Twaweza, siasa zetu na sauti za wananchi nchini kwetu

Muktasari:

  • Lengo la makala hii ni kuunga mkono programu yao iitwayo Sauti za Wananchi. Kwa maelezo yao; programu hii inatoa fursa kwa wadau wa Serikali wafanya maamuzi vyombo vya habari na wadau wengine kufahamu hali halisi (au kupima mapigo ya moyo) kwenye masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.

Makala hii si utetezi wa Twaweza, ni imani yetu kwamba taasisi hii ni kubwa na ina uwezo wa kujitetea yenyewe au utetezi wake ni kazi zake zinazoonekana wazi kwa wananchi.

Lengo la makala hii ni kuunga mkono programu yao iitwayo Sauti za Wananchi. Kwa maelezo yao; programu hii inatoa fursa kwa wadau wa Serikali wafanya maamuzi vyombo vya habari na wadau wengine kufahamu hali halisi (au kupima mapigo ya moyo) kwenye masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.

Kabla ya programu hii ya Sauti za Wananchi, hapajawahi kuwapo fursa na uwezo wa kufahamu maoni ya wananchi wa kawaida kwa haraka na gharama nafuu.

Sauti za Wananchi imekuwa chipukizi na kinara katika nyanja hii ya kupima mapigo ya moyo wa taifa. Ufanisi huu wa kuandaa, kutekeleza na kusimamia programu uliishawishi Benki ya Dunia kushirikiana na Twaweza katika kuandika kwa pamoja kitabu juu ya namna gani tafiti zenye kutumia simu zinaweza kufanywa – Jambo ambalo limebuniwa na kutendwa Tanzania, sasa linatumika kama mfano bora na la kuelimisha taasisi katika kila pembe ya dunia.

Idara kadhaa za Serikali zimeshatumia taarifa zinazotolewa na Sauti za Wananchi kukusanya takwimu ambazo zinasaidia katika utekelezaji wa kazi zao, likiwamo Jeshi la Polisi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Pia, Twaweza imepokea na kushughulikia maombi ya kutoa ripoti za kina kwa baadhi ya maofisa wa Serikali.

Sauti za Wananchi ilianzishwa mwaka 2013 nchini Tanzania na iliendesha raundi 65 kwa kutumia miundombinu iliyoiweka na kuchapa zaidi ya machapisho 50 kutoka katika maoni, sauti na uzoefu wa wananchi.

Katika kipindi hicho, matokeo ya Sauti za Wananchi yameandikwa au kunukuliwa katika habari (magazetini, redioni na kwenye vipindi vya runinga zaidi ya mara 1,000 huku ikipata ushiriki na mjadala zaidi ya milioni kwenye mitandao ya kijamii.

Kama sikosei, sakata la Twaweza na Serikali limechochewa na programu hii ya Sauti za Wananchi – Pale ambapo programu hiyo ilitoa sauti isizopendeza kwenye masikio ya wakubwa.

Binafsi ninaiunga mkono programu hii kwa kuamini kwamba kiongozi mzuri ni lazima asikilize sauti za wananchi. Bila kusikiliza sauti za wananchi ni kazi ngumu kupanga mipango ya maendeleo na kutekeleza shughuli nyingine za ujenzi wa Taifa.

Si lazima unaposikiliza sauti za wananchi, usikie yale unayoyataka, wakati mwingine utasikia yale usiyoyataka. Ukiwa mkweli unayaweka wazi au unaweza kuamua kuyaficha ili uifurahishe nafsi yako.

Lakini kwa taasisi kama Twaweza, kuficha ukweli wa sauti za wananchi ni kujimaliza yenyewe. Ni imani yangu kwamba, kwa vile wanazingatia weledi, wanatangaza hata yale wasiyopenda kuyasikia, lakini kwa vile ni sauti za wananchi wanaziota jinsi zilivyo.

