Uhusiano wa viwanda, zao moja wilaya moja

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (wa tatu kushoto) akiwa kwenye moja ya maabara ya kiwanda cha kutengeneza dawa ya kuua viluilui vya mbu waenezao malaria alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Picha ya Maktaba

Moja ya sera kubwa ya Serikali ya Rais John Magufuli ni kujenga viwanda, viwanda vikubwa na vidogo. Mara nyingi, nimewahi kuandika sana kuishauri Serikali na wadau wa viwanda kuzingatia mambo makuu yanayoweza kutupatia viwanda vya uhakika, vikubwa na vidogo.

Nikiri kuwa huko nyuma nimewahi kuandika sana kuhusu umuhimu wa kuwekeza fedha nyingi kwenye kilimo ili viwanda viwe na tija kwa kuwa na uhakika wa malighafi za kuzalishia au kuongezwa thamani kupitia viwanda hivyo. Nikiri pia kwamba, mara zote nimekiandika kilimo kwa ujumla sana, sikugusa maeneo mbalimbali maalumu yanayokihusu kilimo.

Leo nawajibika kuzungumza juu ya umuhimu wa wilaya moja zao moja ambayo imetumiwa na kuleta matunda katika nchi nyingi duniani, nchi ambazo zilifanikiwa kwenye mapinduzi ya viwanda, jambo ambalo pia ni ndoto ya Serikali ya awamu ya tano.

Natambua kuwa dhana hii ya zao moja wilaya moja imeshaanza kufanya kazi hapa Tanzania, makala haya yanakwenda kuhuisha kazi iliyokwisha kuanza kufanywa kwa lengo la kuifanya iwe bora na yenye tija.

Maana ya zao moja wilaya moja

Ni swali lenye jibu rahisi sana. Huu ni mchakato wa kimaamuzi ambapo watunga sera na mamlaka juu ya kilimo zinazielekeza wilaya zote Tanzania juu ya mazao mkakati wa wilaya husika. Mazao mkakati hayo ni mengi kulingana na asili ya eneo, udongo uliopo, rutuba yake, hali ya hewa na sifa nyingine nyingi. Yote haya huhitimishwa kutokana na utafiti wa kitaalamu wa kila eneo la wilaya, lakini utafiti huo haujahusishwa na historia ya eneo husika na ushahidi wa mazao ambayo yamekuwa yakilimwa na kustawi sana kwenye eneo la wilaya hiyo.

Michakato yote hii ndiyo huhitimisha na kufanya kuwe na dhana ya wilaya gani inahitaji zao gani. Hata mchakato huu unapokamilika, wilaya husika haifungwi kutokulima mazao mengine, inaweza kuendelea kulima lakini inawajibika kulima zao mkakati kwa kiwango na makisio yaliyowekwa.

Kwa mfano, kama wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani imepangiwa zao mkakati lake kuwa ni muhogo, inapangiwa pia na kiasi cha tani za muhogo unaopaswa kuzalishwa kila mwaka kulingana na hali ya hewa ya Mkuranga kwa mwaka husika.

Hiyo ina maana kuwa, wilaya hiyo inao uwezo wa kulima pamba kwa mfano kiwango chochote kile, lakini bila kuathiri uzalishaji wa muhogo, ubora na wingi uliopangwa.

Lengo la zao moja wilaya moja ni kukimbiza gurudumu la maendeleo kwa mtindo wa kutumia vizuri rasilimali na maliasili za kila wilaya ya Tanzania ili kuzifanya wilaya husika ziwe na mchango wa kipekee katika uchumi wa nchi.

Mipango imara

Mipango imara sana inahitajika na juhudi kubwa zinapaswa kutendwa na watendaji wa Serikali nchi nzima. Kazi ya kuifanya kila wilaya iwe na zao mkakati bila kuingilia mazao mbadala siyo ndogo, inahitaji weledi, kujitoa, ubunifu, uwekezaji wa nguvu kazi na fedha na utashi wa uongozi katika kila wilaya na mkoa wa Tanzania.

Hili ni jambo ambalo pia linahitaji mipango ya muda mrefu na usimamizi wa uhakika unaombatana na kupeleka wataalamu wengi zaidi au kuwafundisha waliopo mbinu mpya za kilimo cha kisasa na kufungua mashamba darasa mengi katika kila wilaya ili maarifa na ujuzi wa kusimamia mazao mkakati viweze kupenyezwa haraka hadi kwa mkulima aliyeko mahali pasikofikika kirahisi.

Kwa sababu nchi yetu inao uzoefu wa kusimamia masuala kama haya, na sote tunajua kikwazo huwa ni kwenye eneo la usimamizi ngazi ya chini, iko haja mkazo ukawekwa kwenye eneo la utekelezaji na usimamizi, na mambo haya yafanywe kwa uhakika kwa mnyororo imara wa Serikali, wizara, mikoa, wilaya, kata na vijiji.

Tukikosa mipango na mnyororo imara kuanzia juu hadi chini, mkakati wa zao moja wilaya moja hautatupa mafanikio tunayoyataka na utatukwamisha kwenye eneo la kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo kwenye maeneo au wilaya husika.

