Tuwakomboe watoto kwenye maisha hatarishi

Mtoto akiponda kokota kwa ujira wa Sh350 kwa ndoo ya lita 20. Ajira kwa watoto ni tatizo linaloendelea kuisumbua Serikali kutokana na watu wengi kutozingatia sheria inayotoa haki kwa mtoto. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Licha ya Serikali na taasisi za kimataifa kutetea haki ya mtoto, bado ushirikiano wa wananchi unahitajika katika kulinda haki ya mtoto ikiwamo kuacha tabia ya kutoa ajira kwa watoto kinyume cha sheria.

Siku hizi ajira za watoto, wengine wakiwa na umri wa chini ya miaka 10, ni tatizo kubwa katika nchi nyingi licha ya kuwepo mikataba mbalimbali ya kimataifa na msururu wa sheria za kulinda haki za mtoto.

Maelfu ya watoto, wakiwemo wenye ulemavu, wanafanyishwa kazi chafu na za hatari ambazo huathiri afya zao na hata kuwa sababu za kuwapotezea maisha.

Mpaka miaka ya mwisho ya 1980 hali hii ya kusikitisha haikuwa mbaya sana Zanzibar, kama ilivyokuwa katika nchi nyingi duniani, zikiwemo zile za jirani.

Hata hivyo, kila kukicha taarifa za hapa na pale zinaonyesha hali inazidi kuwa si ya kuridhisha na ya kusikitisha kama vile jamii ya hivi sasa haikurithishwa njia, mila, utamaduni na desturi nzuri za kulea, kulinda na kuwapenda watoto ambao kwa lugha ya watu wa Zanzibar hawa huitwa malaika.

Unapotembelea baadhi ya maeneo ya Unguja na Pemba, mjini na vijijini, utasikitishwa kuona badala ya watoto kutumia muda mrefu kutafuta elimu, kwenda kusoma madrasa au kucheza wanafanya kazi kubwa kuliko zinazostahiki kwa udhaifu wa miili yao.

Wapo watoto ambao kwa saa nyingi kila siku, iwe wakati jua kali au wakati wa mvua, huwa wanachezea vumbi kuvunja kokoto au kuchonga matofali ya mawe hasa kisiwani Pemba.

Watoto wengine huwa wanapandisha ufukweni au kuteremsha baharini vyombo vya uvuvi, wanapara samaki, wanabeba mizigo mizito na hata kukwea minazi.

Ni hatari tupu

Siku hizi katika mitaa mingi ya mjini Unguja na vitongoji vyake usiku na mchana utaona watoto wanazunguka na magari ya ng’ombe au punda, toroli la kusukuma kwa mkono au vipolo wakiwa wanabeba mchanga au kukusanya taka majumbani kwa malipo madogo.

Kinachosikitisha ni kuona wazee wengi wanaiona hali hii na kuifumbia macho kutokana na kuichukulia kuwa ati ni ya kawaida na wachache wanaoilalamikia huambiwa zama zimebadilika na kutakiwa kwenda na wakati.

Jamii inaonekana haijali hatari za watoto kufanya kazi hizi nzito na hatarishi zinazopelekea baadhi yao kutokwenda shule.

Baadhi ya taasisi za kiraia zimekuwa zinafanya juhudi za kuwaachisha hawa watoto hizi kazi zinazowaharibia maisha yao na kuwarudisha shule, lakini tatizo bado ni kubwa na linahitaji kila mwana jamii kulitolea mchango wa kuikomesha hali hii.

Zanzibar upo mradi maalumu wa kuwarudisha shule watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kulazimika kufanya kazi kupata fedha za kujikimu. Mradi umefanikiwa kuwarejesha shule zaidi ya watoto 1,948 walioacha masomo kwa sababu mbalimbali.

Kuwarejesha shule haitoshi Kinachotakiwa ni kufuatilia maendeleo yao na kuwasaidia wasirejee huko walipokuwa wanaharibikiwa kimaisha.

Nchi nyingi na hasa za Amerika ya Kusini zilizopuuza hatari ya watoto kutokwenda shule na kuanza kazi mbalimbali zilizowaweka karibu sana na watu waliowazidi umri, hivi sasa zinakabiliwa na tatizo la watoto wa mtaani.

Wengi wa watoto hawa wamejiingiza katika vitendo vya uhalifu vya kuiba, kukaba watu na hata kuua ili wapate fedha.

Vilevile wapo watoto wanaotumiwa na majambazi na wezi au kuwa wabebaji wa dawa za kulevya kutoka eneo moja kwenda jingine.

Hili si suala linalostahiki kupuuzwa au kushughulikiwa kwa msimu bali linapaswa kuwa endelevu. Ni muhimu kwanza kutoa elimu ambayo itamhamasisha kila mwana jamii kujitokeza kuchangia kuepukana na hizi ajira mbaya kwa watoto.

Utoaji huu wa elimu unapaswa kwenda sambamba na wana jamii kukumbuka namna kila mmoja alivyopatiwa elimu na kupatiwa malezi mazuri na ya huruma alipokuwa mdogo na kuchukua juhudi muwafaka za kuwazuia watoto wenye kufanya kazi mbalimbali, hasa zile hatarishi.

Ni kwa kila mwana jamii kuona anao wajibu mkubwa wa kuchangia kupambana na hali hii na sio kuiachia Serikali peke yake na baadhi ya taasisi za kiraia ndio tutakapoweza kupata mafanikio.

Kuendelea kwa kila mmoja wetu kulalamika hakutatusaidia. Tuchukue hatua ili tusije kujuta hapo baadaye kwa kuwa na kundi kubwa la watu wasiokuwa na elimu na waliojikita katika vitendo vya uhalifu ili kuendesha maisha yao na huku wakipoteza maisha ya wenzao wasiokuwa na hatia wakati wanapofanya huo uhalifu wao.

Mungu ibariki Tanzania na watoto wake.