Hoja yangu ya pili kwenye makala hii ni kuhoji uhusiano wa makosa ya Twaweza, kama kweli wana makosa, maana tumeshuhudia majibizano kati yake na serikali na juzi waliitisha mkutano na waandishi wa habari; uhusiano wa ‘makosa’ yao na kushikiliwa hati ya kusafiria ya mkurugenzi mtendaji wa Twaweza.

Inawezekana Twaweza, ikafanya makosa. Lakini uraia wa mkurugenzi mtendaji unaingia vipi hapa? Baadhi ya vyombo vya habari vimeandika kwamba Uhamiaji yanahoji uraia wa Aidan Eyakuze, mkurugenzi mtendaji wa Twaweza. Wengine katika mitandao ya kijamii wanahoji hata jina la Eyakuze, kwamba si la Tanzania.

Wanakuwa wavivu wa kufikiri na kukubali ukweli wa kihistoria. Kwamba kuna majina ambayo utayakuta Burundi, Rwanda, Uganda hata na Kenya. Mfano jina la Otieno, liko Uganda, Kenya na Tanzania. Karugendo, liko Burundi, Rwanda, Uganda na Tanzania.

Itakuwa ni kichekesho kama uhamiaji wanamhoji hata na Aidan Eyakuze uraia wake wakijikita kwenye jina lake! Wakawaulize wazee kama mimi na wengine ambao tunamfahamu baba yake Aidan na mama yake. Watuulize sisi tunaoufahamu uzalendo na kazi kubwa alizozifanya Marehemu Dk Eyakuze; aliitumikia Tanzania kwa uzalendo mkubwa na wakati mwingine aliiwakilisha vizuri nchi yake kwenye mataifa mengine.

Mimi hivi sasa nina umri wa miaka 62, nilikutana na Aidan Eyakuze, kwa mara ya kwanza nikiwa na umri wa miaka 16. Nilikuwa ninasoma sekondari ya Lake Mwanza, wakati baba yake, Dk Eyakuze akiwa anafanya kazi kwenye kituo cha utafiti cha tiba Mwanza. Wakati huo Aidan, akiwa mdogo, tunasali pamoja kwenye Kanisa la Nyakahoja.

Inawezekana ushuhuda huu, hautoshi kutetea uraia wa Aidan Eyakuze, lakini kwa vile baba yake ni Mtanzania, na amezikwa kijijini kwake Kasharu- Bukoba na mama yake Maria ni mzaliwa wa Kiziba- Bukoba, basi hapa ni kuhoji uraia wa watu wengi wa ukoo wa baba yake na ukoo wa mama yake. Haitoshi kuhoji uraia wa Aidan, bila kuhoji uraia wa watu wengi ambao ni ndugu zake wa damu.

Kwa faida ya msomaji wa makala hii ni kwamba Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tatu. Uganda, Rwanda na Burundi. Na kuna historia ya miaka mingi ya watu wa nchi hizi kuingiliana, kuwa na utamaduni unaofanana na lugha zinazofanana. Mipaka ya nchi hizi haikufanikiwa kuondoa udugu ulioanzishwa na mababu zetu. Nakumbuka kuandika makala fulani nikisema kwamba mwenyeji wa Mkoa wa Kagera ambaye hana chimbuko Rwanda, Burundi au Uganda si mzaliwa wa mkoa huo.

Tanzania inapakana na nchi nyingi, hivyo mikoa mingi ina tatizo hili la wahamiaji haramu, lakini tatizo hili ni kubwa zaidi Kagera. Ni vigumu kuelewa kwa nini tatizo hili linasikika sana mkoani humo kuliko kwingine. Mfano Mtwara, watu wa Msumbiji wanaingia na kutoka na wengine wanaishi Tanzania bila kelele za “uhamiaji haramu”. Arusha ndugu zangu Wamasai wanaingia Kenya na kurudi Tanzania na kuishi bila kuitambua mipaka ya nchi hizi mbili, lakini hakuna kelele za “uhamiaji haramu”.

