TUONGEE KIUME: Tofauti tano za majambazi na ‘wanawake wa mjini’

Muktasari:

  • Lakini ubaya ni kwamba wengi wanajua kutumia, ila kuzitafuta kwa njia za kawaida za kibanadamu ndiyo mtihani mgumu kwao.

‘Wanawake wa mjini’ ndiyo viumbe wanaoijua thamani ya pesa na namna inavyotakiwa kutumiwa kuliko kiumbe yeyote yule duniani. Mpe Pesa zote za dunia, kisha muwekee muda wa kuhakikisha awe amezimaliza, atakuonesha.

Lakini ubaya ni kwamba wengi wanajua kutumia, ila kuzitafuta kwa njia za kawaida za kibanadamu ndiyo mtihani mgumu kwao.

Na kwa sababu hiyo, ndiyo sasa wamekuwa wanatumia njia ambazo kwa kiasi fulani zinalandana mno na zinazotumiwa na majambazi wanaofanya uhalifu benki.

Hata hivyo, licha ya kuwa wanalandana na majambazi wa mabenki bado kuna tofauti kubwa kati yao.

Majambazi wanataka pesa tu

Majambazi wa benki wenyewe wanataka pesa tu. Ndiyo maana mara nyingi baada ya tukio husikii shuhuda anayesema walichukua simu na cheni yangu ya dhahabu.

Tofauti na ‘wanawake wa mjini’ ni kwamba licha ya kuwa hata wao wanajali zaidi pesa, lakini hilo sio pekee wanaloweza kuchukua. Ukizubaa wanakukomba pesa zote hadi pochi kabisa, sasa jiulize ni vipi watashindwa kujimilikisha na ‘ka-smartphone’ kako.

Hapa ndiyo utasikia stori kwamba jamaa karudi nyumbani asubuhi akiwa kavaa tambala la deki la hoteli, aliibiwa hadi shati huyo.

Majambazi wanatumia silaha za moto

Majambazi wa benki wanatumia silaha za moto. Wataingia na mitutu, watapiga huku na kule kutisha watu.

Lakini ‘wanawake wa mjini’ bunduki za nini? Wenyewe silaha yao kubwa ni maneno na matendo. Atakujaza maneno matamu hadi utasahau kama pesa ulizokuwa nazo ni za pensheni, zingefaa kufungulia kabiashara cha kukupa nafuu ya maisha wakati unamalizia ngwe yako ya maisha iliyobaki. Hakuna bunduki, ni ulimi na vitendo tu.

Majambazi wana ubinadamu kiasi fulani

Majambazi kuna nyakati wanakuwa na huruma fulani hivi. Hii hata ukitazama filamu utakutana nayo kama huajawahi kukutana na tukio la unyang’anyi.

Utakuta jambazi kuna wakati alitakiwa kumshambulia mtu hata kumuua lakini roho ya ubinadamu inamuingia na anaacha.

‘Wanawake wa mjini’ utatafuta hiyo roho kote na usiipate. Wenyewe hawajali chochote kuhusu wewe hata familia yako inayokutegemea. Anaweza akajua una watoto watatu nyumbani, wote wanahitaji kula, kwenda shule na kulala sehemu nzuri, lakini akakukomba ukabaki mweupe ukose hata nauli na kuanza kupiga simu kwa maswahiba wakutumie nauli.

Majambazi wanalinda muda

Majambazi wakiingia benki, hawataki kumaliza hata dakika tano. Kwanini wafanye hivyo? Wanajua nchi siyo yao hii na inalindwa na jeshi la polisi. Wanafanya haraka wanachofanya na kupotea.

Lakini kwa ‘wanawake wa mjini’ mambo tofauti, hata wao hawapendi kupoteza muda lakini mara zote inalazimika iwe hivyo kwa sababu aina yao ya ukwapuaji unahitaji kumlainisha mtu ubongo na kulainisha ubongo kunachukua muda mrefu hata wiki na kuendelea.

Kiasi cha kuibiwa kinategemea na idadi ya waibaji

Kiasi cha kuibiwa majambazi wanapofanya uhalifu kinategemea wako wangapi na wana uwezo wa kubeba kilo ngapi za hela.

Lakini kwa wanawake wa mjini kiwango cha mwisho kuiba kinategemea na akili ya muibaji. Ukiwa zoba unampa fursa ya kukupiga zaidi na ambavyo ukiwa na akili angeweza.