Sunday, July 8, 2018

Ulaya inawakataa wahamiaji haramu inaowatengeneza

 

By Idd Amiri

Hali ya hewa barani Ulaya kwa sasa ni joto na bahari ya Mediterranean imetulia, haina mawimbi yenye rabsha yanayosababisha wahamiaji wanaotumia bahari hiyo kuvuka kwenda Ulaya kupata matatizo wawapo safarini.

Ni kweli kuwa Waafrika na Waarabu hasa wale wanaojaribu kuhatarisha maisha yao kwa kutumia vyombo vya baharini, wanaitumia hali hii kwenda kutafuta maisha bora barani Ulaya.

Hali ya hewa ya joto kuanzia kusini mwa Italia hadi Kaskazini huko Iceland inawavuta wahamiaji na ni wazi kuwa kwa mtu anayetoka Arabuni au Afrika huu ni muda mwafaka kujisogeza Ulaya, kwani ile hali ya baridi kali imetoweka kwa muda.

Hali itakuwa hivi hadi Oktoba ambapo kivumbi cha baridi kali kitarejea na kuichafua bahari hii ambayo imegeuzwa na wahamiaji kuwa ni njia ya kuingilia Ulaya.

Vyombo vya habari vya Ulaya hasa vile vyenye mlengo wa kulia visivyopendelea wageni, kama kawaida vimeendelea kutoa habari za kutisha kwa watu wa bara hilo kama vile wakimbizi wanaoingia huko ni kundi la wauaji hatari ambao wanatakiwa kudhibitiwa kwa nguvu zote.

Vyama visivyopenda wageni

Nchi za Austria, Italia, Hungary na Poland zinatawaliwa na vyama visivyopendelea wageni na hivyo imekuwa ni mtihani mkubwa hata kwa jumuiya ya Ulaya ambayo iliweka idadi fulani ya wakimbizi kuingia katika nchi za umoja huo kulingana na hali ya uchumi wa nchi husika.

Wahamiaji wengi na siyo wakimbizi kama wanavyojulikana Ulaya wanapitia Libya ambako ni karibu na bandari zilizoko Kusini mwa Ulaya kama Malta, Italia na Ugiriki.

Kuwapo kwa sintofahamu hii kumesababisha nchi zilizoko pembezoni mwa bahari ya Mediteranean kama Italia, Ugiriki, na Malta kukataa kuruhusu meli zinazobeba wahamiaji kufunga gati katika bandari zao.

Ulaya kwa ujumla wake na hasa kwa anayeijua, inahitaji watu zaidi kwa sababu maendeleo ya kiuchumi na viwanda yanahitaji wafanyakazi na hasa katika nyanja za kuhudumia jamii ambapo kwa asili watu wa bara hilo hawapendelei sana kazi hizo, wao wenyewe hawazaliani sana kwa hiyo hivi sasa kuna baadhi ya maeneo katika nchi hizo hayana kabisa vijana mfano mzuri ni vijiji vya nchi ya Italia.

Licha ya ukweli huo, lakini wanasiasa na vikundi vya watu wachache wabaguzi wanaoibuka siku hizi barani humo hasa baada ya kukosekana kwa itikadi za kutambulisha vyama vya kisiasa wameona hiyo ndiyo turufu yao ya kushindia masuala yao ya kisiasa na kusahau kabisa mambo mengine kama ya usalama.

Hofu kubwa waliyo nayo wanasiasa wa Ulaya na wafuasi wao ni namna ya kuwahudumia wakimbizi kwa sababu kwa taratibu zao kila mkimbizi ni lazima apatiwe nyumba ya kuishi na alipiwe gharama za huduma zote muhimu kama afya, maji, umeme na shule kwa watoto, lakini hilo haliwezi kuwa tatizo kwa sababu zipo nchi kama Ujerumani ambayo imeamua kuwaweka wakimbizi katika hosteli ambazo bado ni nafuu kwa watu wenye shida ya maisha.

Hoja ya ubinafsi

Mambo mengine yanayochangia kuzuia wahamiaji hao ni pamoja na ubaguzi wa kidini au rangi, uchoyo wa kawaida wa binadamu wa kutopenda kushirikiana kula kile kilichopo na kumezwa kwa utamaduni wao ingawa sababu zote hizo hazina mashiko katika dunia ambayo imekuwa kama kijiji.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), linakadiria kuwa dunia ina wakimbizi wapatao milioni 65.8 walioko maeneo mbalimbali, wakiwa ni wa ndani ya nchi au waliozikimbia nchi zao. Wengi wa hawa hawapo Ulaya, kwa mfano wakimbizi wa Syria wengi wako Uturuki, Iran na Lebanon, hapa kwetu Afrika wale wa Burundi wengi wapo Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wale wa Sudan Kusini wengi wapo Ethiopia, Uganda na Kenya. Hii ni mifano michache ambayo inaweza kutoa picha namna ambavyo wazungu wanalia wakati msiba si wao.

Wakimbizi ni matokeo ya vita, uchumi mbovu, ukatili wa watawala, unyanyasaji wa kijinsia na kwa siku za karibuni mabadiliko ya hali ya hewa ambapo hali ya ukame imewafanya maelfu kwa maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kwenda kutafuta mahari salama pa kupata chakula.

