TFF, Serengeti Boys msibweteke na hizi mechi za CAF-Cecafa

Muktasari:

Ninaipongeza Serengeti Boys pia kwa kuanza vema mechi zake za mashindano ya kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo yatakayofanyika nchini mwakani.

Sina sababu ya kuacha kuwapongeza wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys na benchi zima la ufundi chini ya Kocha Oscar Milambo kwa hicho tunachokiona.

Ninaipongeza Serengeti Boys pia kwa kuanza vema mechi zake za mashindano ya kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo yatakayofanyika nchini mwakani.

Japo tunafahamu kuwa Tanzania ina tiketi mkononi, lakini haizuii kupongeza kwa hapo ilipofikia.

Pamoja na kwamba mechi zinaendelea, na kesho wanacheza na Rwanda na matokeo yoyote hayawezi kuwaathiri kwa vyovyote.

Tumewashuhudia wakiwalaza Burundi mabao 2-1 na baadaye Sudan 5-0, inapendeza sana.

Pamoja na pongezi hizo lakini ninawatahadharisha wachezaji na benchi la ufundi la Serengeti Boys, kuhakikisha wanaongeza bidii mara dufu ili waweze kushinda mechi zote zilizosalia na kutwaa ubingwa huo.

Hata hivyo, ninalitahadharisha Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) pamoja na Serikali na kamati ya maandalizi kwa ujumla kuchukulia matokeo hayo mazuri kama chachu ya kuipa maandalizi ya uhakika zaidi ili timu hiyo, ili kinachofanywa leo kifanywe kwenye fainali za Afrika hapo mwakani.

Kwa kuwa mwakani tutakutana na timu bora zilizoandaliwa kwa uhakika ni vyema Serengeti Boys ikaandaliwa kwa umakini zaidi na kwa mechi nyingi ngumu kulinganisha hizi za CAF-Cecafa ambazo tunaziona kama si kipimo sahihi japo ni nzuri kwa kuiangalia timu nini inafanya na matarajio yake..

TFF na Kamati ya Maandalizi inapaswa kutekeleza ahadi za kuipa kambi ya maandalizi kwani ikiwemo kuipa mechi nyingi zaidi hasa mataifa ya Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi na hata nje ya Afrika.

Kila mmoja ameona kuwa vijana wetu wana vipaji vya kuzaliwa navyo lakini pengine kutokana na udogo wa umri wao au kutopata mazoezi ya kutosha bado wanafanya makosa mengi ambayo wakikutana na timu bora watafungwa kirahisi.

Matokeo ya CAF-Cecafa si ya kuvimbisha vichwa kwa kuwa timu nyingi ni kama hazikuandaliwa na wala kutoa ushindani kama ilivyo kwa Somalia, Eritrea, Burundi na timu zote za Sudan na Sudan Kusini.

Timu inashinda, lakini inashindana na nani? Je wachezaji wanapata ile hali ya mechi?

Ikumbukwe kuwa Ukanda wa Cecafa soka lake lipo chini hivyo kucheza mechi nyingi za timu za Cecafa tunadhani si kipimo sahihi kujiandaa na mashindano yajayo.

Tunaweza kujiaminisha kuwa Serengeti yetu iko sawasawa lakini kumbe hakukuwa na umakini na kupata matokeo ya kushangaza na kuanza kujiuliza kinachotokea.

Bila shaka tukitekeleza hili la maandalizi ya uhakika tangu sasa tutapata furaha isiyokoma na hapo tutapata mwanzo mzuri wa timu. Mechi za CAF-Cecafa ziwe sehemu muhimu ya maandalizi.

Ninarejea kuwapongeza wachezaji wa Serengeti Boys kwa hatua hii waliyofikia ya kuingia nusu fainali kwamba hawakopeshi kitu wapinzani wao wanapokuwa wabovu.

Hii inaonyesha kuwa wana kiu ya kufunga na ukiangalia mechi ile walifunga mabao 10, lakini wanashindwa kujipanga kung;amua mtego wa kuotea japokuwa ni nzuri mwamuzi anaweza kujichanganya.

Ninawatakiwa kila la kheri katika mechi zao lakini pia kudumisha nidhamu na utii kwenye timu na kufanya maandalizi ya maana na akili zao kuelekeza fainali za mwakani za AFCON 2019, Tanzania ikiwa mwenyeji.