Usiyoyafahamu kuhusu shambulio la Osama bin Laden Septemba 11

Muktasari:

  • Jumanne iliyopita Septemba 11, mwaka huu Marekani iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 ya shambulizi ambalo kundi la kigaidi la Al-Qaida chini ya kiongozi wake Osama bin Laden lilikiri kulifanya.

Kila ifikapo Septemba 11 ya kila mwaka Marekani hukumbuka shambulizi baya la kigaidi kuwahi kutokea la kulipuliwa kwa majengo pacha ya Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) mjini New York mwaka 2001.

Jumanne iliyopita Septemba 11, mwaka huu Marekani iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 ya shambulizi ambalo kundi la kigaidi la Al-Qaida chini ya kiongozi wake Osama bin Laden lilikiri kulifanya.

Idara ya Polisi ya New York imelichukulia tukio hili kwa uzito mara mbili ya ule wa taifa zima kwa kuwa yenyewe pia ilipoteza maofisa wake wanaokadiriwa kufikia 23 katika shambulizi hilo. Kwa sababu hiyo, idara zote za polisi kutoka maeneo yote ya Marekani na Canada waliungana kufanya matembezi karibuni na eneo la Manhattan ambapo shambulizi hilo lilitokea.

Tukio hili lilichukua uhai wa raia zaidi ya 2,977 mjini New York, makao makuu ya jeshi la Marekani maarufu kama Pentagon na eneo la wazi mjini Pennsylvania. Shambulizi hili na madhara yake limeibadili sera ya Marekani kuhusu ulinzi kwa miaka 17 sasa na kulifanya taifa hilo kuwa makini zaidi juu ya ugaidi.

Hata hivyo, bado imekuwa vigumu kuwasahaulisha wananchi wa Marekani tukio hilo baya. Yapo mambo ambayo kama si umeyasahau basi huyafahamu kuhusu Septemba 11. Haya ni baadhi ya mambo hayo.

Haijulikani namna watekaji wa ndege walivyoingia katika vyumba vya marubani. Baada ya shambulizi hili iliundwa kamati ambayo ilikuja na ripoti iliyochapishwa mwaka 2004, ripoti hiyo ilieleza kwamba hakuna hata mmoja anayefahamu ni kwa namna gani watekaji waliingia kwenye ndege mpaka kwenye vyumba vya marubani wa ndege nne ambazo zilitumika katika shambulizi hilo.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa “huenda mmoja wa marubani au ofisa wa ndege alibanwa na kutoa ufunguo wa ndege au alilazimishwa kufungua mlango katika ndege ya abiria iliyoitwa American Airlines 11.”

Baada ya watekaji kuingia katika chumba cha rubani waliielekeza katika majengo-pacha ya makao makuu ya WTO, New York na kuligonga lile la upande wa kaskazini saa 8:46 asubuhi. Abiria wote 81, watekaji watano na wahudumu tisa na marubani wawili waliokuwemo katika ndege hiyo iliyokuwa inatoka Boston kwenda Los Angeles walifariki dunia pamoja na watu waliokuwepo katika jengo hilo ambao idadi yao haikufahamika.

Inaendelea uk 24

Inatoka uk 23

Abiria waliwataarifu jamaa na familia zao kuhusu kutekwa kwao, inadaiwa kwamba abiria wote waliokuwamo katika ndege zote nne zilizotekwa, yaani American Airlines 11, United Airlines 175, American Airlines 77 na United Airlines 93 walizipiga simu ama simu zao au nyingine zilizokuwapo katika ndege kuwataarifu juu ya uwepo wa watekaji hao.

Hata hivyo, walishindwa kuwa na msaada kwani waligundua kwamba mfumo wa taarifa ulikwisha kuzimwa.

Ndege iliyoitwa American Airlines 77 iliondoka katika uwanja wa Dulles mjini Washington ilitekwa karibu na Indianapolis kisha ikarudishwa Washington na kuangushwa Pentagon. Mke wa mwanasheria wa Serikali, Jenerali Ted Olson, Barbara Olson alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwepo katika ndege hiyo, alimpigia simu mumewe kumweleza kuwa wametekwa. Hata hivyo, American 77 ilianguka Pentagon saa 9:37 asubuhi na kuua watu 69 waliokuwemo ndani ya ndege.

