HOJA BINAFSI: Ubinafsi wa fisi, maisha kubet

Muktasari:

  • Sasa maji yamekauka nyumbani na bahari inazidi kuongezeka. Eti wewe ukishinda bahari inashinda. Wanapaswa kusema kwamba wewe ukishinda, bahari inashinda, ukishindwa, bahari inashinda zaidi, ukifilisika, mawimbi ya bahari yanabaki yanakucheka kwa kejeli.

Juzi nilitembelewa na jamaa mmoja ambaye alikuwa na madonge yake.

‘Unajua Makengeza, ulivyoandika kuhusu kubet, ulinishtua na nilikusifu kweli. Kweli kubet ni sawa na kumwaga maji ya ndoo baharini kwa mategemeo kwamba baada ya hapo utapata maji ya kunywa. Ningependa kutamba na mimi kwamba siwaelewi hawa wanaomwaga maji hivyo, lakini ukweli ni kwamba hata mimi nilipeleka ndoo nyingi baharini.

Sasa maji yamekauka nyumbani na bahari inazidi kuongezeka. Eti wewe ukishinda bahari inashinda. Wanapaswa kusema kwamba wewe ukishinda, bahari inashinda, ukishindwa, bahari inashinda zaidi, ukifilisika, mawimbi ya bahari yanabaki yanakucheka kwa kejeli.

Yaani Makengeza nilibet, nilibet, kila nikitaka kuacha kubet nikawasikia watangazaji wa redio wanaupamba huu mpango mzima wa kubet kana kwamba wamecheza na kushinda na wao. Kumbe wanalipwa ili waturubuni. Ndiyo. Nikaanza kutafakari kama ulivyosema. Ili upate mshindi wa elfu kumi tu, lazima watu ishirini wawe wameweka dau. Hivyo fursa ni moja kwa ishirini na ukishafanikiwa kupata, tayari umeshatumia elful kumi kwa mia tanotano zako. Sasa ili mtu mmoja apate milioni ishirini, itabidi waweke wangapi. Naona mpango kama DECI vile.’

‘Si ndiyo. Ndiyo maana unaona maofisi makubwamakubwa ya kubet yanafunguliwa kila mahali huku asilimia 99 ya watu wanaobet wanazidi kuvaa mitumba. Au sijui, kwa lugha ya siku hizi, tuviite viwanda vya kubet. Kwa kubet tu tunaweza kufikia karibu nusu ya viwanda vyote vinavyotakiwa katika mipango yetu ya taifa.’

‘Ni kweli Makengeza, na majuto ni mjukuu lakini sijui wengine watakuja kujuta lini. Lakini tuache hayo, mimi nadhani kuna aina nyingine ya kubet ambayo nayo ni hatari.’

‘Aina gani?’

‘Ujasiriamali.’

‘Eti nini?’

‘Ndiyo ujasiriamali. Oh inatumia akili kidogo kuliko kuchagua namba tatu, labda tufananishe na kuweka mkeka maana hapo angalau unaweza kufikiri kidogo.’

‘Lakini wewe Bwana unawezaje kulinganisha mpango mkuu wa kuwatoa vijana kwenye umaskini na hali ya kubet?’

‘Ninao uhakika vijana wengi hawaoni tofauti. Kila upande ni kubahatisha. Kwa mfano wewe utafanikiwaje huku unajasiriamali na bidhaa zilezile za mwenzio? Kuna tofauti gani na bahati nasibu zaidi ya kwamba bahati nasibu haihitaji juhudi na maarifa. Cheza bila jasho. Unafikiri wajasiriamali wangapi wanafanikiwa na wangapi wanashindwa ili yule mmoja afanikiwe? Hebu tuchukue mfano wa dada zetu. Unaenda barabarani jioni unakuta zaidi ya dada ishirini wanauza chapati. Chapati zilezile. Ishirini zaidi samaki wa kupima …

‘Wa kukaanga Bwana.’

‘We huwezi kujua. Walikosea kwenda kupima kwa wakubwa ndiyo maana wakaumbuka. Wakipima kwa sisi Waswahili, nani atapiga kelele? Rula oyeee!’

‘Mmh, rafiki yangu, mbona hivyo? Kitu gani kimekuswibu.’

‘Maisha si unayaona jamani. Hawa ishirini nao wanauza samaki walewale. Maandazi, katlesi, kila kitu vilevile. Siwalaumu dada zetu wote wanaohangaika hivyo, lakini anayewaambia watakuja kuwa milionea kwa maandazi haya anawadanganya.’

‘Lakini kwa misingi ya ujasiriamali, atakayeshinda ni yule anayepika vizuri zaidi, au kutangaza bidhaa zake vizuri zaidi.’

‘Usinichekeshe Bwana. Kweli soko linaweza kumudu watu ishiriniishirini wanaouza vitu vilevile? Lakini tunaimbiwa kwamba mtu asitake kufanya kazi ofisini, bora kujiajiri, eti uko huru, eti nini na nini lakini wewe bado ni mtumwa wa soko na nakwambia wengi wanashindwa kazi au wanabaki kuhangaika kupata angalau za kula siku ile. Kisha hawa manabii wa ujasiriamali wanataka kutuaminisha kwamba tukishindwa ni kosa letu. Si kosa letu, ni kosa la mfumo.’

