Uhusiano kati ya serikali kuu na serikali za mitaa

Muktasari:

  • Kuhama kunaleta furaha na vifijo kwa wanachama wa CCM na ni kilio kwa upande wa vyama vya upinzani. Tusiokuwa na vyama na kubaki na uzalendo wetu, tunabaki na maswali mengi na kuumizwa na gharama hizi za chaguzi ndogo ambazo zinaendelea kulitesa taifa letu.

Baada ya wimbi kubwa la madiwani na (wabunge wachache) kuhama kutoka kwenye vyama vyao vya siasa na kutimkia chama tawala cha CCM na jambo hili kuendelea kuligharimu taifa fedha nyingi kurudia chaguzi, fedha ambazo zingeweza kufanya mambo mengine ya maendeleo ni muhimu kujadili na kuhoji kama kweli Watanzania wanafahamu uhusiano uliopo kati ya Serikali Kuu na serikali za mitaa.

Kuhama kunaleta furaha na vifijo kwa wanachama wa CCM na ni kilio kwa upande wa vyama vya upinzani. Tusiokuwa na vyama na kubaki na uzalendo wetu, tunabaki na maswali mengi na kuumizwa na gharama hizi za chaguzi ndogo ambazo zinaendelea kulitesa taifa letu.

Wale wanaohama vyama vyao vya siasa, wanatoa sababu ya kumuunga mkono Rais. Ambalo hawatuambii ni je, ni lazima wahame vyama vyao na kusababisha gharama kubwa au wanaweza kukaa walipo na kuendelea kumuunga mkono?

Tuache ushabiki wa vyama vya siasa, ushabiki huu hauwezi kutufikisha popote. Hakuna ushahidi wa kihistoria wa ushabiki wa kisiasa kulivusha taifa lolote lile duniani. Ushabiki wa kisiasa unazalisha maasi. Tusitamani maasi kwenye taifa letu. Hivyo kila anayelitakia mema taifa letu, ni muhimu azingatie Katiba na kufuata sheria.

Maswali muhimu

Ingawa wananchi wanaonyesha kuzikubali serikali za mitaa, swali la kujiuliza ni je, mambo haya mawili serikali za mitaa na Serikali kuu yako wazi kwa Watanzania wote? Je, majukumu ya serikali hizi mbili yanafahamika vizuri kwa wananchi? Je, kuna uhusiano gani kati ya serikali za mitaa na Serikali kuu?

Lengo la makala hii ni kujaribu kuweka bayana uhusiano uliopo katika ya Serikali Kuu na serikali za mitaa. Kwa kufahamu uhusiano uliopo, ufanisi utaongezeka na uwajibikaji kwa pande zote; wananchi kwa upande mmoja na Serikali zote mbili kwa upande mwingine, utakuwa mkubwa na kusaidia kuharakisha maendeleo katika taifa letu. Madiwani wanaohama vyama vyao na kutusababishia hasara kubwa ya kurudia uchaguzi, watagundua kwamba si lazima kuhama, wanaweza kukaa kwenye vyama vyao na kuendelea kutekeleza wajibu wao na hata kumuunga mkono Rais.

Je, serikali za mitaa ni zipi? Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, “serikali za mitaa” maana yake ni vyombo vya kiserikali vilivyoundwa kwa mujibu wa ibara ya 145 ya Katiba hiyo kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka ya umma. Vyombo vya kiserikali vilivyoundwa na sheria kufuatia maelekezo hayo ya Katiba ni halmashauri za wilaya/ miji/manispaa/majiji/ halmashauri za vijiji. Majukumu ya mamlaka za serikali za mitaa yameainishwa katika Katiba na Sheria za Serikali za mitaa, ambayo ni kuhusu mahusiano ya vyombo hivi na Serikali kuu.

Sheria za serikali za mitaa na Sheria nyingine za nchi zinaeleza kwa undani zaidi majukumu na mipaka ya serikali za mitaa na vyombo mbalimbali vya Serikali kuu ili kuondoa mwingiliano. Kwa hiyo, mahusiano kati ya serikali za mitaa na Serikali kuu yanatawaliwa na sheria, na kamwe hayategemei maelewano kati ya viongozi na watumishi wa umma walio katika serikali za mitaa na Serikali kuu. Si mambo ya kujuana, hapana, kila kitu kinaongozwa na sheria. Anayefanikiwa si kwa vile ana mvuto, bali ni kwa vile anakuwa amefuata na kuzisimamia sheria zilizopo.

Hivyo kama suala ni kusimamia sheria, mtu unaweza kusimamia sheria ukiwa upinzani au ukiwa chama tawala. Si lazima kuhama chama cha siasa ili usimamie sheria. Maana sheria ni sheria na haifungamani na chama cha sheria. Tukitaka kusimamia sheria kufungamana na vyama vya siasa, tutakuwa tunatengeneza taifa la aina yake duniani na taifa hili haliwezi kuwa na maisha.

Mamlaka ya serikali hizo

Je, Serikali kuu na serikali za mitaa zina nafasi gani katika utawala na uongozi wa nchi? Kwa mujibu wa Ibara ya 6 na Ibara ya 151 ya Katiba ya Tanzania, neno “Serikali” maana yake ni pamoja na Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, serikali za mitaa na pia mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya serikali yoyote. Hivyo ni dhahiri kwamba kuna mamlaka tatu za kiserikali katika nchi moja. Hali hii inaweza kusababisha misuguano. Njia pekee ya kuondoa hali hiyo ni kwa kuainisha kisheria majukumu na mahusiano ya kiutendaji baina ya serikali hizo.

