UCHAMBUZI: Sitaki, nataka ya Kubenea ya Katiba mpya

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amekubaliana na Rais John Magufuli kuwa huu si muda wa kuendelea na Katiba mpya, lakini ametofautiana naye hasa kuhusu hoja ya kutotenga fedha.

Kubenea alikuwa anazungumza hoja iliyotolewa na Rais Magufuli kwenye kongamano la mjadala wa “Siasa na Uchumi” lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo Rais Magufuli alisema: “Nafahamu hamu ya Watanzania kuwa na Katiba mpya ila sasa tunafanyaje? Twende na Katiba Pendekezwa au Rasimu ya Warioba.”

Rais Magufuli aliendelea: “Hapo ndipo ninapoona tuache kupoteza muda kutafuta majibu tuchape kazi. Tusitumie hela kuwalipa watu wakae vikao. Ni bora tukajenge reli. Kwa sasa sitegemei kutenga hela kwa ajili ya kuwapeleka watu kujadili katiba na kama kuna mtu anataka kutupa hela kwa ajili hiyo azilete, azilete tutajenga reli.”

Akizungumzia kauli hiyo, Kubenea alisema hakubaliani na sababu hizo kwa kuwa Katiba ni jambo la muhimu si kwa wananchi tu hata kwa Rais mwenyewe.

Alisema suala la Katiba linaweza kuahirishwa kwa sababu kadhaa, ikiwamo kupata mwafaka wa kitaifa kuhusu kipi kishughulikiwe kati ya Katiba Inayopendekezwa au Rasimu ya Warioba.

Anasema sababu nyingine ni nani wawe wawakilishi katika Bunge la Katiba, waende na Bunge zima la sasa au kuwe na Bunge Maalumu litakalojumuisha watu wengine mbalimbali.

Kubenea anasema suala la Katiba linatakiwa lifikiwe mwafaka wa kitaifa. Pia, hata Katiba Pendekezwa si mbaya kama inavyodhaniwa hoja iliyofanya wapinzani watoke kwenye ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba ni kuhusu muundo wa Serikali, kwamba kuwe na Serikali mbili au tatu.

Mbunge huyo hakusahau suala aliloliita chuki za kisiasa kwa viongozi wa upinzani kukamatwa, kufunguliwa mashtaka, kuzuiwa mikutano ya kisiasa na mashambulizi dhidi ya viongozi wa kisiasa kwamba taifa haliwezi kwenda kwenye Katiba mpya bila kupata mwafaka wa masuala haya.

Mbunge huyo alieleza kumhurumia Rais Magufuli kwa ugumu wa kazi ya urais na namna anavyolazimika kwenda chumba cha kulala na mafaili ambayo yote yanasubiri uamuzi wake.

Hata hivyo, alisema Katiba mpya itasaidia kumpunguzia Rais Magufuli mzigo wa kazi na kumpa nafuu zaidi ikiwamo kuacha kwenda na mafaili chumbani kwake.

Kubenea anasema Rais anakuwa na kazi nyingi kwa kuwa Katiba iliyopo imempa madaraka makubwa na mengi, yanayomfanya aendelee na majukumu yake hata akiwa chumbani.

Anataja baadhi ya majukumu hayo ni kuteua mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Pia, japo Bunge lina madaraka, lakini Rais naye ana madaraka ya kulivunja Bunge ambayo ni makubwa kuliko Bunge.