‘Mbona unatia chumvi sana.’

‘Wala sitoi chumvi. Nakwambia wengi wanabaki wanaomba miujiza kama vile kubet. Juzi hata mimi nilikuwa muujiza kwao maana nilikwama kwenye jiwe kubwa baada ya malori kujaza njia zote huko bandarini … kwa nini hawatangazi kwamba malori watakuwa na dansi yao? Sasa niliwaita vijana ambao walikuwa wamekaa pembeni. Walinisukuma vizuri sana, nikawapa hela. Mmoja alisema … lakini si unajua Bwana, tusingedai hela lakini hali ngumu … hali ngumu. Nilishangaa alivyoomba radhi lakini nilimwelewa. Sasa ili ufanikiwe, lazima ubuni kitu kipya, ambao si wengi wenye sifa hizo, au uibe ubunifu wa wengine, labda wengi wana sifa hiyo, au utengeneze na kutangaza vizuri kuliko mwenzio, lakini hii si rahisi kwa rasilimali ndogo tuliyo nayo. Utabuni kitu gani kipya kama muuza maandazi? Au mwenye bodaboda maana nazo zinauana kibiashara siku hizi. Au kuuza soda kwenye mabasi? Nawaheshimu sana wanaohangaika hivyo. Hawakati tamaa, wanaendelea kupambana na hali yao, lakini ni ukatili kuwadanganya kwamba ndiyo siri ya kuwa milionea.’

‘Kwa hiyo ina maana unabet kamtaji kako ukiomba Mungu utafanikiwa kuliko mwenzio?’

‘Si ndiyo. Kwa nini tudanganyane? Wachache kweli watafanikiwa lakini si wengi.’

‘Na hii mikopo ya ujasiriamali?’

‘Kwa walio wengi ni sawa na kuwapa pesa za kwenda kubet tu. Tena kubet ni bora maana utarudi nyumbani na kulala badala ya kuhangaika na mwishowe kushindwa. Nimesoma utafiti mahali ambapo hii mikopo inafanya kazi vizuri kwa wale ambao tayari wamejijenga, wanajua wanalolifanya na kale kamkopo ni kama kumpigia teke chura. Lakini kwa walio wengi ni kama pesa za dezo waweze angalau kuishi zaidi.’

‘Rafiki yangu naona uko hasi sana leo, sijui kitu gani kimekuvuruga. Mimi naona ujasiriamali umewezesha vijana wengi kujikimu. Bila mkono kwenye kinywani wataishije?’

‘Nimekubali kwamba wengi wanajikimu hivyo lakini sipendi itikadi ya manabii wa ujasiriamali eti bora kujiajiri. Anayeajiriwa ni mtumwa. Thubutu. Kwani walimu, wauguzi, wahasibu wote ni watumwa. Mtu akifanya kazi anayoipenda na kupata ujira wa haki katika kazi yake, utumwa uko wapi. Hawa wanaohangaika kujikimu kila siku bila matazamio ya mshahara wala masihara wanakuwa watumwa zaidi nakuambia.’

‘Duh, rafiki yangu.’

‘Tuangalie hali halisi. Lakini tatizo la pili tunaliona sasa. Zamani, tulikuwa na umoja wa wafanyakazi, watu waliungana kupigania haki zao kwa pamoja wakijua kwamba umoja ni nguvu lakini siku hizi, tunasema nini? Kupambana na hali yako. Kwa hiyo wewe na waandishi wenzio mlifanya nini mbele ya sheria mpya. Wengine walikuwa wajanja wa kuhamisha, wengine walitangaza kujiua kibiashara na wengi hasa walijipeleka kimyakimya bila kubisha ingawa wanajua kwamba sheria hii inawapiga chini na kutisha uhai wa biashara zao. Ndiyo itikadi ya ujasiriamali, ubinafsi wa fisi kabisa.’

‘Labda kuna ukweli ndani yake kidogo. Ni kweli, kila tasnia ikiminywa, hakuna hatua za pamoja. Kama unavyosema, kila mtu anatafuta njia yake ya kuishi. Kwenye huduma za jamii vivyo hivyo. Badala ya kuungana na kupigania shule bora za serikali, kila mmoja wetu anatafuta nafasi kwenye shule binafsi. Kwenye afya vivyo hivyo. Pambana na hali yako, si ungana na mwenzio mweze kupambana vizuri. Ajabu ni kwamba wenye umoja wa kweli ni wenye bodaboda pekee. Umguse mmoja na ishirini wanakufuata. Bahati mbaya wanaitumia vibaya lakini ni mfano mzuri. Sisi wengine tutazama mmojammoja katika kupambana na hali yetu. Nakuambia …’

‘Yawezekana kuna ukweli ndani yake. Mambo yote tisa …