii, unaogusa namna tunavyopaswa kutatua matatizo yetu, huwa tunakimbilia na kutafuta kujua mawazo haya yametolewa na mtu wa rangi gani.

Serikali zetu za Afrika zimekuwa zikiendesha nchi kwa mifumo ya kimagharibi na kuacha kabisa kujaribu kujenga utaratibu wa kinyumbani na kikwetu ambao unaweza kuzigusa jamii kirahisi na kutatua matatizo yetu bila itifaki na mizunguko isiyokuwa na maana yoyote.

Kama serikali ya Tanzania iliweza kufanya na kusimamia maamuzi ya uanzishaji wa shule za kata, inashindwa vipi kufanya uamuzi mwingine, wa kuzipanua shule hizo na kuziongezea programu ya pili ya uendeshaji wa shule za ufundi kwa kila kata?

Nauliza swali hili kwa sababu mafanikio ya kuanzisha shule za ufundi kwa kila kata yangelikuwa makubwa mara 100 kuliko ambayo tumeyapata tangu tuanzishe mfumo wa sekondari katika kila kata.

Sanasana mfumo huo wa sekondari za kata peke yake umesaidia kutoa vijana wengi ambao wameelimika sana lakini hawana kazi, kumbe mfumo wa shule za ufundi za kata ungelifanyika pia wakati ule na mifumo yote hii ikafanya kazi sambamba leo tungelikuwa na mamilioni ya vijana wana shahada za chuo kikuu na wamejiajiri mara moja bila kujali ikiwa walichokisomea chuo kikuu kina ajira mtaani.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF. Simu; +255787536759 Barua Pepe; [email protected])