Kwa mfano, serikali za mitaa ni vyombo vya kiserikali vilivyoundwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka kwa umma. serikali za mitaa ni vyombo vyenye mamlaka na madaraka katika eneo husika la Tanzania ambavyo vinashughulikia masuala yaliyoainishwa katika Katiba na sheria zinazoviunda.

Kwa upande mwingine Serikali kuu ni chombo chenye mamlaka na madaraka katika nchi nzima kwa mujibu wa Katiba na sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge.

Ingawa serikali hizi mbili chimbuko lake ni Katiba ileile, lakini kazi zake na majukumu yake yanatofautiana katika upana na maeneo ya utekelezaji na uwajibikaji. Wakati serikali za mitaa zinajishughulisha na maeneo husika, kama vijiji, mitaa, kata na wilaya, Serikali kuu inajishughulisha na taifa lote. Ukiangalia kwa undani, majukumu yaliyo mengi, kazi za vyombo hivi viwili ni ya kukamilishana au kwa maneno ya kisasa ni ya ubia.

Hata hivyo, iko wazi kisheria kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye serikali moja. Ndani ya serikali hii moja kuna serikali za mitaa nyingi ambazo zinafikia 10,000, Ili kuhifadhi utaifa katika nchi moja, ni lazima Katiba na Sheria za nchi kuwa wazi kwamba Serikali kuu ndiyo kiongozi wa nchi na hivyo serikali za mitaa zinatakiwa kuzingatia sera, sheria na kanuni za kitaifa katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali za mitaa.

Sera ya uboreshaji wa serikali za mitaa ya 1998 inaelekeza kwamba mahusiano baina ya serikali za mitaa na Serikali kuu yatatawaliwa na sheria. Hili ndilo muhimu kuzingatia hapa. Tuna sheria na sheria hizi ni za taifa letu na wala si za chama chochote cha siasa. Aidha, mahusiano yataegemea zaidi katika mashauriano, majadiliano na maelewano badala ya kuegemea katika kutoa, kupokea na kutekeleza amri kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Msimamo huu ni chimbuko la serikali za mitaa kufanya vizuri na kukubaliwa na wananchi. Kutokana na msimamo huo wa sera, sheria za serikali za mitaa Na.7 na 8 za 1982 (Vifungu 174A na 54A kwa mfuatano) zimeelekeza wazi jinsi mahusiano kati ya vyombo hivyo yanavyopaswa kuwa kwa kutaja majukumu ya Serikali kuu mintarafu uwezo na kazi serikali za mitaa.

Kwa kifupi au kwa maneno mengine wajibu wa Serikali kuu ni ule wa kuziwezesha serikali za mitaa kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kisheria.

Viongozi na vyombo vya Serikali kuu vyenye mahusiano ya karibu na serikali za mitaa ni, waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa, mkuu wa mkoa, sekretarieti ya mkoa, mkuu wa wilaya na ofisa tarafa.

Ili kuleta ufanisi na kuepusha migongano, majukumu ya viongozi na vyombo vya Serikali kuu vyenye mahusiano ya karibu na serikali za mitaa yamewekwa bayana.

Majukumu ya waziri

Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa amepewa majukumu kadhaa kuhusu serikali za mitaa.

Majukumu ya waziri huyo, yakifahamika pande zote mbili na kufuatwa kama yalivyoainishwa, hakuna mgongano unaoweza kutokea na matokeo yake ni ufanisi mkubwa wa serikali za mitaa na maendeleo ya haraka nchini. Serikali za mitaa ni chombo muhimu katika maendeleo kwa vile serikali hizi zinakwenda chini kwa wananchi na kushughulikia yale yote yanayogusa maisha ya kila siku ya mwananchi.

Katika mfumo huu majukumu ya mkuu wa mkoa kuhusu serikali za mitaa yapo kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya 1997.

Na kama tulivyoona pale mwanzoni ni kwamba moja ya majukumu ya Serikali kuu ni kuweka sera. Na ni Jukumu la serikali za mitaa kutekeleza sera za Serikali kuu kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kwa mujibu wa sera na sheria za nchi. Wajibu huu upo kisheria na wala si kutaka kwa mtu au kiongozi yoyote yule kwa juhudi au mipango yake mwenyewe.

Kwa mujibu wa vifungu Namba 54(1)(c) cha Sheria Na.8 ya mwaka 1982 na Kifungu Namba.111(1) ( c) cha Sheria Namba 7 ya mwaka 1982, moja ya wajibu na majukumu ya mamlaka za serikali za mitaa ni kupanga mipango ya maendeleo kwa mujibu wa sera na sheria za nchi.

Tunapojitahidi kulijenga taifa ili kuleta maendeleo kwa kila Mtanzania, mahusiano ni muhimu sana. Maana majukumu na mipaka ya kila mmoja yanapojulikana, nafasi za kuingiliana na kuleta misuguano hupungua au kutoweka kabisa. Matokeo yake ushirikiano huongezeka na mafanikio ya kazi za halmashauri huwa makubwa.

Jambo la muhimu hapa ni kwa kila mwananchi kutambua kwamba waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa, ndiye anayewajibika kisiasa katika Bunge kuhusu maendeleo na ufanisi wa serikali za mitaa. Hivyo ni wajibu wa waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa, kuziongoza, kuzisaidia na kuziwezesha halmashauri ili zitekeleze majukumu yao kwa mujibu wa Katiba, sera na sheria za nchi. Haya yakieleweka vizuri, hakuna tena msukumo wa madiwani kuhama kwa kisingizio cha kuunga mkono. Wafuate Katiba na sheria za nchi. Hivi ni vitu muhimu zaidi kwenye uhai wa taifa letu zaidi ya vyama vya siasa.

Padri Privatus Karugendo +255 754633122