Mawasiliano yaliyopatikana katika visanduku vya mawasiliano yaliunganishwa baadaye na kugundua namna ambavyo ndege ilitekwa.

Idadi ndogo ya abiria waliokuwamo ilirahisisha watekaji wasigundulike, ripoti zinaeleza kuwa maofisa waliochunguza kisa hicho wanasema kuwa idadi ndogo ya abiria kuliko ile iliyotakiwa kubebwa na ndege hizo ilichangia watekaji kupenya kirahisi na kupata nafasi ndani ya ndege bila kugundulika. Kwa mfano, American 11 iliyoondoka Boston kwenda Los Angeles ilikuwa na abiria 81 kati ya 158 iliyotakiwa kubeba.

Pia, United 175 iliyoondoka Boston kwenda Los Angeles ilikuwa na abiria 56 pekee kati ya 168, hiyo ni sawa na asilimia 33 ambayo ni chini ya asilimia 49 ya uzito iliyotakiwa kubeba. American 77 ilikuwa inaelekea Los Angeles kutoka Washington ilikuwa na abiria 58 kati ya abiria 176 iliyotakiwa kubeba.

United 93 iliyotoka New York kwenda San Francisco ilikuwa na abiria 37 ambao ni sawa na asilimia 20 ya uwezo wake ikiwa ni chini ya asilimia 52 ya uzito iliyotakiwa kubeba. Idadi hii inadaiwa kuwapa watekaji nafasi ya kuketi bila kugundulika kwa kuwa kama ndege zingekuwa na abiria wote basi wangeonekana kwani wangekosa mahala pa kuketi.

Kupungua idadi ya watekaji kulisababisha United 93 isilete madhara makubwa, inadaiwa kwamba watekelezaji wa shambulizi hili walipanga kwamba kila ndege iwe na watekaji watano, lakini Mohamed al Kahtani alizuiliwa na maofisa uhamiaji wa uwanja wa Florida Orlando baada ya kuhisiwa, ” inasema ripoti ya Septemba 11.

Ndege zote tatu zilikuwa na watekaji watano huku United 93 ikiwa na watekaji wanne pekee na kushindwa kuwadhibiti abiria na marubani. Kutokana na hilo, United 93 haikulenga kama ilivyokusudiwa.”

Kwa sababu hiyo baadhi ya abiria walijaribu kuelekea kwenye chumba cha marubani kumdhibiti, aliamua kuiangusha ndege katika eneo la wazi huko Shakville ikiwa ni dakika 20 tu baada ya ndege hiyo kupaa.

Makamu wa Rais, Cheney aliamuru United 93 itunguliwe. Kabla ya abiria kupambana na watekaji na ndege hiyo kuanguka, makamu wa Rais, Dick Cheney alitoa amri ya ndege hiyo kutunguliwa kabla haijafika Washington, inaeleza ripoti ya Septemba 11. Hata hivyo, ripoti inaongeza kuwa waliopewa kazi ya kuitungua walikuwa na uwezekano mdogo wa kufanya hivyo kwa muda muafaka. Mamlaka za jeshi zilisema kuwa kama si abiria kusababisha United 93 kuanguka, wangehakikisha haifiki Washington, jambo ambalo baadaye walikiri kuwa haukuwa uamuzi sahihi.

Baada ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania kulipuliwa Agosti 7, 1998, Rais Bill Clinton aliamuru jeshi la Marekani kumuua Osama kabla ya Septemba 11 ambapo shirika la kijasusi la CIA pamoja na mashirika mengine yaliandaa mipango kadhaa ya kumkamata Osama mwaka 1998, ilisema ripoti hiyo.

Hata hivyo, mipango hiyo ilikufa na kufufuka mara kadhaa kwa kuwa walitegemea zaidi msaada kutoka kwa viongozi wa jadi wa Afghanistan.

Mshauri wa masuala ya ulinzi wa Marekani, Sandy Berger alijaribu kuibua mjadala kwamba ingekuaje kama ungekosekana ushahidi wa kumtia hatiani Osama katika mahakama ya Marekani kabla ya kufanyika kwa mashambulizi ya makombora dhidi ya Osama katika makazi yake huko Afghanistan na kuuawa mwaka 2011.

