Uamuzi wa Chadema kususa uchaguzi, ni woga au ujasiri?

Muktasari:

  • Ni uamuzi uliokuja wakati mezani kuna uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Liwale, Lindi na madiwani wa kata 37 utakaofanyika Oktoba 13, huku madiwani wengine wakiendelea kuacha kata zao wazi kwa kujitoa upinzani na kujiunga na CCM.

Ni uamuzi mgumu, ndivyo unavyoweza kuelezea hatua ya Chadema kutoshiriki chaguzi ndogo zinazotangazwa kila kukicha.

Ni uamuzi uliokuja wakati mezani kuna uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Liwale, Lindi na madiwani wa kata 37 utakaofanyika Oktoba 13, huku madiwani wengine wakiendelea kuacha kata zao wazi kwa kujitoa upinzani na kujiunga na CCM.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anataja sababu tatu za kutoshiriki chaguzi hizo.

Mosi, anasema hadi sasa wapigakura wapya hawajaandikishwa tangu 2015 kama sheria inavyotaka, pili, chama hicho kimekuwa kinafanyiwa hujuma za wazi, tatu, katika chaguzi hizo kumekuwa na matumizi makubwa ya nguvu za dola na wapigakura kutishwa.

Katika chaguzi ndogo tano, kuanzia ule wa Novemba 26, 2017 mpaka ule uliopita wa Septemba 15 mwaka huu, CCM imeshinda majimbo yote tisa ya ubunge na kata 86 zilizotokana na wawakilishi wake kuhama vyama na kujiunga na chama tawala. Chadema imeambulia kata moja ya Ibhigi mkoani Mbeya.

Matokeo hayo yameifanya historia mpya nchini katika uchaguzi kwa upinzani kupata matokeo mabaya ya uchaguzi katikati ya malalamiko.

Novemba 26, 2017, CCM ilitangazwa kushinda kata 42 kati ya 43 kupitia uchaguzi mdogo wa marudio nchini. Januari 14, CCM kilipata ushindi uchaguzi wa ubunge katika majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.

Katika chaguzi nne za mwaka huu, CCM imeshinda maeneo yote. Februari 17, CCM ilishinda jimbo la Kinondoni na Siha kabla ya Agosti 12, kushinda tena jimbo la Buyungu na kata 38.

Septemba 15 chama hicho tawala, kilishinda kata tatu na majimbo ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli na sasa kinajipanga kushiriki tena katika uchaguzi wa jimbo la Liwale na kata 37.

Katika chaguzi hizo, viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho wamekutana na changamoto ya kufunguliwa kesi mahakamani, kujeruhiwa na vifo kadhaa, hali ambayo imesababisha Chadema kutoa uamuzi wa kususia uchaguzi.

Uamuzi huo wa Chadema umekuwa mjadala mkubwa wa kisiasa. Wasomi na wanasiasa wana mawazo tofauti juu yake, baadhi wanasema ni mzuri na ulikuwa haukwepeki, lakini wengine wanasema kushiriki uchaguzi ni jukumu la chama cha siasa, bila kujali kitapata nini katika uchaguzi husika.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Joran Bashange, Katibu Mkuu wa NLD, Tozy Matwanga na Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi wa Vyama 11 vya siasa visivyokuwa na uwakilishi bungeni, Renatus Muhabhi ni miongoni mwa wanaunga mkono msimamo huo.

Kwa nyakati tofauti wanasema kuendelea kushiriki uchaguzi wenye kasoro za wazi na kuubeba upande mmoja kunahalalisha haramu dhidi ya vyama vya upinzani.

Hoja za viongozi hao zinaibuka juu ya malalamiko yasiyokoma ya mawakala wa vyama vya upinzani kunyimwa utambulisho wa kuwaruhusu kusimamia kura zao, hivyo kura kupigwa chini ya mawakala wa upande mmoja.

