Tume Huru ya Uchaguzi mwarobaini wa kuzuia mawakala wa upinzani

Muktasari:

  • Lilianza kujitokeza zilipoanza chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Ni malalamiko yasiyokoma. Kila uchaguzi yanajitokeza ama kwa sura ileile au kwa namna tofauti. Ni suala la mawakala wa vyama vya upinzani, hasa Chadema, kukataliwa kwenye vituo vua kupigia kura.

Lilianza kujitokeza zilipoanza chaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Tatizo kubwa lilianza kuonekana katika uchaguzi wa jimbo la Kinondoni mkoani Dar es Salaam, limeendelea katika majimbo mengine na kata zilizofanya uchaguzi baadaye. Inavyoelekea ni malalamiko ambayo hayatokama leo wala kesho.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikidai kwamba ama mawakala wake wananyimwa hati za viapo, au barua za utambulisho zinazotakiwa kuonyeshwa kwa wasimamizi wa uchaguzi. Mara nyingine hati hizo hucheleweshwa na kupatikana baadaye wakati uchaguzi unaendelea.

Madai mengine ambayo hata hivyo yanakanushwa na mamlaka zinazohusika ni kuwa, mawakala wengine hukamatwa na polisi siku moja kabla au siku ya uchaguzi ili wasiwepo vituoni.

Katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita wilayani Monduli, yaliibuka mapya kwamba baadhi ya mawakala walitekwa na kushikiliwa kusikojulikana na gari la mbunge lililokuwa linasambaza wengine lilivamiwa na kutobolewa matairi kwa risasi. Polisi wanasema si risasi ni kitu chenye ncha kali kama kisu au bisibisi.

Mwisho wa matukio hayo ya kuzuiwa mawakala wa upinzani ni kituo cha kupigia kura kubaki na mawakala wa chama tawala pekee, wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Jambo linalowaliza wapinzani kuamini kwamba kura zao haziwezi kubaki salama bila zikiwa mikononi mwa washindani wao pekee.

Wakati Chadema na wapinzani wengine wakiendelea kulalamikia kwa kufanyiwa vitendo hivyo, wasomi na wanasiasa wameeleza kuwa sababu za matukio ni kutokuwapo Tume Huru ya Uchaguzi.

Sababu hiyo imeelezwa siku mbili baada ya uchaguzi uliofanyika Jumapili ukihusisha wabunge wa majimbo ya Ukonga, Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha na madiwani wa kata 23 na CCM imenyakua yote.

Kama ilivyokuwa kwa chaguzi zilizotangulia, Chadema imelalamikia vitendo vya mawakala wake kunyimwa fomu, hati za viapo pamoja na barua za watendaji.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Athumani Kihamia alipoulizwa jana kuhusu kujirudia kwa tatizo hilo na kwa nini linatokea tu kwa wapinzani, alisema “Niko hospitali, mtafute mwenyekiti wa Tume, Jaji Semistocles Kaijage, ambaye hata hivyo hakupatikana.

Hata hivyo, Akizungumza na Mwananchi Jumapili wakati uchaguzi unaendelea, Kihamia alikiri kupokea malalamiko kuhusu kukataliwa kwa mawakala katika majimbo ya Monduli na Ukonga na kuwa alikuwa ameyafanyia kazi.

“Hata huku Monduli niliko lilikuwapo, nimelifanyia kazi mimi mwenyewe na sasa kila kitu kinakwenda sawa. Hata hivyo, Mnyika hajarudi kwangu, kwa hiyo ni dhahiri hakuna tena tatizo, maana nilimweleza kama bado kuna shida anijulishe,” alisema Kihamia.

Hata hivyo, baadaye mchana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alipotembelea vituo vya uchaguzi katika Jimbo la Ukonga alikanusha madai kuwa mawakala wamezuiliwa kuingia vituoni huku akikiri kuwapo na idadi ndogo ya wapiga kura.

Alisema katika majimbo yote ya Monduli na Ukonga uchaguzi ulianza kwa wakati na ulikuwa unaendelea vizuri.

Alisema katika jimbo la Monduli lenye vituo 256 ni mawakala wanne tu walizuiliwa kuingia vituoni na ni kwa sababu za msingi.

“Hao mawakala wanne walizuiliwa kwa kuwa hawakutambuliwa na msimamizi, hawakuapishwa walikwenda kwa niaba ya wengine. Hizi habari zinazosambazwa kuwa mawakala wote Monduli wamezuiliwa si kweli watu wasisambaze taarifa ambazo hawana uhakika nazo. Naona kila kitu kinakwenda sawa hakuna wakala aliyezuiliwa na kama hajafika ni kwa utashi wake.”

Uzoefu wa Dk Bisimba

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkurugenzi, Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema mara nyingi madai ya mawakala kunyimwa fomu, hati za viapo na barua za utambulisho kutoka kwa watendaji hutokea kwa vyama vya upinzani pekee kwa sababu hiyo ni mbinu chafu za kuharibu uchaguzi.

“Mara zote kunakuwa na hila za wazi katika vituo ili kuharibu uchaguzi na CCM ionekane imeshinda jambo ambalo si sahihi,” anasema Dk Bisimba.

Dk Bisimba anakumbushia tukio la mwaka 2017 alipokuwa mwangalizi wa uchaguzi mdogo Katika Jimbo la Kinondoni, kuwa vitendo hivyo vilikithiri.