Ukiangalia kwa jicho la ndani sehemu kubwa ya wakimbizi duniani wanatokana na matendo ya nchi hizo za Ulaya Magharibi hasa pale linapokuja suala la vita.

Kwa bahati mbaya sana raia nchi hizo hawataki kujua ni matatizo gani wanayopata wale wanaopokea wakimbizi katika nchi kama Uturuki, Tanzania, Kenya, Uganda na nyingine nyingi ambazo zimeruhusu wakimbizi kuishi huko.

Raia wa Ulaya ambao hawataki kuwaona wageni wakiingia kwao wamekuwa hawafanyi chochote hasa pale watawala wa huko wanapofanya muungano wa kupeleka majeshi kwenda kupigana katika nchi za nje kwa kisingizio cha kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.

Enzi za Blair, Bush

Wakati wa utawala wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair wa Uingereza aliungana na George W. Bush wa Marekani mwaka 2003 kupeleka majeshi, vifaru na ndege za kivita kwenda kuung’oa utawala wa Saddam Husein huko Iraq kwa kisingizio cha kuwa alikuwa akimiliki silaha kali za kemikali kitu ambacho baadaye kilionekana kuwa ulikuwa ni uwongo, lakini maelfu kwa maelfu ya raia wa nchi hiyo walikufa na wengine mpaka leo ni wakimbizi katika nchi mbalimbali za ghuba na wachache sana walifanikiwa kupata hadhi za ukimbizi huko Ulaya.

Miaka miwili kabla ya kuivamia Irak, umoja huo uliivamia kwa mabomu na vifaru nchi ya Afghanistan kwa nia ya kumtafuta Ossama Bin Laden ambaye walimtuhumu kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi katika majengo pacha jijini New York mwaka 2001 ambapo watu karibu 3,000 walikufa, mapigano hayo yalisababisha pia maelfu kwa maelfu kuihama nchi hiyo na kwenda nchi jirani za Pakistan na India na mpaka leo hali haijawa shwari ikionyesha kuwa bado watu wa nchi hiyo wanajitosa katika kutumia njia za hatari ili kujaribu kama watafanikiwa wafike Ulaya ambako hali ya usalama ni nzuri na pia miasha si mabaya.

Mifano iko mingi, mataifa hayo yaliungana ili kuuondoa utawala wa Muammar Ghaddaf, aliyekuwa Kiongozi wa Libya na hivyo kusababisha hali ya sintofahamu hadi leo hii nchi hiyo haijatulia ikimaanisha kuwa watu bado wanakimbia vita ili kusalimisha maisha yao popote pale palipo na usalama.

Nchi za Syria na Yemen nako hali si shwari na huko kote kuna mkono wa mataifa hayo yanayozuia wakimbizi kuingia kwao. Huku Afrika kuna mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini ambako nako mataifa haya hayawezi kukwepa kuonyeshewa kidole cha lawama.

Uchumi kwa Afrika

Kwa upande wa kiuchumi ambako kwa sehemu kubwa nako ni matokeo ya watu kuzihama nchi zao huwezi kuacha kuzilaumu nchi zilizoendelea za bara la Ulaya, kwa mfano matokeo ya ukoloni yalizifanya nchi nyingi hasa Afrika kuwa tegemezi. Afrika ilikuwa sehemu ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya Ulaya na hivyo kutoa bei ndogo sana ya mazao ya kibiashara kama kahawa, kakao, chai na korosho.

Mfumo huu umefanya nchi za kiafrika zinaponunua bidhaa za viwandani, mitambo ya kilimo na hata dawa kuwa gharama kiasi ambacho kinarudisha nyumba maendeleo na ustawi wa watu wake.

Ipo mifano ya wazi kabisa kuwa mfumo huu unawapa wazungu urahisi wa gharama za maisha kuliko hata Waafrika wenyewe, kwa mfano unaweza kunywa kikombe cha kahawa kwa bei ndogo sana jijini London kuliko huko Ethiopia inakozalishwa na vilevile ukala keki ya kakao kwa bei rahisi London kuliko Ghana zinakolimwa.

Zao la chai ambalo linapatikana hapa kwetu ni nadra sana kuwakuta watu wakinywa chai ya daraja la kwanza kwa sababu ya bei na ukiritimba lakini chai hiyo ipo jijini London, Uingereza inapatikana kwa bei nafuu kabisa.

Mfumo huu wa uchumi usio wa haki ambao kwa sasa umeimarishwa kwa kuwekwa masharti magumu sana ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Afrika na Ulaya umewafanya watu wengi kushindwa kupata fursa za kuendesha maisha yao na hivyo kuona njia pekee ni kukimbilia huko Ulaya ambako kuna unafuu wa maisha.

Hivyo basi kwa kuwa Ulaya ndiyo mshiriki mkuu wa visababishi vya kuibuka kwa wimbi la wakimbizi au wahamiaji huko Ulaya, haina ujanja wala sababu za kuwakataa, ni wajibu wa wakazi wa bara hilo kutafuta suluhu wakishirikiana na mataifa ambayo watu hao wanatoka.

Mwandishi aliwahi kuishi nchini Uingereza na Ethiopia.

Iddamiri2018@yahoo.com, 0783 165 487

-->