Ubunge mali ya chama au mali ya wapiga kura

Muktasari:

  • Uamuzi huo unafuatia agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kwa Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kuwaandikia barua wabunge wote ambao hawakuhudhuria kikao cha Bunge siku ya kupigia kura Bajeti ya Serikali.

Chama cha Mapinduzi (CCM) mapema wiki hii kimetangaza nia ya kuchukua hatua kwa wabunge wake wasiohudhuria vikao vya Bunge bila sababu za msingi.

Uamuzi huo unafuatia agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kwa Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kuwaandikia barua wabunge wote ambao hawakuhudhuria kikao cha Bunge siku ya kupigia kura Bajeti ya Serikali.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, kwa sasa wanafanya uchunguzi wa wabunge hao ambao hawajahudhuria vikao vya Bunge kuanzia mwaka 2016 na kwamba endapo kuna ambao watathibitika hawakuhudhuria vikao hivyo bila sababu za msingi watachukuliwa hatua.

Dk Bashiru alienda mbali zaidi na kusema kuwa chama hicho kimeamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu Bajeti ni chama, kinaomba fedha serikalini ili kitekeleze ilani yake na kwamba huo ni utaratibu wa ndani ya chama.

Anasema hatua hiyo inalenga kujenga nidhamu ndani ya chama hicho kwa kuwa ubunge ni mali ya chama.

“Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017, nyongeza B, inaeleza kuwa kuna kanuni zinazotambua kamati ya wabunge wa CCM na huko kuna utaratibu wao na suala la mahudhurio ni la CCM kwa sababu ubunge wao, ni wa chama na wao wamepewa dhamana tu,” anasema Dk Bashiru.

Misingi ya demokrasia

Hatua hiyo imezua maswali miongoni mwa wadau wa siasa nchini, wakikosoa hatua hiyo kwamba inavunja misingi ya demokrasia iliyopo na uhuru wa mbunge binafsi.

Wachambuzi hao wanatofautiana na kauli ya Dk Bashiru kwamba ubunge ni mali ya chama kiasi cha kutaka kuwapangia nini cha kufanya na kusema.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, chama ni tiketi tu ya mbunge kuingia bungeni kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kwamba mara baada ya kuwa mbunge anapaswa kutekeleza yale ambayo wananchi au wapiga kura wake wanataka.

Hata hivyo, Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza anakubaliana na chama chake akisema kuwa mbunge anawajibika kwa chama, hivyo anapaswa kutekeleza yale ambayo chama kinataka.

Mtazamo wa kisheria

Lakini, wakili wa kujitegemea, Peter Mshikilwa yeye hakubaliani na hilo na badala yake anasema kuwa kazi za mbunge ziko kikatiba na msingi mkuu ni kuwawakilisha wananchi na siyo chama.

Mshikilwa anasema kazi za mbunge zimeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hakuna mtu au chama kinachoweza kuzibadili.

Kwa mujibu wa Mshikilwa, mbunge ana kazi kuu tatu kikatiba ambazo ni kuwawakilisha wananchi, kusimamia serikali na kutunga sheria.

“Katika kazi hizo zote ambazo anapaswa kufanya, mbunge anaongozwa na nguvu ya kisheria ya uwakilishi, anapokwenda kuomba ridhaa ya chama chake kuwa mbunge lengo ni kuwawakilisha wananchi na si vinginevyo,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Mshikilwa, mara baada ya mbunge kupata ubunge, anapaswa kuwawakilisha wananchi katika masuala mbalimbali.

“Sasa tuna Katiba, hili suala la kuwaandikia barua wabunge na kuwapa vitisho linaturudisha nyuma katika mfumo wa chama kimoja kushika hatamu.

“Wakati huo wa mfumo wa chama kimoja ilikuwa ni sawa jambo likitokea kuwa na vikao vya party caucus na kukubaliana jambo fulani,” anaongeza.

Mwanasheria huyo anasema kitendo cha chama kuwapangia kazi za kufanya wabunge wake ni kukiuka Katiba, lakini pia inasababisha hofu kwa wabunge kutimiza majukumu yao.

“Huwezi kuwa na mbunge ambaye wakati wote atakuwa na hofu ya ama kusimamishwa au kufukuzwa uanachama wake kwa sababu tu hajahudhuria vikao vya Bunge, hili haliko sawa lazima tusimamie Katiba yetu inasema nini,” anasisitiza Mshikilwa.

Katibu wa wabunge CCM

Tofauti na maoni hayo, Rweikiza anasema, “Hatuwezi kuwa na mbunge asiyefuata taratibu na kujiamulia mambo yeye mwenyewe bila kuzingatia maslahi ya chama.

