UCHAMBUZI: TRA itusaidie kutegua kitendawili cha stika

Tangu mwaka 2014, pombe kali bandia zimekuwa zikikamatwa mkoani Kilimanjaro zikiwa na stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na huu sasa tunaamini ni wakati mwafaka TRA kutegua kitendawili hiki.

Hatusemi TRA kama taasisi inahusika, la hasha, bali wapo watu wasio waaminifu wanaotaka kuipaka matope taasisi hii ili ionekane kuwa inajali fedha kuliko afya za mamilioni ya Watanzania. Ninasema ni wakati mwafaka kwa sababu ninaamini pombe hizi zinazotengenezwa kienyeji zimeshaathiri maisha ya wanywaji wengi tunaowajua na tusiowajua kwa kunyweshwa sumu bila kujua.

Kwa uelewa nilionao ni kwamba, stika hizi zinatolewa na TRA baada ya kujiridhisha na uhalali wa biashara, aina ya bidhaa inayoombewa stika na kama muombaji amesajiliwa kama mlipa kodi na kutmabuliwa na taasisi zingine husika.

Stika hizi zina namba za utambuzi ambazo zinaiwezesha TRA kutambua stika inayoanzia namba fulani hadi namba fulani alipewa mfanyabiashara fulani na yuko mahali fulani.

Kama stika za mfanyabiashara halali zitakutwa kwenye pombe bandia, lazima atuambie zimefikaje huko na hii ni pamoja na kutuonyesha taarifa aliyoifungua polisi ya kuibwa kwa stika zake.

Tofauti na mazingira hayo, yeyote anayehusika na utoaji wa stika hizi kwa wazalishaji wa pombe bandia anapaswa kuchukuliwa kuwa mhujumu wa uchumi. Hakuna ubishi kuwa wanywaji wengi wa pombe kali wanaamini iliyo na stika hizi za TRA ni halali wala hawahangaiki kutazama kama ina nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au la.

Kwa faida ya wasomaji wa makala haya, nitaweka baadhi ya matukio ya kukamatwa kwa shehena za pombe kali bandia zikiwa na stika halali za TRA ili sasa watuambie usafi wa nyumba yao.

Wiki mbili zilizopita, maofisa wa polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah pamoja na wa TRA, walikamata shehena ya pombe kali bandia eneo la Msaranga mjini Moshi. Katika nyumba zilimokuwa kulikutwa chupa tupu za Highlife 2,400, chupa zisizo na nembo 230, vizibo vya chupa za Konyagi, lita 750 za spiriti na jiko la “mchina” linalotumika katika kufungasha pombe hizo.

Mbali na malighafi hizo na zingine ambazo tayari zilishajazwa pombe, katika nyumba hiyo polisi na maofisa wa TRA walikuta stempu za mamlaka hiyo ambazo hubandikwa katika pombe hizo.

Desemba 22, 2015 katika eneo la Shah Tours Sango, kulikamatwa katoni 186 za pombe kali bandia aina ya Konyagi na viroba 93 na vyote vilikuwa na stika za TRA, kwa maana hiyo wanamfahamu mhusika.

Lakini Desemba 30 mwaka huohuo, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, mfanyabiashara Joseph Maole maarufu “Tajiri mtoto”, mauaji ambayo yana utata hadi leo.

Katika upekuzi wa polisi katika nyumba ya marehemu kulikutwa malighafi pamoja na vifungashio vya pombe kali aina ya Konyagi, licha ya kwamba alikuwa si mtengenezaji wala muuzaji wa pombe hizo.

Kamanda wa polisi wakati huo, Ramadhan Mungi akasema; “Ni kweli kulikutwa hizo stika za TRA na sisi kazi yetu ni kuchimbua ziliingiaje mikononi mwa Maole wakati sio muuzaji wa Pombe.”

Aprili 8, 2014 watuhumiwa wanane wakazi wa Dar es Salaam na Arusha, walikamatwa huko Bomang’ombe wilayani Hai wakiwa tayari wamezalisha katoni 45 za pombe bandia za Konyagi.

Huko nako walikutwa na stika halali za TRA namba LS10CL ambazo tayari walizibandika katika pombe hizo. Hii ni mifano michache tu, lakini ipo mingi ya kugushiwa kwa pombe zingine kali.

Ndio maana nimetangulia kusema TRA sasa watusaidie kutegua kitendawili cha mtandao huu unaolisha sumu Watanzania, vinginevyo tutawaona kuwa nao ni sehemu ya mtandao huu wa kihalifu. Katika kutegua kitendawili hiki, TRA ituambie ni watumishi wangapi wasio waaminifu na wafanyabiashara wangapi wameshachukuliwa hatua kwa kutumia kiholela stika hizi.

Ingawa mimi si mtaalamu wa afya, lakini athari za pombe bandia ni kubwa kwani huathiri nguvu ya macho kuona na pia viungo vingine muhimu kama ini na kusababisha mauti.

Viwanda vya mitaani vinavyozalisha pombe hizo feki havina mashine zinazoweza kutenganisha kati ya ethanol na methanol na hivyo pombe kuwa na kemikali zote mbili.

Ethanol haina madhara lakini, methanol ni sumu na ina athari kubwa kwa sababu katika kutengeneza pombe hizo bandia, mashine hizi za mitaani mara nyingine zinashindwa kutenganisha kemikali hizo.

Daniel Mjema ni mwandishi wa Gazeti la Mwananchi mkoani Kilimanjaro. Anapatikana kwa simu namba 0769-600900