Tite aliupenda utamaduni, dunia ikabadili tabia zake

Muktasari:

  • Soka limebeba uhalisia wa maisha yao na limebeba furaha ya wengi. Ni soka hili ndilo liliwafanya kwa pamoja kama Taifa wamchukie Moacir Barbosa ambaye waliamini kuwa alikuwa chanzo cha wao kutokutwaa taji la dunia mwaka 1950 baada ya kufanya kosa lililozaa goli la timu ya taifa ya Uruguay.

Kwenye mji wa Rio de Janeiro kuna maisha ya aina moja tu ambayo huleta watu pamoja nayo ni soka. Haya ni maisha ambayo yamesambaa kwenye maeneo mengi ya Amerika ya Kusini lakini kwa Wabrazil ni kama utamaduni.

Soka limebeba uhalisia wa maisha yao na limebeba furaha ya wengi. Ni soka hili ndilo liliwafanya kwa pamoja kama Taifa wamchukie Moacir Barbosa ambaye waliamini kuwa alikuwa chanzo cha wao kutokutwaa taji la dunia mwaka 1950 baada ya kufanya kosa lililozaa goli la timu ya taifa ya Uruguay.

Ni soka hili pia lililowafanya wabrazil wasamehe dhambi zote za uzinzi na ulevi uliopindukia wa winga Manu Garrincha mpaka wakaamua kumpachika jina la Alegri Do Povo ikiwa na tafsiri ya furaha ya watu.

Waliamini kuwa huyu alibeba furaha yao na huyu ndiye ambaye aliibeba nembo na bendera ya taifa lao uwanjani. Ulevi wake, sigara zake na anasa zake kwao zilikuwa zinavumilika na alikuwa malaika wao “mlevi.”

Ni miongo mingi imepita na furaha iliwahi kubebewa kwenye miguu ya wengine mpaka kilipofika kizazi cha akina Dunga, Romario mpaka walipokaribishwa akina Ronaldo De Lima, kisha Ronaldinho na Kaka na mwisho wa ubora na mwanzo wa ukawaida ukaanza.

Ni katika kipindi hiki ambacho taratibu Samba ilianza kuonekana zaidi Hispania katika ile filosofia ya TikiTaka kuliko katika miguu ya Wabrazil.

Uhalisia kabisa ni kuwa maisha ya kweli ya kisoka ya Wabrazil yalimalizika baada ya fainali za kombe la dunia mwaka 2006 walipofungwa na Ufaransa.

Nyota wao hawakuwa na nguvu tena miguuni, nyota wao hawakuwa wanaacha kizazi kingine chenye ubunifu kama wao nyuma. Wabrazil walianza kuishi maisha ya “Liverpool” imani kuwa bado walikuwa bora mpaka pale ambapo risasi saba za Wajerumani zilipowadhuru kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Kipindi chote hiki hakukuwa na imani thabiti tena mpaka alipofika kikosini kocha Tite ambaye aliweza kuiunganisha timu na kuleta pamoja vipaji vingi ambavyo pengine ndio kikosi bora kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Brazil walikuwa na wachezaji takribani wawili bora kwenye kila nafasi na hawakumwangusha Tite wakati wa kufuzu kuja Urusi na Tite “alifall In Love” na kikosi chake hicho haswa kikosi chake cha kwanza.

Tite ni kocha ambaye anaamini katika njia iliyompa utajiri kabla na hawezi kujaribu njia mpya na mbadala kwa sababu safari yake haikuwahi kushindikana.

Lakini katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kulikuwa na hali tofauti kidogo na ilivyokuwa kwenye hatua ya kufuzu kuja huku.

Katika hatua hizi, hakukuwa na “underdog” kama ilivyozoeleka kwenye fainali nyingine na kila timu ilijiandaa kufanya makubwa haswa dhidi ya Mataifa ambayo yalionekana yanapewa nafasi zaidi.

Katika michezo mingi, kulionekana kuna shida kwenye muunganiko wa kikosi chake hasa namna ambayo Neymar, Willian na Gabriel Jesus wangeweza kucheza pamoja kutokana na Willian kuwa na namna moja ya uchezaji wakati Gabriel Jesus akiwa hawezi kufungua ngome za upinzani kutokana na umbo lake hivyo kuonekana kuwa wachezaji wawili ambao hawakuwa na makali ya wembe kuacha majeraha ya kudumu.

Mabadiliko ya Firmino ambaye kimsingi alikuwa na msimu bora kuliko, Gabriel Jesus yaliweza kuipa uhai Brazil siku zote na kumfanya Neymar kuwa na nafasi zaidi kutokana na uwezo wa Firmino kuweza kutanua uchezaji wa mabeki wa timu pinzani.

Douglas Costa kwa upande mwingine alikuwa anaongeza ubunifu na kasi kuliko Willian kutokana na uwezo wake wa kukokota mipira na kusogelea ngome ya upinzani.

Lakini bahati mbaya ni kuwa Tite kama ilivyokuwa wahenga wengi, anaamini kuwa wakati wa mvua hutakiwi kuvaa nguo nyekundu au firigisi ni ya baba tu sio watoto.

Kwa Tite mchezaji aliyemfikisha hapa ndiye ambaye angemfikisha pia kwenye nchi ya ahadi ya kombe la dunia.

Haikuwa rahisi na pamoja na kelele nyingi mitandaoni hakukuwa na uhalali wa Firmino au Douglas Costa kuanza kwa sababu kwenye imani ya Tite, moyo wake na utamaduni wake, miguu ya Gabriel Jesus na Willian ilimletea mvua hapo kabla na aliamini kuwa ungefika wakati ambao hali ingerudi kawaida.

Huwezi kumlaumu kwani hata wakati ambao alipata tabu kwenye michuano hii, Firmino au Costa wangeweza kuingia na kubadili mchezo. Lakini wahenga walisema marefu yote huwa na ncha yake na mbio za sakafuni ukingoni huishia.

Majaribio na imani ya Tite lazima kuna wakati ambao ingejaribiwa na muda huo haukuwa mbali, hatua ya robo fainali ilifika na Ubelgiji ndio walikuwa wapinzani wao.

Kwa ubora wa wapinzani hawa ni wazi kuwa kila timu ilikuwa na nafasi ndogo ya makosa “no room for error” na yule ambaye angechanga karata zake vyema ndiye aliyekuwa mshindi.

Tite alirejea kwenye imani yake, bahati mbaya kipindi hiki hakuliona hata wingu kwenye miguu ya Jesus na Willian na badala yake kilikuwepo kiangazi muda mwingi uwanjani na Ubelgiji walitumia nafasi ya kutokuwepo kwa ulinzi wa Casemiro kupata mabao mawili ya haraka ambayo yalimaliza mchezo.

Wakati anakumbuka shuka kipindi cha pili mbu walikuwa wameshaathiri mwili wake na ugonjwa ulikuwa ndani ya damu yake tayari.

Maisha hayakuwa sawa tena pamoja na ukweli kuwa walileta hatari kila ambapo Costa alipokuwa na mpira huku Firmino akiwafanya mabeki wa kati wasicheze kwa uhuru. 0

Tite bado anabaki kuwa kocha bora, na ana kikosi imara chenye vijana wengi. Pengine ilibidi itokee hili aelewe kuwa tabia nchi zimebadilika na wakati wa kiangazi unaweza kuwa masika muda wowote. Angekuwa “flexible” alikuwa na kikosi cha kutwaa ubingwa. Sahau sarakasi za Neymar ambazo hazikuwa zikiwasaidia pia na ambazo ziliwaumiza kupata ahueni ya mwamuzi kwenye mchezo huo.