CIA walimuonya Rais Clinton mara kadhaa kuhusu utwekaji wa ndege tangu mwaka 1998. Desemba 4, mwaka 1998 ilitolewa taarifa kwa Rais kuwa Osama ameandaa mpango wa kuteka nyara ndege za Marekani na mashambulizi ili kushinikiza kuachiwa kwa Yousef na magaidi wengine. Inaeleza ripoti ya Septemba 11.

Shambulizi lilihusishwa na Saudi Arabia, ripoti ya Septemba ilieleza kuna baadhi ya kurasa zaidi ya 28 ambazo hazijawekwa wazi zinafichua kwamba kulikuwa na viashiria uhusika au kuwapo mkono wa Saudi Arabia katika shambulizi hilo. Kurasa hizo zinaonyesha kwamba kulikuwa na ufadhili kutoka kwa mwana wa mfalme wa Saudia, Bandar aliyekuwa balozi nchini Marekani. Taarifa kutoka gazeti la USA Today zilieleza kuwa “Kuna uwezekano wa ufadhili wa kifedha kutoka kwa familia ya kifalme ya Saudia kwa raia wake wanaoishi Marekani wakiwemo watekaji wawili miongoni mwa waliohusika huko San Diego. Taarifa pia zinaonyesha kuwa kulikuwa na ufadhili kwa misikiti ya Waislamu wenye msimamo mkali mjini California.” Hata hivyo kurasa hizo hazijawekwa wazi kwa sababu haikuthibitishwa kuwa taarifa hizo zinahusika moja kwa moja na shambulizi la Septemba 11. Taarifa zinaeleza kuwa watekaji 19 waliohusika na shambulizi hilo walitoka Saudi Arabia.

Kulikuwa na mipango mingine hapo awali ya kushambulia ndege za abiria. Ripoti ya Septemba 11 inaeleza kwamba kulikuwa na misururu ya mipango ya mashambulizi dhidi ya ndege za abiria za Marekani kabla ya Septemba 11, 2001. Mtuhumiwa namba moja wa mipango hiyo, Ramzi Yousef anatajwa kupanga ulipuaji wa makao makuu ya WTO mwaka 1993 na mashambulizi ya ndege 12 za Marekani ukanda wa Pacific mwaka 1995. Yousef alifanya kazi hiyo na mjomba wake aliyeitwa Khalid Sheikh Mohammed ambaye naye alihusika kwa kiasi kikubwa katika shambulizi la Septemba 11. Yousef alikamatwa Februari 7, 1995 huko Islamabad, Pakistan. Alipanga shambulizi lingine Manila, Ufilipino ambalo halikufanikiwa.

Shambulizi la Septemba 11 dhidi ya majengo ya WTO, Mjini New York halikuwa la kwanza. Itakumbukwa mchana wa tarehe Februari 26, mwaka 1993 bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari dogo lilipuka katika maegesho ya magari ya ardhini katika moja ya majengo hayo. Ripoti ya Septemba 11 inaeleza kuwa watu sita waliuawa katika mlipuko huo na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa. Ripoti zinasema kwamba Ramzi Yousef ambaye ni muumini wa dhehebu la Sunni ndiye aliyepanga shambulizi hili la kigaidi na alilenga kuua watu 250,000.

Ni miaka takribani 15 imepita tangu kutokea kwa shambulizi la New York. Tukio hili lilifufua upya vita vikali dhidi ya ugaidi ambapo kila nchi duniani kwa sasa inapambana kuhakikisha hakuna kitisho dhidi ya ugaidi.

Baraza la Umoja wa Mataifa linapambana na makundi haya ambayo yanazidi kukua kila siku. Makundi kama Islamic State, Boko Haram, Al-Shabaab na mengine ni miongoni mwa makundi yanayosumbua usalama wa raia katika nchi mbalimbali. Ni wajibu wa kila nchi kuimarisha idara zake za usalama kuhakikisha ya Septemba 11 au zaidi hayajirudii.

Imetafsiriwa na kuandikwa na mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anafanya mazoezi kwa vitendo Mwananchi Communications Ltd.0672395558.