Tujenge hekalu : Pendekezo

Muktasari:

  • Taifa la Tanzania linapitia kwenye kipindi kigumu cha vituko kwenye chaguzi za marudio kutoka na wabunge na madiwani kujiuzulu, pia hali ya wananchi kukata tamaa na siasa zinazoendelea nchini, hivyo kuna haja ya kujenga hekalu ya kuwaleta wananchi pamoja ikiwamo kurudisha imani kwa taifa lao.

Oktoba 12, 2018 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kiliandaa Mbongi (mjadala) ya makamu wa chuo, ikiwa ni kukumbuka miaka 19 bila kuwa na Baba wa Taifa.

Mada ya Mbongi, ilikuwa juu ya chaguzi – kupiga kura kwenye nchi za Afrika. Wachokoza mada walikuwa ni maprofesa Ransford Gyampo kutoka Ghana, Musambayi Katunga kutoka Kenya na Alexander Makulilo wa UDSM.

Ni vigumu kuchambua Mbongi kwenye makala moja. Labda kwa ufupi ni kwamba sauti kubwa ni kwamba zoezi la kupiga kura katika nchi za Afrika bado linatawaliwa na kigugumizi.

Wachangiaji wengi, walionyesha wasiwasi huu kwa kutoa mifano mbalimbali ya chaguzi za Afrika. Mfano vyama vinavyokuwa madarakani mara nyingi vinatumia nguvu za dola ili kujihakikishia ushindi.

Na kwa kiasi kikubwa idadi ya wapiga kura katika nchi za Afrika inashuka sana kiasi cha kuhoji uhalali wa baadhi ya serikali zinazoshinda uchaguzi kwa idadi ndogo sana ya wapiga kura.

Vituko vya chaguzi

Mfano wa chaguzi za Tanzania, hizi ambazo watu wanahama vyama vyao vya siasa na kujiunga na chama tawala – ilihojiwa na vijana wadogo wa sekondari, hasa kuhusu gharama kubwa ambazo taifa linaingia. Lakini pia tumemshuhudia mgombea ambaye alitamka waziwazi kwamba hata kwa kura mbili yeye atapitishwa tu. Swali ni kushinda kwa kura au ni kupitishwa? Ni wingi wa idadi ya kura unazozipata au ni kutangazwa?

Historia itakuwa mwamuzi

Tunaweza kusema, si tu kutokana na mjadala wa Mbongi, bali kufuatana na hali ilivyo sasa, upigaji kura ni zoezi la kutuingiza kwenye gharama kubwa, si zoezi la kuleta mabadiliko yoyote nchini.

Ni zoezi ambalo wananchi wameanza kulichoka na kuanza kufikiria aina nyingine ya kuwachagua viongozi wao? Haina maana kwenye uchaguzi ambao mgombea ana imani hata kwa kura mbili atashinda au atatangazwa.

Ninakubaliana na Dk Bashiru Ally, katibu mkuu wa CCM, kwa hoja yake kwamba tunahitaji kufanya mijadala, na kwamba mijadala italiponya taifa letu. Ni kweli ni lazima tufanye mijadala na kutafuta njia bora ya kuishi na kuendelea kama taifa moja la Tanzania. Ni lazima tufanye mijadala na kufikia hatua ya kukubaliana kwamba Tanzania ni yetu sote! Kila Mtanzania ni lazima ashirikishwe juu ya mipango ya taifa lake.

Hakuna mtu mmoja mwenye uwezo wa kuliamua hili hata kama ana madaraka ya namna gani. Ni lazima uwe uamuzi wa pamoja. Hakuna njia zaidi ya kujenga Hekalu. Hili ndilo pendekezo langu, ambalo ninalitoa kwa unyenyekevu mkubwa.

Hii ni hoja yangu ya siku nyingi. Kila nikifikiria ni jinsi gani tunaweza kujenga jamii iliyo bora, yenye maadili bora, yenye mshikamano na yenye kupiga hatua ya maendeleo kwa pamoja, wazo la hekalu linakuja akilini mwangu. Wale wanaosoma makala zangu, wanajua jinsi ninavyoliongelea jambo hili na kusisitiza umuhimu wake.

Ninashindwa kupata neno zuri. Labda wengine wanachanganya neno hekalu na nyumba za ibada tulizozizoea. Sina maana ya kanisa wala msikiti. Nina maana ya “kitu” cha kuwaunganisha Watanzania wote. Nafasi isiyokuwa na tabaka, isiyowatenga matajiri na masikini, waheshimiwa na walalahoi. Nafasi isiyowatenga wanaume na wanawake, kabila na kabila na dini na dini. Ni mtu gani ana neno zuri zaidi ya hekalu? Basi ajitokeze!

