Tuesday, September 11, 2018

Simulizi ya walemavu wa akili waliosoma na kuajiriwa

 

By Salome Gregory, Mwananchi

Zama za walemavu kutazamwa kama mizigo zimepita. Wakiwezeshwa, walemavu wanaweza kufanya makubwa kwa jamii.

Nani kwa mfano anaweza kudhani kama mtoto mwenye mtindio wa ubongo anaweza kusoma hadi kufikia hatua ya kuajiriwa?

Zamani watoto hawa na wengineo wenye ulemavu wa aina mbalimbali, walibaki nyumbani, hawakupata fursa za elimu na kibaya zaidi walikuwa wakifichwa.

Hata hivyo, kwa Abdallah Kimweri (25) na Theofan Remmy (23) waishio wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga, wana habari ya kusisimua. Hawa wana tatizo la mtindio wa ubongo, lakini leo wameajiriwa.

Simulizi yao

Vijana hawa wamefanikiwa kusoma katika Shule maalumu ya wanafunzi wenye ulemavu Irente iliyopo mkoani Tanga na kupata ajira zinazowasaidia kumudu mahitaji yao ya kila siku.

Abdalla na Thefan wamekua wanafunzi wa kwanza kupata ajira maalumu tangu kuanzishwa kwa shule hiyo inayofundisha kwa kutumia mbinu maalumu za kuwazesha wanafunzi wa aina hiyo kufanya kazi kwenye mazingira.

Abdalla ameajiriwa katika hifadhi ya Irente tangu mwaka 2014 akiwa na jukumu la kutunza mazingira. Baba yake, mzee Mohammed Baweni anasema ana watoto wawili wenye mtindio wa ubongo kati ya 11 alionao.

Baweni anasema, watoto wake Abdallah na Ally walizaliwa bila ulemavu wa aina yoyote. Baada ya Abdallah kufikisha miaka nane na Ally kufikisha miaka sita kufikisha miaka sita walipatwa na homa kali kwa nyakati tofauti na baada ya hapo ulemavu ulijtokeza. Wakati huo wote walikua wakisoma katika Shule ya Msingi Kana iliyopo Tanga Mjini kabla familia haijahamia Lushoto. Ingawa Abdallah ana uwezo wa kuongea vema, lakini muda wote wa mahojiano alikua akisikilizwa kwa umakini. Alipoanza kusema majibu yake yalikuwa mafupi huku akitabasamu muda wote.

Abdallah kwa uhalisia anapata kiasi kidogo kama malipo ya kazi yake, lakini inampa furaha kuona anaweza kusaidia familia yake. Anatoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapa nafasi watoto wao wasome.

Theofan ni mwanafunzi wa pili kupata ajira kutoka Irente bada ya kuajiriwa Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (Sekomu). Chuo hicho kina idara ya Elimu, Sayansi na Sheria. Ameajiriwa chuoni hapo kama mtunza bustani tangu Agosti mwaka 2017.

Selina Msumari ni mama yake Theofan. Anasema baba yake Theofan alimtelekeza mtoto alipofikisha miaka minne baada ya kugundua kuwa alikuwa mlemavu.

“Maisha yangu yote sijawahi kuwa na kazi ya kudumu na nina familia ya watoto wawili. Bila msaada wa walimu Irente kuruhusu Theofan apate usafiri na kusoma bure na baadaye kufanya jitihada za kumtafutia kazi, mwanagu asingefika hapa leo,” anasema Selina.

Kipato cha Selina zaidi kinategemea kazi za vibarua ikiwemo kufulia watu nguo zao, kulima mashamba na wakati mwingine kuwachotea maji.

“ Nina furaha kuona mwanangu ana kazi kwa sasa. Haikua rahisi kumudu gharama za kumuwezesha kusoma Irente kwa zaidi ya miaka 10. Tofauti na kujifunza ujuzi mbalimbali wa kimaisha mwanangu kwa sasa anaweza kufanya vitu tofauti tofauti katika jamii,’ anaeleza.

Theofan anaweza kutunza pesa zake sasa na anafahamu maeneo mbalimbali ya Lushoto na hana woga wa kukutana na watu kama ilivyokua awali.

Akipata mshahara wake analipa Sh40,000 kodi ya nyumba huku akiweka Sh40,000 kama akiba. Pia anatumia Sh20,000 kutatua mahitaji yake madogo madogo.

Theofan anapendelea kutumia vifaa mbalimbali vya kisasa kama vile simu anayosema inamrahishisha mawasilaino na mama yake maana mara nyingi hujisahau kurudi nyumbani hivyo mama yake humpigia kumkumbusha kurudi.

Irente na wanafunzi wenye ulemavu

Lucy Mwinuka ni mratibu wa programu za kuwafikia wanafunzi majumbani kwao kupitia shule ya Irente. Shule hii inaendeshwa kwa ushirikaino wa Serikali na Kanisa la Kilutheri Tanzania.

Lucy ndiye aliyemtafutia kazi Theofan baada ya kuona jitihada zake za kila siku akiwa shuleni.

Anasema si rahisi kuwashawishi waajiri kuwa watu wenye ulemavu nao wana uwezo wa kufanya kazi kama wengine, hivyo kuwapatia nafasi inakua changamoto kubwa.

‘’Kupitia programu ya kutembelea nyumbani, inawawezesha wazazi au watoa huduma kujifunza namna mbalimbali za kuwahudumia watu wenye ulemavu. Vilevile kuongeza uelewa wa masuala ya ulemavu kwenye jamii na kuondoa imani potofu,’’ anasema.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Irente Rainbow, Yassin Sheghalilo anasema kuwa Abdallah na Theofan wameiletea shule sifa nzuri na sasa wanatumika kama mfano mzuri kwa jamii.

Anasema, kuwa wanafunzi wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo hawafanyi mitihani ya kitaifa bali hujifunza stadi za kimaisha kwa kutumia hatua tatu tofauti wakati wa kujifunza.

Anasema wanafunzi hawa hufundishwa namna ya kujitunza kwa kwa kufanya usafi binafsi, kusaidia wazazi wao na watu wengine kwenye jamii yao.

Lakini pia namna ya kutunza fedha zao na kuangalia fursa mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri.

Shule ya Irente Rainbow ina miradi mbalimbali inayofunza aina mbalimbali za ujuzi ikiwamo kutengeneza batiki, ufugaji, kutengeneza mapambo au viatu kwa kutumia shanga, ufundi seremala na ufundi mwingine. Shule hiyo ina walimu saba na wanafunzi 43. Moja ya mahitaji yao ni kuongezewa walimu wawili.

-->