TUONGEE KIUME: ‘Ushushu’ kabla ya kuoa ulikuwa na faida zake enzi hizo

Muktasari:

  • Kipindi hicho ilikuwa ni lazima kigori afanyiwe udadisi wa maana, ule wa kuzama ndani kabisa. Achunguzwe baba yake, wamjue, wajue tabia zake nje ndani, afuatie mama na usishangae mwendo huo ukafanyika hadi kwa shangazi na wajomba.

Waliobahatika kuishi enzi za analogia wanafahamu jinsi kuoa katika kipindi hicho ilivyokuwa shughuli nzito. Ilikuwa unaweza kuwa umepata mtu unayempenda kabisa lakini hadi apitishwe na wakuu wa familia ni lazima awe amekubalika kweli kweli.

Kipindi hicho ilikuwa ni lazima kigori afanyiwe udadisi wa maana, ule wa kuzama ndani kabisa. Achunguzwe baba yake, wamjue, wajue tabia zake nje ndani, afuatie mama na usishangae mwendo huo ukafanyika hadi kwa shangazi na wajomba.

Yaani kuoa kwenye enzi za analogia hakukuwa na tofauti na usalama wa taifa duniani wanavyotafuta maofisa wake.

Ila yote ile ilikuwa ni upande wa mwanaume kuhakikisha mtoto wao hapotei, anapata mke ambaye atakwenda kuwa kiranja mzuri wa nyumba—ukiwa na mke safi nyumba mbona itapendeza tu.

Sasa siku hizi, enzi za dijitali, kuoa kwa maana ya kupata mke imekuwa rahisi sana. Mke na mume wanakutana kwenye daladala, wanabadilishana namba za simu, wanawasiliana whatsapp siku mbili tatu, ya nne anakuja nyumbani, ya tano mnaita ndugu kadhaa mnaunda kamati, ya tano mnasambaza kadi za michango ya harusi, mnamalizia na kuoana, mnakuwa wanandoa.

Ndoa za hivi zinatunyima fursa ya kufahamiana kiukweli, kufahamiana kiundani, kwa sababu kuna wakati, unabahatika kupata mke safi lakini kuna baadhi ya mambo yanamchafua.

Kwa mfano, kuna jamaa yetu ameoa mke safi tu, lakini kwa sababu hawakuwa wakifahamiana kindakindaki, mume amekuja kugundua kasoro fulani nje ya mke wake ambazo huenda alitakiwa kuzifahamu mapema.

Walitembelewa na mkwe, mama wa mkewe, lakini ajabu, mkwe alikuja na sheria zake na kuibadilisha nyumba kuwa kama shule ya bweni hivi. Jamaa anakwambia, siku ya kwanza alichelewa kurudi, akamkuta mkwe yuko sebuleni anamsubiri, alipoingia tu, anaulizwa eti: “Mbona umechelewa kurudi? Kama ratiba zako ziko hivi huku si kumtesa mwanangu?” jamaa akawa mpole akidhani ni masihara tu ya wakwe wa kisasa.

Lakini kesho na kesho kutwa mambo yakaendelea vile vile. Ndiyo jamaa akagundua kumbe kuna vitu alikuwa havifahamu kuhusu familia ya mke wake, kwa sababu mambo ya namna ile angeyafahamu, huenda angekuwa sehemu nzuri, angejiandaa kuyakabili.

Sema uzuri jamaa mwenyewe alikuwa na akili za kushikiwa, aliapa kwamba atatumia njia za kihuni ili moja kati ya mambo haya mawili yatokee—mama mkwe abadilike au arudi nyumbani kabisa aiache nyumba na amani kama alivyoikuta.

Alichokifanya ni kununua pensi moja kubwa sana, isiyomtosha kabisa. Halafu akaanza kuwa na ratiba za kuwahi kurudi nyumbani, kisha wakikaa sebuleni na familia, anahakikisha anaketi mbele ya alipoketi mama mkwe tena kwa kuitanua miguu—sasa kujichanua, jumlisha pensi kubwa, jibu analo mama mkwe kwa sababu baada ya siku mbili aliomba nauli.