Vyama vya siasa, vinaleta mgawanyiko. Hata vikijengwa vyuo vya itikadi, kama tunabaki kwenye mgawanyiko huu wa sasa hivi wa CCM na vyama vya upinzani, vyuo hivi haviwezi kutusaidia kitu chochote zaidi ya kuwazalisha wateule wachache.

Nina amini kwamba Watanzania, tunahitaji kitu cha kutuunganisha, kujenga uzalendo, kujenga maadili yetu. Tunahitaji kitu cha kutufanya kuipenda si Tanzania ya leo tu, bali na Tanzania ya vizazi vijavyo. Nilishaeleza kule nyuma kwamba mifumo yote tuliyonayo sasa hivi haitusaidii. Vyama vya siasa havitusaidii, dini hazitusaidii. Tufanye nini?

Kitabu cha Daktari Adolf Mihanjo, cha falsafa kwa lugha ya Kiswahili; “Falsafa na Usanifu wa Hoja- kutoka Wayunani hadi Watanzania (Waafrika)” ni msaada mkubwa kwetu. Ni msaada mkubwa kwa kila mtu anayethamini kufikiri na kutafakari mambo mbalimbali katika jamii.

Katika kitabu hiki mtu anagundua jinsi maendeleo ya mwanadamu yanavyokuja kwa watu kukaa chini kufikiri na kutafakari, na kwamba wanadamu wanasumbuliwa na mambo mbalimbali katika vipindi mbalimbali vya maisha. Wakati huu sisi tunasumbuliwa na namna ya kujenga jamii iliyo bora, yenye mshikamano, maadili na uzalendo. Wanafalsafa wa mwanzo wa kule Uyunani walisumbuliwa na kutaka kujua chanzo cha kila kitu. Kwa vile wao walianzisha hoja hiyo na kuitafakari, iliendelea na kufikia kiasi kwamba si hoja tena. Falsafa yao ilisaidia sana maendeleo ya sayansi ya siku hizi.

Mwanafalsafa Thales, aliyeishi kati ya 624 na 546 BC, alifanyia kazi utafiti wa kisayansi kuhusu asili ya vitu vyote. Vitu vyote vimetengenezwa na nini au ni aina gani ya maada ni chanzo cha kila kitu? Kitu ambacho Thales alitaka kujua kutokana na maswali yake ni namna ya kupata njia au utaratibu ambao ungemwezesha kutoa maelezo yaliyokuwa sahihi na ya kweli juu ya Ulimwengu ambao ulikuwa na vitu vingi vya aina mbalimbali kama vile ardhi, mawingu, maziwa, bahari na vitu vingine. Aliona kuwa baadhi ya hivi vitu vinabadilika kutoka muda hadi muda na vinabadilika kuwa vitu vingine na kwamba vitu hivi vinafanana kwa namna fulani. Mchango wa pekee wa huyu mwanafalsafa katika historia ya kukua kwa fikara, ilikuwa ni wazo alilolitoa kuwa, licha ya tofauti iliyopo kati vitu mbalimbali, kuna ufananisho au mlingano wa msingi kati ya vitu na mlingano huo unaviunganisha licha ya tofauti. Yeye alifikiri kwamba kitu kinachounganisha vitu vyote pamoja na tofauti zote, ni maji! Kutokana na fikra hizi kuna kipindi watu wa Uyunani waliamini kwamba chanzo cha kila kitu ni maji!

Kwa vile watu Uyunani waliendelea kutafari na sikupokea kila kitu kama misaafu, mwanafunzi wa Thales, aliyejulikana kwa jina la Anaximander, alikubaliana na mwalimu wake kwamba ni lazima kuna kitu ambacho ni chanzo cha kila kitu, lakini kitu hicho si maji, bali ni kitu kisichokuwa na mipaka au ukingo. Yeye aliachia hapo na wala hakuelezea hicho kitu kisichokuwa na mipaka ni kitu gani.

Mwanafalsafa wa tatu katika hoja hii ya mwanzo wa kila kitu, alikuwa Anaximenes. Huyu alikuwa mwanafunzi wa Anaximander. Alikubaliana na mwalimu wake kwamba kitu ambacho ni chanzo cha kila kitu ni lazima kisiwe na mipaka, alitofautiana na mwalimu wake kwa kukitaja kitu hicho kuwa ni hewa. Anaximenes alifikia uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa hewa ndio msingi wa uhai wa kitu chochote kile kinachoishi na hicho kitu kikikosa hewa hufa.

