UCHAMBUZI: Jela inavyowajenga wanasiasa kisiasa

Nimejifunza kitu. Mungu husikiliza maombi ya wenye haki hata kama anachelewa kujibu kwa wakati.

Mungu alipotaka yatokee mageuzi ya mfumo wa utawala Afrika Kusini hakumwacha kaburu Balthazar Johannes “B. J.” Vorster aendelee kuishi. Katikati ya makaburu Mungu alimwinua mwenye roho nzuri Frederik de Klerk.

Vorster ndiye alikuwa waziri wa sheria (1961-66) zilizokuwa zikiwakandamiza Waafrika enzi za apartheid na alikuwa mhimili katika usikilizwaji kesi kwenye mahakama ya Rivonia na kufungwa maisha kwa mpigania uhuru Nelson Mandela. Baadaye Vorster alikuwa waziri mkuu (1966-78), rais (1978-9) lakini alikufa mwaka 1983.

De Klerk, 82, akiwa rais mwaka 1989 alianzisha mageuzi yaliyowezesha Februari 11, 1990 Mandela kutoka jela, akasimamia uchaguzi mkuu wa kwanza huru na haki mwaka 1994 uliowezesha Mandela kuwa rais huku yeye akiwa naibu wake.

Mungu amemwacha De Klerk awe kielelezo cha maisha ya siasa safi na utawala bora kwa watawala wengine Waafrika wajifunze kuongoza kwa upendo, kujali demokrasia na haki.

Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema: “Njia ya kuelekea jamii huru haijawahi kuwa rahisi; Kuna kurasa nyingi za kutisha na za mafanikio katika historia yetu.”

Wanasiasa wenye historia ya kutesekea haki na wakaja kufanikiwa wapo. Mfano aliyekuwa rais wa Brazil, Dilma Vana Rousseff, baada ya kushiriki harakati za mapambano dhidi ya utawala wa kidikteta wa kijeshi, alikamatwa, akateswa na akafungwa kuanzia 1970 hadi 1972.

Hakufia jela, alitoka akaendeleza harakati na mwaka 2010 alishinda urais, akachaguliwa tena mwaka 2014 japo aliondolewa na Bunge mwaka 2016.

Kifungo huwapaisha wanasiasa. Kule Malaysia kuna mwanasiasa anaitwa Anwar Ibrahim. Alikuwa naibu waziri mkuu kuanzia 1993-8 akawa waziri wa fedha lakini aliondolewa na akafungwa Aprili 1999-2004. Alirudi kwenye siasa moto.

Mwaka 2015 alitupwa tena jela kwa kosa la kulawiti. Mei 16, 2018 aliachiwa. Makubaliano yaliyofikiwa na Mahathir Mohamad aliyetumia chama chake kukiangusha chama tawala ni kwamba miaka miwili ijayo Ibrahim atakuwa waziri mkuu. Isitoshe Oktoba ulifanyika uchaguzi mdogo akashinda kiti cha ubunge.

Nasema Mungu ana makusudi yake. Miaka mitano ya utawala wa Sani Abacha (1993-8), Nigeria iligeuka kuwa jehanamu. Ukikosoa jela; ukipinga sera kifo. Mungu hakutaka aishi aushi maana angezuia maono aliyopata Olusegun Obasanjo aliyeokoka akiwa gerezani.

Kama Abacha asingekufa Juni 8, 1998, Obasanjo angeendelea kuozea jela. Lakini Mungu aliingilia kati Abacha akafa, Obasanjo akaachiwa jela; mwaka 1999 akagombea na kuwa rais.

Sikia ya Senegal. Abdoulaye Wade alijitoa kwenye chama cha Léopold Sédar Senghor mwaka 1974 na akachuana naye, na miaka iliyofuata alichuana na Abdou Diouf. Pamoja na kupewa vifungo vya nje na ndani Machi 2000 alishinda urais na akaongoza hadi mwaka 2012. Diouf, 83, na Wade, 92 wako hai.

Jela haijawahi kufifisha nyota ya siasa kwa wanasiasa.