“Bahati nzuri mimi nilishawahi kuwa mwangalizi wa hizi chaguzi ndogo, nilishuhudia figisufigisu nyingi ikiwamo hilo la mawakala kuwekewa vigingi. Nakumbuka nikiwa katika Kata ya Magomeni kituo cha kupiga kura cha Magomeni Kondoa mawakala wa Chadema walizuiliwa kuingia ndani mpaka saa 9:00 mchana kwa kisingizio cha kutokuwa na barua zilizopaswa kuwa nazo,” aliongeza.

“Lakini cha kushangaza ilipofika saa 9, alikuja mgombea wa Chadema, Salimu Mwalimu na kuomba kukagua barua walizokuwa nazo CCM, ndipo alipogundua hazikuwa na tofauti yoyote na zile walizokuwa nazo wenzao wakaruhusiwa kuingia lakini muda ulikuwa umeshaisha,” alisisitiza.

Dk Bisimba alisema alishuhudia kuna maeneo mengine wapinzani wakizuiliwa kuingia ndani na vituo, hawakujitokeza watu kupiga kura, lakini jioni wakati wa kuhesabu zilipatikana kura nyingi.

Dk Bisimba analaani vitendo hivyo na kusema kuwa havihashirii uwapo wa demokrasia ya kweli kwa kuwa havitoi haki sawa kwa vyama vyote.

Kufuatia hali hiyo Dk Bisimba anashauri wapinzani kutokaa kimya, badala yake wafuate taratibu za kisheria ikiwamo kwenda mahakamani.

“Bahati mbaya sasa nimeona Watanzania wamekata tamaa na matokeo yake wameamua kutojitokeza kupiga kura, hili halisaidii badala yake wapinzani wanatakiwa kuhakikisha wanadai haki hiyo kwa nguvu zote,” aliongeza.

Hata hivyo, Dk Bisimba anaonya kuwa vitendo hivyo endapo vitaendelea itasababisha mtafaruku mkubwa kwani ipo siku Watanzania watachoka na kuripuka.

Ukiacha ya Dk Bisimba, Wakili Peter Mshikilwa anasema vitendo hivyo vinafanywa kwa vyama vya upinzani kwa sababu hakuna Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itafanya kazi bila kuwa na wasiwasi wowote.

“Lazima utii mamlaka iliyokuchagua ndiyo kinachoonekana kwa Tume yetu ya uchaguzi, kukiwa na Tume huru kila kitu kitaenda sawa na haya hayatajitokeza,” alisisitiza Mshikilwa.

Wakili huyo alisema ili kuepukana na vitendo hivyo, kuna vitu vitatu ambavyo wapinzani wanaweza kuvifanya na kupata suluhisho la kudumu.

Mosi, anasema jambo la kwanza ni kwa wapinzani wanapaswa kulalamika mahakamani juu ya vitendo anavyofanyiwa na mahakama ikatoa tafsiri ya kisheria.

Pili, wapinzani wanaweza kutumia Mahakama kupinga matokeo hayo badala ya kuendelea kulalamika bila kuchukua hatua.

Tatu, ni kuwapo mpango wa muda mrefu wa kudai Tume huru ya uchaguzi.

“Sasa Tanzania hatuna Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na hili linaweza kupatikana kama wapinzani wakiamua kushinikiza

Ili kuhakikisha inapatikana kama ilivyo kwa jirani zetu Kenya ambako wameweza kupata suluhisho la kudumu,” alisisitiza.

Hata hivyo, CCM inasema suala la mawakala kupata matatizo si kwa wapinzani pekee bali pia mawakala wake hukumbwa na kadhia kama hiyo.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole anasema, “Ungekuwa umetaja maeneo maalumu ningeuwa kwenye nafasi nzuri ya kujibu, ukisema kwa ujumla si sawa, kwa sababu kuna mahali hata mawakala wa CCM walizuiliwa,” anasema Polepole.

Hoja tofauti ya Profesa Safari

Akizungumzia hilo Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari anasema vikwazo wanavyowekewa mawakala wa upinzani ni kwa sababu hakuna uchaguzi wa kweli.

Profesa Safari ambaye pia ni mwanasheria anasema kutokana na hali hiyo yeye haoni sababu za kwenda katika chaguzi hizo na badala yake wawaachie CCM pekee washiriki.

“Nilishawahi kusema kwamba msimamo wangu sioni sababu ya kuendelea kushiriki chaguzi hizi kwani ni fake (za kuigiza) na leo hii inadhihirisha kwamba chama tawala kinatumia kila njia kuhakikisha kinashinda kwa hila,” alisisitiza.

Alipoulizwa kwamba haoni kususia uchaguzi kunawanyima wapigakura kutumia haki yao kuchagua, makamu huyo mwenyekiti wa Chadema alisema haoni sababu ya kujidanganya kwamba wanapata haki yao ilhali hakuna usawa.

“Ni bora wakatulia nyumbani kuliko kushiriki kufanya maigizo,” anasema.

Akichangia mada hiyo, Waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema naye hali hiyo inatokana na kutokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

“Tunachofanya sasa ni maigizo tu, haiwezekani Mkurugenzi wa halmashauri kuwa ndiye msimamizi wa uchaguzi ukategemea kuwe na uchaguzi huru, hawa watu wanaripoti kwa Serikali kamwe hawezi kufanya vinginevyo,” anasisitiza Kasaka.

Kasaka anasema nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania wapinzani wamekuwa wakishindana na Serikali badala ya kushindana na chama tawala.

“Nchi nyingi zimeshindwa kutengeneza mpaka wa Serikali na chama tawala, matokeo yake vyama vya upinzani vinajikuta vikipambana na Serikali badala ya chama tawala ndiyo maana unakuta Tume haitendi haki,” aliongeza.