Tunaweza kuona jinsi hoja inavyojengwa juu ya nyingine. Mfano, mimi ninaposema ili tujenge jamii iliyo bora, yenye uzalendo, maadili mema na mshikamano, tunahitaji hekalu. Mwingine, anaweza kusema tunahitaji hekalu lililojengwa kwa vifaa vya hapa hapa nchini na wala si vya kutoka nje ya nchi. Na mwingine akasema wakandarasi wa kujenga Hekalu, wawe Watanzania.

Wanafalsafa wengine waliojaribu kutafakari juu ya chanzo cha kila kitu ni Pythagoras, Heraclitus, na wengine ni Wanaatomi walioongozwa na Democritus na Leccippus. Hawa waliamini kuwa chanzo cha kila kitu ni atomi.

Si lengo la makala hii kufundisha falsafa. Ni kutaka kuonyesha jinsi fikra zinavyosaidia kuleta maendeleo. Ni namna ya kutaka kuonyesha kwamba hatuwezi kuwategemea wanasiasa na viongozi wa serikali peke yao kutuletea maendeleo. Ni kutaka kuonyesha kwamba watu wanapokuwa na kitu kinachowasumbua au ambacho wangetaka kujua, wanakaa chini na kutafakari na kuleta hoja mbalimbali. Mfano, hawa wanafalsafa wa mwanzo, kwa kutafuta chanzo cha kila kitu walijaribu kila kitu, huyu anasema ni maji, huyu anasema ni hewa, huyu anasema ni moto, huyu anasema ni hesabu na mwingine anasema ni atomi. Kila hoja inajengwa juu ya nyingine, hatimaye kinapatikana kitu cha manufaa kwa jamii husika na wakati mwingine kwa dunia nzima.

Watanzania tuna kitu kinachotusumbua. Tunataka kujenga jamii iliyo bora. Tunataka kujenga jamii yenye mshikamano na uzalendo. Tunataka kujenga jamii yenye maadili mema na kuwarithisha watoto wetu maadili hayo. Tunataka kujenga jamii ambayo itarithisha vizazi vijavyo Tanzania yenye neema. Tutaijenga vipi jamii hii? Tuanze kutafakari na kufikiri. Tunahitaji wanafalsafa wa Kitanzania, ambao watakaa chini na kukuna bongo zao kama walivyofanya wanafalsafa wa mwanzo.

Mimi ninapendekeza Hekalu. Tukilijenga Hekalu la Kitanzania, halitakuwa na chama, halitakuwa na dini, halitakuwa na kabila. Hekalu “ nyumba ya Mungu”, nafasi ya watu kukutana na kuungana, litawapokea wote, wanawake, wanaume, watoto, wazee, wasiojiweza, yatima, walemavu. Katika Hekalu hili tunaweza kuwafundisha vijana wetu maadili. Sasa hivi hakuna sehemu yoyote ya kuwafundisha vijana maadili. Ni wapi? Shuleni hakuna nafasi ya kufundisha maadili, vyuo vyetu havina nafasi ya kufundisha maadili, viongozi wa dini nao hawana tena nafasi ya kufundisha maadili.

Mwingine, anaweza kupendekeza kitu kingine ambacho ni tofauti na vyama vya siasa na dini. Vyama vya siasa vimeonyesha kuligawa taifa badala ya kuliunganisha, vimepandikiza chuki na kuwatenga wateule wachache wakula matunda ya taifa letu. Dini nazo zinawagawa watu badala ya kuwaunganisha.

Azimio la Arusha, ulikuwa msingi imara ya kulijenga na kulisimika Hekalu letu. Ujamaa na kujitegemea zilikuwa nguzo imara za kulisimamisha Hekalu letu. Jeshi la Kujenga Taifa, yalikuwa matofali imara ya kulijenga taifa letu.

Mwalimu Nyerere, alitaka kutujengea Hekalu la Kitanzania, hekalu ambalo lingemkumbatia kila Mtanzania. Hekalu ambalo kila goti liwe la kiongozi, la tajiri, la masikini lingepigwa. Hekalu ambalo lingelinda uhuru, haki na heshima ya kila Mtanzania. Hekalu ambalo lingelinda utajiri wa taifa letu, utamaduni wa taifa letu na maadili ya taifa letu.

Tulisitisha ujenzi wa hekalu kwa makosa, Sasa ni wakati wa kulijenga tena. Uwe wakati wa kuikumbatia falsafa na usanifu wa hoja, kinyume na hapo ni kujiangusha sisi wenyewe na vizazi vyetu.

Padri Privatus Karugendo.

+255754633122