Chanzo cha tatizo

Hali imefikia hatua hiyo kutokana na malalamiko ya kila uchaguzi unaofanyika yanajitokeza ama kwa sura ileile. Ni suala la mawakala wa vyama vya upinzani, hasa Chadema, kukataliwa kwenye vituo vua kupigia kura.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikidai kwamba ama mawakala wake wananyimwa hati za viapo, au barua za utambulisho zinazotakiwa kuonyeshwa kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Mara nyingine hati hizo hucheleweshwa na kupatikana baadaye wakati uchaguzi unaendelea. Madai mengine ambayo hata hivyo yanakanushwa na mamlaka zinazohusika ni kuwa, mawakala wengine hukamatwa na polisi siku moja kabla au siku ya uchaguzi ili wasiwepo vituoni.

Mwisho wa matukio hayo ya kuzuiwa mawakala wa upinzani ni kituo cha kupigia kura kubaki na mawakala wa chama tawala pekee, wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Athumani Kihamia pamoja na kukiri kupokea malalamiko kuhusu kukataliwa kwa mawakala katika majimbo ya Monduli na Ukonga, alisema tatizo hilo si la jumla na limekuwa linasababishwa na wapinzani wenyewe kwa kuitaka kubadili mawakala na kuleta ambao hawajaapishwa.

“Hata huku Monduli niliko lilikuwapo, nimelifanyia kazi mimi mwenyewe na sasa kila kitu kinakwenda sawa.

Akizungumzia malalamiko ya Chadema, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage anasema “Kila chama kina hiari ya kushiriki na tume haiwezi kukilazimisha. Tume inaendelea kufanya tathmini ya uchaguzi baada ya kukamilisha itatoa taarifa.

“Kama uchaguzi ulifanyika kinyume cha sheria, wahusika walipaswa kufuata sheria kwa kwenda kutoa malalamiko yao kwenye vyombo husika badala ya kupeleka kwenye vyombo vya habari.”

Pamoja na uongozi wa NEC kuona malalamiko Chadema na upinzani si ya msingi, wachambuzi wa siasa na wanasiasa wanayatazama kwa jicho tofauti.

Profesa wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohammed Bakari anasema nafasi ya kupata ushindi kwa Chadema na upinzani kwa jumla imezidi kuwa finyu kutokana na mazingira ya kisheria, kikatiba pamoja na ya kisiasa.

Anasema uwezekano wa kushinda hata katika zile nafasi zenye matumaini umepotea.

“Sheria ni zilezile, Tume ni ileile, na huko nyuma kulikuwa na baadhi ya maeneo wangeweza kushinda lakini kwa sasa mazingira fulani ya kisiasa yaliyojitokeza, ambayo ukichanganya na udhaifu wa kisheria, kikatiba na muundo wa NEC, nafasi imekuwa finyu,” anasema Profesa Bakari.

Hata hivyo, msomi huyo wa masuala ya siasa, anafafanua kuwa pamoja na mazingira magumu kwa chama hicho kikuu cha upinzani, hoja ya kususia inatakiwa iendane na mikakati mingine mbadala, vinginevyo umaarufu na ushawishi wa chama hicho utaendelea kuporomoka zaidi.

“Uhai wa chama ni kushiriki kazi za siasa na chaguzi ni fursa kubwa ya chama kujitangaza na kuongeza ushawishi kwa maeneo mengi zaidi, sasa wanasusia chaguzi hizo wakati huo wamezuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa, kususia bila mbadala itavunja moyo, na inawezekana kabisa chama kikaendelea kupoteza umaarufu,” anasema Profesa Bakari.

Anasema nguvu ya chama huporomoka baada ya wafuasi na wanachama kuanza kukata tamaa ya kushiriki chaguzi.

“Wapiga kura wana tabia ya kufanya tathmini, je nikienda kushiriki kura yangu itakuwa na thamani? Au utamaduni ni uleule tu? Mtu anaona hakuna umuhimu wa kupiga kura, anakata tamaa ya kushiriki tena, ni dalili za kufanya vibaya zaidi kwa chama,” anasema.

