Ubunifu ulivyowasukuma wanawake kutengeneza juisi ya viazi

Muktasari:

  • Katika kilele cha maonyesho ya wakulima maarufu Nanenane mjini Morogoro juisi hiyo inayotengenezwa kwa viazi lishe vyenye rangi ya karoti, ilikuwa miongoni mwa mambo yaliyovutia wengi waliotembelea banda la Ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sugeco).

Imezoeleka kuona viazi vikitumika kama mlo lakini kumbe vinaweza kutumika katika kutengeneza kinywaji laini (juisi) yenye ladha na mwonekanao mzuri.

Katika kilele cha maonyesho ya wakulima maarufu Nanenane mjini Morogoro juisi hiyo inayotengenezwa kwa viazi lishe vyenye rangi ya karoti, ilikuwa miongoni mwa mambo yaliyovutia wengi waliotembelea banda la Ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sugeco).

Juisi kwa kawaida imezoeleka hutengenezwa kwa matunda ya aina mbalimbali ikiwamo nanasi, embe, tikititi maji, miwa, parachichi na tufaa, hivyo viazi lishe kutumika kutengeneza juisi ni habari mpya na njema kwa wajasiliamali wa sekta hiyo.

Veronica Kavishe ni mmoja wa wajasiriamali ambaye amenufaika na mafunzo aliyoyapata kutoka kwa wataalamu wa lishe wa Sugeco jinsi kutengeneza juisi hiyo na hatimaye akaamua kuitambulisha kwenye maonyesho hayo.

“Ingawa utengenezaji wake ni mgumu kidogo tofauti na ule wa matunda niliyozoea lakini najisikia furaha maana imewavutia wateja wengi wakiwemo watoto,” anasema Kavishe.

Anabainisha kuwa kugundulika kuwa kiazi hicho kinafaa kwa juisi imekuwa neema kwake hasa kwa kuwa matunda yamekuwa adimu hasa maembe, hivyo amepata mbadala wa kuendeleza biashara yake na kuwa na uhakika wa kujiingizia kipato.

Anasema juisi hiyo anauza kwa bei ya Sh1,000 kwa glasi, ambapo siku za mwanzo wa maonyesho hao alijuta kutengeneza kiasi kidogo, kwani iliisha haraka huku wateja wakiwa wanahitaji.

“Utengenezaji wake hii juisi unachukua muda mrefu katika kuiandaa kwani viazi vikishamemwa vinatakiwa kupikwa, vikiiva, vinapondwa, kisha unaacha vipoe kidogo kabla ya kuvisaga kwenye blenda huku unakadiria maji kulingana na wingi wa viazi,” anasema.

Anasisitika kwamba mafunzo aliyopata ni kwamba juisi yoyote inapaswa kutengenezwa kwa usafi wa hali ya juu, hivyo ni muhimu kwa mtengenezaji kuhakikisha mikono yake ni safi.

“Lazima kuvaa kufunika mdomo kwa mask, pia kuvaa mipira kwenye mikono(gloves), kama ni matunda lazima yaoshwe kwa maji ya uvuguvugu kabla ya kumenywa na kukatwa katwa, pia hata unapaswa kuchuja kwenye vyombo ambavyo vimeoshwa kwa maji safi na kukaushwa,” anasema.

Mtaalam wa Lishe wa Sugeco, Jolenta Joseph anaeleza kuwa kiazi lishe kinachotumika katika kutengeneza juisi hiyo ni Jeuledi ambacho kina ulaini ambao ukikiponda unaweza kunywa uji wake unaweza kunywa bila hata kuchuja.

Joseph anasema kwa mahitaji ya juisi ya viazi hivyo inachanganywa ili kuifanya iwe na ladha ya uchachu kwa mbali ambayo husaidia pia katika ufyonzaji wa chakula.

“Ladha ya kiazi hupooza hasa inapofanywa kuwa juice, hivyo ili kuichangamsha tunalazimika kuiongezea tunda lenye ladha ya uchachu kiasi kama vile passion au ukwaju, ambavyo husababisha mnywaji ajisikie hamu ya kunywa hata zaidi ya glasi moja,” anasema Joseph.

Anasema pia katika kuhakikisha juisi hiyo inakuwa bora kwa afya na siyo ya kuburidisha kinywaji pekee, mwandaaji hutakuwa kuongeza kiwango kidogo cha mafuta wakati viazi lishe vikiwa vinachemka, hatua hiyo husaidia kurahisisha ufyonzwaji wa vitamin A iliyopo ndani ya viazi hivyo.

Joseph anaeleza kuwa pia juisi inapokamilika vyombo vinavyotarajiwa kutumika katika kunywa navyo vinapaswa kuhakikishwa kuwa ni safi na salama kwa afya ya mtumiaji.

“Kwa pale Sugeco mjasiriamali anayejihusisha na shughuli ya kutengeneza juisi hiyo ana chombo kinachoitwa ‘sterilizer’ ambayo hutumiwa katika kupasha moto ili kuua vidudu hatari vinavyoweza kuwa kwenye vyombo, usalama wa afya ni muhimu sana kwenye biashara hasa hizi za vinywaji na vyakula,” anasema.

Ukwaju na passion ni matunda yanayopatikana kwa wingi tofauti na viazi lishe ambavyo kwa sasa vinalimwa katika maeneo machache nchini, ikiwamo katika wilaya za Gairo na Kilosa ambapo mradi wa kuboresha lishe na kuongeza kipato cha ngazi ya kaya unatekelezwa.

Mradi huo unalenga katika kuongeza kipato cha wakulima wadogo kwa ngazi ya kaya kwa kusaidia familia 3,000 kuzalisha, kutumia na kuuza mazao yenye virutubisho, unakelezwa na Segeco, unasimamiwa na Farm Afrika na kufadhiliwa na Big Lottery.

Anashauri kwamba kama unahitaji kutumia ukwaju unapaswa kuandaa kwa kuuosha kisha unaweka kwenye sufuria yenye maji ya saizi na injika jikoni uache uchemke kwa robo saa ili kuua wadudu hivyo kuufanya uwe salama kwa lishe.

Anasema baada ya kuuchemsha unapaswa kuuacha upoe kwa muda kisha unakoroga na mwiko ukijitahidi kutenganisha mbegu na baada ya hapo unaweza kuchuja au kusaga kwa chujio au kusaga kwenye blenda.

Ukwaju licha ya kuongeza ladha kwenye juisi ya viazi pia inapunguza wingi wa lehemu (cholesterol) na hivyo kuimarisha afya ya moyo.

“Pia ukwaju una viuasumu mwilini ‘antioxidants’ ambavyo inatajwa na wataalamu wa afya kuwa unasaidia huzuia saratani, kushusha joto la mwili na kuondosha homa,” anasema.

Wataalam wa afya wanabainisha kwamba husaidia myeyusho na mmeng’enyo wa chakula na kuondoa kuvimbiwa, kiungulia au gesi, pamoja na kusaidia kurahisisha choo (laxative). Pia, husaidia ngozi kuwa nyororo