Na mara nyingi hili suala la uraia, linawakumba watu wa Mkoa wa Kagera. Hili halikuwa tatizo wakati wa uongozi wa kwanza wa taifa letu. Mwalimu Nyerere aliifahamu vizuri historia ya Afrika na bado aliamini umuhimu wa muungano wa Afrika nzima.

Ukiachia mbali historia ya bara letu la Afrika ya mipaka ya nchi zetu kuibuka 1884? Mwalimu Nyerere, alifungua mipaka ya nchi yetu kwa Waafrika wote. Tanzania, iliwapokea wakimbizi na wapigania uhuru. Kwa miaka mingi, ilikuwa ni kimbilio la wengi na msamiati huu wa “wahamiaji haramu” haukujulikana.

Kwa njia hii watu wengi wa nchi jirani walipata uraia wa Tanzania na wengine waliendelea kuishi hivyohivyo bila hata kujishughulisha kuomba uraia. Kwa maana nyingine, huko nyuma hakukuwa na mpango wa kudumu wa kulishughulikia suala la wahamiaji haramu...au hakukuwa na umuhimu wa kutengeneza mpango wa kulishughulikia suala hili.

Mwalimu Nyerere, hakuimba tu wimbo wa binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni lazima iungane; hakutumia mvinyo ili aseme ukweli. Alitekeleza kwa matendo!

Ndio maana wakati wa uongozi wake, Tanzania, ilikuwa kimbilio la kila mwanadamu. Wapigania uhuru walikaribishwa Tanzania na kuishi kama nyumbani kwao; walipotaka kutembelea nchi za nje kama Ulaya na kwingineko, walitumia pasi za Tanzania; walianzisha makambi ya mapambano hapahapa. Uganda, ilipopinduliwa na kutawaliwa na Iddi Amin, Mwalimu alikataa kukaa kimya, alifanya uamuzi mgumu wa kuingilia kwenye mapambano ya vita vya Kagera.

Hatukusikia lugha ya wahamiaji haramu wakati wa uongozi wa Mwalimu. Sasa hivi ni kinyume. Watanzania tumeanza kujenga utamaduni wa ubaguzi, tena ubaguzi mbaya kabisa. Hivi karibuni Tanzania, tumekuwa na zoezi la kuwafukuza wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi na Uganda.

Ndugu zetu ambao tunaunganishwa na damu, na wengine tunaongea lugha moja na utamaduni unaofanana, lakini tunateganishwa na mipaka ya kikoloni.

Hivyo tusiimbe wimbo wa Umoja wa Afrika, tusiimbe wimbo wa binadamu wote ni sawa, wimbo wa Azimio la Arusha, bali tutekeleze falsafa hii. Tusimkumbuke Mwalimu Nyerere kwa mihadhara mizuri ya kupendeza, bali tuunde mifumo ya kutuwezesha kutekeleza falsafa hii ambayo ni urithi wetu.

Mwalimu, aliwaheshimu binadamu wote na alifanya jambo hili kwa matendo! Mwalimu aliamini kwamba Afrika ni lazima iungane na alifanya hivyo kwa matendo kwa kufungua milango ya Tanzania kwa kila Mwafrika.

Tuache utamaduni huu wa kutumia uraia kama silaha ya kuwanyamazisha watu wanaohoji na kuwa na mawazo tofauti. Tutalijenga taifa letu kwa kusikiliza sauti za wananchi na hasa kusikia yale tusiyopenda kuyasikia na kuyafanyia kazi.

Hivyo programu ya Twaweza ya Sauti za Wananchi ni ya kuungwa mkono ingawa wakati mwingine italeta sauti zisizotufurahisha. Si ukweli kwamba sauti zisizotufurahisha ni za watu kutoka nje ya Tanzania.

Watanzania zaidi ya milioni hamsini hawawezi kuwa na sauti moja, ni lazima watakuwa na maoni tofauti na kawaida tofauti zetu zinatuunganisha; chanya na hasi inazaa maisha, hii ni sayansi ya maisha na wala hakuna kupinga.

Padre Privatus Karugendo+255 754633122