Siasa zetu zijenge umoja wa kitaifa, la sivyo tutayumba

Muktasari:

  • Ni hali ya hatari. Mtu, anayeutafuta utukufu wake na usalama wa familia yake, hawezi kujenga umoja wa kitaifa.

Tunaanza kuyumba. Tunaacha hoja ya msingi ya kujenga umoja wetu wa kitaifa, tunaanza kukimbilia vyama vya siasa.

Wimbi kubwa la “vijana” kuhama vyama vyao vya siasa na kukimbilia chama tawala linatisha. Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanasema kwamba watu wenye uchu wa madaraka wakifikisha miaka 45 bila kufanikiwa kupanda ngazi za juu kwenye utawala wanaanza mbinu za kufa na kupona na hakuna tena cha itikadi, sera wala uzalendo; ni tumbo lake, familia yake na utukufu wake hata kama ni kula haramu.

Ni hali ya hatari. Mtu, anayeutafuta utukufu wake na usalama wa familia yake, hawezi kujenga umoja wa kitaifa.

Uongozi wa awamu zilizopita haukutoa nafasi kwa wapinzani na wale waliokuwa na harufu ya upinzani, hata ukihama chama, unakaa benchi kwa miaka, sasa hivi mambo yamebadilika. Nafasi zinatolewa hata kwa wale ambao siku za nyuma kidogo ilielezwa kwamba watakaribishwa kwenye zizi lakini mikia yao imekatika, hivyo kulikuwa na hatari ya kutengwa kwenye zizi. Kwa hali hii iliyojitokeza, hatuwezi kusema kwamba vijana wetu wanahama vyama vyao kwa nia ya kulijenga taifa letu, bali kujijenga wao na utukufu wao. Hii ni hatari kwa taifa changa kama letu.

Tunataka au tusitake, iwe mvua liwe jua, kitu muhimu si vyama vya siasa, makabila yetu wala imani zetu za kidini; muhimu ni umoja wetu wa kitaifa.

Bila umoja wa kitaifa, sote hatuko salama. Matajiri, masikini, wazee, vijana na viongozi wa dini hawatakuwa salama. Watawala nao hawatakuwa salama na vizazi vijavyo havitakuwa salama.

Tunaposhiriki kulijenga taifa letu, ni muhimu kusimamia na kuitetea hoja yetu ya msingi. Umoja wetu wa kitaifa. Tusiyumbishwe na wajanja wachache wenye ajenga za siri za kuibua ushindani bandia wa vyama vya siasa (kikiwa kisingizio chenye ushawishi mkubwa) na kujificha nyuma ya kumuunga mkono Rais Magufuli.

Wachache hawa, lakini wenye nguvu za kutisha hawana nia njema kwa taifa letu. Tukisimama imara na kuuweka ujinga nyuma yetu, tutawashinda!

Baada ya Uhuru wetu, kazi kubwa ilikuwa ni kuimarisha umoja wa kitaifa, kupandikiza moyo wa kizalendo kwa watanzania wote. Maana mkoloni alikuwa amefanya kazi ya kuwafanya watanzania kujichukia, kuchukia mila zao, miungu wao na hata lugha zao. Mkoloni alitawala nchi, miili yetu na fikra zetu! Jukumu hili la kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo lilikuwa ni la kila Mtanzania mwenye upeo wa kuona mbali. Mwalimu Nyerere, kwa kutumia chama cha siasa kilichoshiriki kuleta uhuru wa taifa letu, alijitahidi kujenga umoja na kupandikiza uzalendo. Tanu na baadaye CCM, kwa wakati ule kilikuwa na picha tofauti. Kutojiunga na chama, kulionekana kama usaliti. Sababu kubwa ikiwa kwamba wakati wa mkoloni, kuna vyama vilivyounga mkono wakoloni. Kuna vyama vilivyotaka wakoloni waendelee kutawala. Lakini, pia kulikuwa na vyama ambavyo, havikulenga kujenga umoja wa kitaifa, vilitaka Tanzania, ibaki ni ya watu weusi tu! Vyama hivi vilitaka kuifuta historia, kitu ambacho ni kigumu kufanyika.

Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, iliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere, chini ya Azimio la Arusha, lengo lake kubwa ilikuwa ni kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo. Mwalimu, alitaka kutufikisha katika hatua ya kuutanguliza utaifa, kabla ya kitu chochote kile. Alitaifisha mashule na mahospitali ya mashirika ya kidini, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki sawa. Wajinga na wenye ufinyu wa uchambuzi, wanaeneza propaganda za kiwendawazimu kwamba Mwalimu, alifanya makosa kutaifisha mali na kuanzisha ujamaa.

Vijiji vya ujamaa, Jeshi la kujenga taifa na Azimio la Musoma, vililenga kumtengeneza Mtanzania mwenye mshikamano na mzalendo. Wakati ule tulikuwa na chama kimoja cha siasa. Ingawa si watu wote waliojiunga na chama cha siasa, lakini wengi walikuwa na imani juu ya nia ya chama hicho cha siasa. Na kusema kweli chama hicho kiliangalia maslahi ya kila Mtanzania – ni tofauti kabisa na sasa hivi tunaposikia misemo ya CCM ina wenyewe. Na kweli kimatendo ni kwamba CCM ina wenyewe! Na kwa fikra potovu, fikra ambazo ni lazima zifanyiwe kazi kubwa, ni kwamba hawa wana CCM, wanafikiri wao ndo watanzania peke yao na wana haki zaidi ya wengine!

Mwalimu, alitengeneza falsafa ya chama kimoja. Aliielezea falsafa yake na watu wakaielewa. Watanzania walio wengi walipenda sana mfumo wa chama kimoja, maana waliona umuhimu wake. Lakini hasa waliona umuhimu wa chama cha Mwalimu, ambacho kilikuwa na lengo na kuunda umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo. Upepo wa kuanzisha vyama vingi vya siasa ulioikumbwa dunia nzima, ulipoingia Tanzania, asilimia 80 ya watanzania walipenda nchi yetu kuendelea na mfumo wa chama kimoja. Asilimia 20 tu ndo walikubali mfumo wa vyama vingi.

Bahati mbaya tulikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi kabla ya kuimarisha umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli. Vitu hivi viwili ni vigumu kuvijenga katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Au niseme kwa maneno mengine, kwamba mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, unafaa kwa nchi ambayo imefanikiwa kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli si chini ya miaka 100. Nchi changa kama yetu ni vigumu kuendesha siasa ya vyama vingi bila kuleta mtengano na wakati mwingine vita au mapambano ya dola na vyama ambavyo havikushika madaraka.

Wakati wa mkoloni, kigezo cha kupima uzalendo wa mtu ilikuwa ni uanachama wa chama cha siasa, na hasa chama kilichokuwa kikilenga kuleta ukombozi, kama Tanu, chama ambacho baadaye kiligeuka na kuwa CCM, baada ya kuungana ASP cha Zanzibar. Mtizamo huu ambao ulikuwa na maana wakati ule, umeendelea leo hii. Watu wengi, na hasa wale wanachama wa CCM, bado wanafikiri kigezo cha uzalendo ni kujiunga na chama cha CCM. Na wana mawazo kwamba yule aliye nje ya CCM ni msaliti!

Tatizo hili limejitokeza kwa vile wimbi la kuanzisha vyama vingi lilikuja kabla ya wakati wake. Lilikuja bila maandalizi! Kwa upande mmoja ni vizuri na kwa upande mwingine ni vibaya. Ni vizuri kwa sababu chama kimoja, kinawafanya watu kuwa vipofu na kushindwa kuona ukweli wa mambo katika jamii. Vyama vingi vya siasa vinasaidia kufichua dosari na kukifanya chama kinachotawala kisijisahau. Lakini kwa upande mwingine ni vibaya maana, kinachotokea kuanzisha vyama vingi bila msingi imara, matokeo yake ni kuendeleza chama kimoja, kama ilivyo sasa hivi kwa CCM.

Lakini, pia kuna ukweli wa maisha kwamba daima mambo yanakwenda kwa kuunganisha chanya na hasi. Bila kuwa na vitu viwili vinavyopingana na vigumu sana kuwa na matokeo ya kitu chochote kile. Hiyo ndiyo sayansi. Kwamba una chanya na hasi. Si upinzani lakini ni kuwa na mawazo mbadala ili kusukuma mambo, au ili kuunganisha chanya na hasi ili kupata matokeo. Ukiwa chanya peke yake, hakuna kitakachokwenda, na ukiwa na hasi peke yake hakuna kitakachokwenda. Sipendi kusema kwamba CCM ni chanya na vyama vya upinzani ni hasi, ni mfano wa kujipima kwa wakati uliopo. Inaweza kutokea hata CCM ikawa ni chama cha upinzani na vyama vya upinzani vikawa ni tawala, kosa lisijirudie.