Ni muhimu watendaji wa Serikali katika ngazi zote, wakachota mwelekeo wa Rais Magufuli katika usimamizi wa mambo, ngazi za chini za utekelezaji kukawa na uthabiti wa utekelezaji na morali ukakuzwa ili kuwa na matokeo ya uhakika. Kama zao moja wilaya moja litakosa msukumo na uthabiti huu wa kutoka kwa mkuu wa nchi hadi chini, eneo hili muhimu la ujenzi wa uchumi wa viwanda litakwama.

Zao mkakati, ajira na uchumi

Kama nchi yetu ikifanikiwa kusimamia na kuhitimisha mkakati wa aina hii kwa uzito wa kipekee, na kila wilaya ya Tanzania ikaweza kuzalisha walau asilimia 50 tu ya zao mkakati lililopangwa, tunao uwezo wa kutatua mambo makubwa mawili kwa asilimia 20 hadi 30 kwa uchache, mambo hayo ni ajira na uchumi wa majumbani na maeneo ya vijijini.

Nchi zilizofanikiwa sana kwenye mazao mkakati zina sifa moja ya msingi, sifa yenyewe ni kubadilika moja kwa moja kwa hali ya ajira na uchumi kwa watu wanaoishi kwenye maeneo yanayolima zao husika. Mambo haya mawili yanaweza kutowahusu moja kwa moja watu ambao hawajihusishi na zao mkakati kwenye eneo husika, lakini yanaweza kuwagusa kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Vijana na kina mama ambao watashiriki moja kwa moja katika mazao mkakati watakuwa na uwezo mkubwa wa kujiajiri na kuanza kubadilisha uwezo wao wa kimapato na ule wa kiuchumi, haya siyo mambo rahisi hata kidogo, lakini yanawezekana ikiwa kweli yale tuyasemayo yanaweza kutendwa vilivyo na watendaji au wasimamizi wa mazao hayo.

Kanuni ya kukuza uchumi wa nchi kutokea kijijini ni ya muhimu zaidi, kwa Tanzania yetu, vijiji ndivyo vinachukua sehemu kubwa ya nchi na wananchi wengi wako huko, japokuwa kumekuwa na uhamaji mkubwa kutoka vijijini kwenda mjini, lakini vijiji vinabaki kuwa alama ya uhai na uzima wa taifa letu.

Zao moja wilaya moja vikisimamiwa vizuri vinaweza kabisa kuondoa matatizo makubwa ya uchumi na ajira vijijini.

Zao mkakati na viwanda

Dhana hizi mbili zinategemeana na ni mchezo wa yai na kuku. Dhana yoyote ile kati ya hizi mbili inaweza kuwa na nguvu au kudai yenyewe ndiyo italeta tija kwa mwenzake, lakini kwa sababu dhana haziwezi kugombana ni rahisi kusema kwamba chochote kinaweza kuanza, kiwanda au zao mkakati.

Kwa maoni yangu katika eneo hili ni vema tuanze na vyote viwili, au kwa uzito tuanze na zao mkakati lakini tukiwa na uhakika wa wapi kilipo kiwanda. Siyo lazima kuwa na kiwanda cha zao mkakati katika kila wilaya, tunaweza kuongeza thamani ya zao mkakati la muhogo linalozalishwa Mkuranga, Pwani; Handeni, Tanga; Kondoa, Dodoma au Nzega, Tabora – kwa kuweka kiwanda mkakati kimoja Dodoma walau kwa kuanza.

Kumbe basi, dhana ya ujenzi wa viwanda kwa kuihusisha na zao mkakati inaweza kutohitaji viwanda vingi kwa wakati mmoja. Tunaweza kuwa na viwanda vichache na vikatusaidia kufika mbali, jambo hili haliwezekani kirahisi kama hatutakuwa na shabaha ya kufanya hivyo. Shabaha inahitajika kuanza mara moja ili tusichelewe.

Nchi yetu imejaliwa uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya chakula na biashara, mahitaji ya ndani na nje ya chakula ni makubwa. Kinachopaswa kuwekwa nguvu ni uthubutu. Mimi ambaye nimekulia kijiji cha Kiabakari, Mara, nakumbuka kuwa kwa mfano Gereza la Kilimo la Kiabakari, enzi hizo lilikuwa na uwezo wa kuzalisha maelfu ya tani za mahindi na maharage, gereza moja lilifanya uzalishaji mkubwa mno.

Kama wananchi wakihamasishwa na mkazo ukawekwa na kukawa na uhakika wa wapi mazao mkakati yatapelekwa kwa uhakika kuwa wakulima watapata fedha za kuendelea kuzalisha msimu unaofuatia, jambo hilo linawezekana.

Kama gereza moja linaweza kustaajabisha wilaya nzima kwa kuzalisha pomoni, vipi wananchi kwa maelfu wakiwekewa mikakati ya kutosha ya uzalishaji na wakasaidiwa pamoja na mazao yao mengine kila mmoja azalishe zao mkakati kitaalamu? Hakika tutafika mbali.

Makala haya yatukumbushe kuwa, kazi ya ujenzi wa viwanda inachochewa zaidi na kilimo, wimbo huu sote tunaujua na tumekuwa tukiuimba, ni wakati wa kuutekeleza kwa vitendo na kuuwekea fedha na mipango ya kutosha.

Zao moja wilaya moja ni jambo linalowezekana, tuifanye mipango yetu kuwa vitendo.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mfasiri na mkalimani. Simu; +255787536759: Barua Pepe; [email protected])