Mbunge huyo wa Bukoba Vijijini anasema mbali na kutekeleza yale ambayo chama kinataka, ni lazima mbunge ahakikishe anashiriki katika masuala yote ya Bunge.

Hata hivyo, Mjumbe huyo wa kamati Kuu ya CCM, anasema mbunge kutokuwapo bungeni wakati wa upigaji kura kupitisha Bajeti si jambo la ajabu.

Rweikiza anafafanua kuwa mbunge ni binadamu kama wengine, hivyo anaweza kushindwa kuhudhuria vikao kutokana na sababu mbalimbali.

“Mbunge ana jukumu la kuhudhuria vikao vya Bunge na si suala moja tu la kupiga kura, anapaswa kushiriki katika kamati, kujadili mijadala ndani ya Bunge na pia kushiriki shughuli zozote za kibunge,” anasisitiza.

Anataja mambo yanayoweza kusababisha mbunge kutohudhuria kikao kuwa ni pamoja na ugonjwa, kufiwa au kuomba ruhusa kwa spika au katibu wa wabunge kuhudhuria shughuli za kibiashara au utoro.

“Zote hizo ni dharura ambazo awe mbunge ama wa CCM au upinzani anaweza kuwa nazo, hivyo inategemea hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu gani,” anaongeza Rweikiza.

CUF yaponda

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya anasema kitendo kilichofanywa na chama hicho tawala si sawa kwa kuwa Bunge ni mali ya Watanzania.

“Inategemea katiba yao inasemaje, lakini ukweli ni kwamba wabunge wanapaswa kuwawakilisha wapiga kura wao wanataka nini na si vinginevyo,” anasisitiza Kambaye ambaye anamuunga mkono Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Hata hivyo, Kambaya anasema hilo ni tatizo la siasa za Afrika na siyo Tanzania pekee ambako chama kinataka kuwa na nguvu ya kumdhibiti mbunge wake, jambo ambalo halina mantiki.

“Msimamo wa chama chetu katika hili ni kuwaacha wabunge wenyewe wasimamie matakwa ya wananchi na wapiga kura wao, chama ni njia tu ya kumfikisha mbunge kufikia matarajio yake,” anaongeza Kambaya.

Kauli ya Mrema

Maoni hayo si ya wanasiasa wote, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema kwa upande wake anasema CCM imechelewa kuchukua hatua kwa sababu wabunge wengi hawana nidhamu katika utendaji wao wa kazi.

“Kwa uzoefu wangu, mimi nimewahi kuwa mbunge lakini pia ni mwenyekiti wa chama, nimeshuhudia wabunge wengi hawaudhurii vikao vya Bunge bila sababu za msingi na kwa sababu hakuna chama chenye utaratibu wa kuwadhibiti wabunge wake, hilo limeachwa na matokeo yake unakuta siku viti vipo vitupu,” anaongeza.

Mrema anasema kuna wakati hali ilikuwa mbaya zaidi na siku moja alishuhudia hoja mbalimbali zinashindwa kupitishwa kutokana na kukosekana kwa idadi ya wabunge inayotakiwa, jambo lililomshutua hata Spika Job Ndugai ambaye aliwaonya na muda mfupi baadaye taasisi hiyo ikaanzisha utaratibu wa kusaini kwa kuweka alama ya kidole gumba mara mbili kwa siku.

“Kutoudhuria vikao vya Bunge ni kosa. Waende mbali kwa kutoa adhabu kali zaidi, pengine itasaidia kurudisha nidhamu ambayo kwa muda mrefu imetoweka,” anaongeza Mrema.

Mrema anasema wabunge wengi hata wa upinzani badala ya kufanya walichotumwa wanaenda kuchukua posho tu na kushindwa kushiriki mijadala na shughuli mbalimbali za kibunge kama kuhudhuria mikutano ya Kamati za Bunge, jambo linalochangia hoja nyingi kupita bila kujadiliwa kwa kina.

“Wasipokuwa macho Bunge litakuwa kama ‘kijiwe’ badala ya kuwa sehemu ya kutunga sheria. Watafanya wanavyotaka kwa kuwa chama hakiwezi kuwachukulia hatua,” anasisitiza mrema.

Mrema anatoa mfano kuwa yeye pia alifanya kosa wakati alipokuwa mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, chama hicho kilisambaratika kwa kuwa tu walishindwa kuwadhibiti wabunge wasio na nidhamu.

“Wabunge wetu hawakuwa na nidhamu, baadhi walikuwa hawaudhurii mikutano, wengine walikuwa wanaongoza migomo ndiyo maana NCCR ilisambaratika,” anasema Mrema

Mrema anasema usipowadhibiti wabunge kila mmoja atafanya anavyotaka na itafika siku hakutakuwa na koramu ya kupitisha bajeti jambo ambayo itaathiri utendaji wa kazi.