Anasema kwa bahati mbaya zaidi, vyama vya upinzani vimezuiliwa kufanya mikutano ya hadhara huku chama kikiwa na wanachama waliojiandaa kuwa viongozi kupitia nafasi za uwakilishi wa wananchi.

Mbadala wa kususia chaguzi

Pamoja na mazingira hayo magumu kwa Chadema, baadhi ya wachambuzi wa duru za kisiasa wanahofia dalili za Taifa kurejea katika mazingira ya chama kimoja.

Hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi wa upinzani kuhamia CCM kisha kurejeshwa tena katika majimbo na kata zilezile, kuzuiliwa kufanya siasa za majukwaani, viongozi wa Chadema kufunguliwa kesi za uchochezi, madai ya dosari za kisheria, kikatiba na Tume ya Uchaguzi kupuuzwa.

Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anaonyesha wasiwasi wa nchi kuelekea kwenye mfumo wa chama kimoja. “Labda turudi kwenye chama kimoja na upinzani uwe ndani ya CCM kama tulivyokuwa awali. Tulikuwa na Tanu na ndani yake kulikuwa na upinzani,” anasema. Profesa Bakari anasema mahakama ni sehemu sahihi ya kutumika kudai mabadiliko ya kisheria, kikatiba na udhaifu unaoendelea lakini changamoto iliyopo ni mtazamo hasi uliojengwa na Chadema.

“Upinzani Kenya wamekuwa wakitumia vizuri mahakama na wanafanikiwa lakini hapa nchini wamejenga dhana potofu kwamba mahakama haziwatendei haki, sasa changamoto ni kwamba wanadai yawepo mabadiliko ya kikatiba, kisheria na CCM haiko tayari, pengine inategemea zaidi ushirikiano wa vyama na asasi za kiraia,” anasema.

Muhabhi anavitaka vyama vyote vya upinzani bila kujali tofauti zao, kuitisha mkutano wa kitaifa kwa ajili ya kupitisha tamko la pamoja kuhusu hali ya kisiasa na ushiriki wa chaguzi zijazo.

“Chadema wamechukua uamuzi sahihi kususia chaguzi hizi maana zimekuwa za kichefuchefu, kinachotakiwa ni kukutana vyama vyote, sisi tuna umoja wa vyama 11 visivyo na uwakilishi, bila kujali tofauti zetu wote upinzani tukutane na tuache unafiki, tutoe tamko la kususia chaguzi zote halafu tuone kama CCM wataingia peke yao kwenye uchaguzi,” anasema.

Muhabi anasema hatua hiyo itasaidia kuchochea mabadiliko ya kisheria, kikatiba na udhaifu unaotokana na muundo wa Tume ya Uchaguzi.

Tutarajie nini 2020

Profesa Shumbusho anasema hali haiwezi kubadilika hadi kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020. “Kwa nini waendelee kuingia kwenye uchaguzi ambao wanajua hawatashinda? Nafikiri uamuzi wao ni sahihi, waache hadi hapo Katiba itakapobadilisha Tume ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi,” anasema.

Wachambuzi wengine wanasema tatizo kubwa ni viongozi wa NEC na wasimamizi wa uchaguzi wanateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama shindani.

Ushauri wa Lowassa,

Pamoja msimamo wa Chadema kama chama, mjumbe wake wa kamati kuu, Edward Lowassa anasema suluhisho la kuwa na uchaguzi huru ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi vinginevyo CCM itaendelea kutangazwa kushinda katika kila uchaguzi.

Anasema ili kufanya uchaguzi uwe wa huru na haki, ni lazima kuwe na sheria ambayo itafanya tume iwe inabanwa. “Lazima kuwe na chombo ambacho kinaibana tume, lakini sasa tume haiwezi kubanwa.”

Alisema jambo jingine ambalo linafanya uchaguzi huo kutokuwa huru ni kutokana na wakurugenzi na maofisa wanaosimamia uchaguzi kuwa wateule wa Rais.

“Wakurugenzi wengi walioteuliwa ni makada wa CCM ambao walianguka katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2015, Rais akawateua, usitarajie kama wapo huru hao,” alisema.