Kama tungelikuwa tumefikia ukomavu wa kisiasa, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, chama cha CCM, kingevunjwa kwanza, na vyama vyote vikaanza upya. Tungeanzisha vyama ambavyo nia na lengo kubwa lingekuwa ni kujenga taifa letu kwa kuleta mshikamano na kuimarisha uzalendo. Vyama vingekuja na sera mbalimbali za kutimiza lengo hilo. Kwa vile CCM, inatokana na vyama vilivyoshiriki kumfukuza mkoloni na ni chama kilichoendelea kutawala hadi tunaingia mfumo wa vyama vingi, kinapata upendeleo wa kihistoria.

CCM, ambayo ilitokana na Tanu, lengo lake la msingi lilikuwa ni kupambana na mkoloni na kuleta uhuru. Kazi hii ilifanyika vizuri. Baada ya hapo CCM, iliendelea kufanya kazi ya kuimarisha uhuru wetu. Kwa maoni yangu mimi, kazi hii ingeendelea zaidi ya miaka 50, kabla ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa. Maana, tungeanza na mfumo wa vyama vingi tukiwa na agenda tofauti na ile ya ukoloni.

Nyakati hizi tulizomo, ni vigumu chama cha siasa kujenga umoja wa kitaifa. Tunahitaji chombo cha kujenga umoja wa kitaifa. Tunahitaji chombo cha kuwakusanya Watanzania wote bila kuangalia mapenzi na imani yao kwenye vyama. Mfano mzuri ni ndege yetu mpya ya Dreamliner. Ni kati ya kitu kinachowaunganisha Watanzania, na kila mtu amefurahi na kuishangilia. Nilipata bahati ya kuwa abiria wa kwanza wakati ndege hii ikiianza safari zake. Wakati wasafiri wengine tulikuwa tukifurahi ndege yetu ya Kitanzania, wana CCM walikuwa wamevalia sare zao wakikitukuza chama chao na kuuonyesha kwa uwazi kabisa tofauti kati yao na wengine ambao hawakuwa na uniformu za kijani na wakati mwingine wakipenyeza maneno ya kichokozi na wengine ni watu wenye majina makubwa. Wakati Rais anabuni vitu vya kutuunganisha kama kataifa, chama chake bado kinaendelea kuwatenganisha watu. Wakati inajulikana wazi kwamba ndege hii imenunuliwa kwa kodi za watanzania wote, wenye vyama na ambao hawana vyama, sare za CCM na majigambo ya CCM yana nafasi gani katika uzinduzi wa kitu cha kitaifa? Dreamliner, inatuunganisha, lakini CCM, inatutenganisha. Hili ni baya kabisa. Hata na hii hamahama ya vyama ni kuwatenganisha watanzania badala ya kuwaunganisha.

Bila kuwa na lengo mmoja kama taifa, mfano kama lengo letu la zamani la kumfukuza mkoloni, ni vigumu kuyafikia maendeleo ya kweli. Ni lazima tuwe na chombo cha kutuunganisha, kiasi kwamba Chadema, ikiingia madarakani ifanye kazi na Watanzania wote, bila kuangalia imani zao za vyama na dini zao. Ikitawala TLP, ifanye kazi na Watanzania wote bila kuangalia imani zao za vyama na dini zao. Ikitawala CUF ifanye kazi na watanzania wote bila kuangalia imani zao za vyama na dini zao. Na ikitawala CCM, kama inavyofanya sasa hivi ifanye kazi na Watanzania wote bila kuangalia imani na itikadi zao za vyama. Ujenzi wa umoja wa taifa letu ni lazima utajwe kwenye katiba mpya. Vyovyote vile tunahitaji Katiba mpya.

Tunahitaji chombo cha kututoa usingizini na kutufundisha kwama chama cha siasa, si kitu cha kwanza katika taifa, utaifa ndicho kitu cha kwanza na vingine vinafuata. Leo hii chama ndicho kitu cha kwanza na mengine yanafuata. Huku ni kupotoka!

Na, Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122