Utafiti kuhusu utendaji wa Rais jambo lisiloepukika

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole (kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji walipohudhuria shughuli ya kutolewa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza, jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Ripoti hiyo ya Twaweza iliibua mjadala mkubwa na bado haujazimika. Mwaka juzi (2006) Twaweza walieleza kukubalika kwa Rais Magufuli kulikuwa asilimia 96, mwaka jana ilikuwa asilimia 71. Twaweza walionyesha pia namna Rais wa Nne, Jakaya Kikwete na mtangulizi wake, Benjamin Mkapa walivyokuwa wanakubalika.

Taasisi ya Twaweza ambayo hushughulika na utafiti wa kijamii na kisiasa, hivi karibuni ilitoa ripoti kuhusu maoni ya wananchi juu ya uongozi wa kisiasa nchini. Ripoti hiyo pamoja na kueleza nafasi ya vyama vya siasa, ilionyesha kwamba utendaji wa Rais John Magufuli unakubalika kwa asilimia 55.

Ripoti hiyo ya Twaweza iliibua mjadala mkubwa na bado haujazimika. Mwaka juzi (2006) Twaweza walieleza kukubalika kwa Rais Magufuli kulikuwa asilimia 96, mwaka jana ilikuwa asilimia 71. Twaweza walionyesha pia namna Rais wa Nne, Jakaya Kikwete na mtangulizi wake, Benjamin Mkapa walivyokuwa wanakubalika.

Pamoja na yote yaliyotokea, ushauri ni kwamba Rais Magufuli mwenyewe anaweza kuajiri taasisi huru ya kimataifa ikafanya utafiti ili kuona ni kwa namna gani Watanzania wanautafsiri uongozi wake hasa kipindi hiki anapotimiza nusu ya muhula wake madarakani.

Kwa kuwa uongozi ni sayansi, majibu ambayo Rais atayapokea bila shaka yatamsaidia kutambua tafsiri ya Watanzania juu ya uongozi wake katika nusu ya kwanza ya muhula wake wa kwanza, kisha ataamua njia za kupita kiuongozi katika nusu iliyobaki kuelekea Oktoba 2020.

Kwa msisitizo; uongozi ni sayansi na muhula mmoja ukikamilika Rais Magufuli atatakiwa kurejea kwa wananchi kuzungumza nao ili kuomba ridhaa kwa ajili ya kuongezewa muhula wa pili. Hivyo ni vizuri kutambua hisia na mapokeo ya wapigakura wake.

Utafiti wa taasisi huru ya kimataifa iliyo nje ya nchi, bila shaka hautakuwa na mwangwi wa kisiasa wala kubeba hisia za kutumiwa na wanasiasa. Zaidi unaweza kuwa na majibu ukweli ulio mweupe au mweusi. Na katika hii nusu muhula ya kwanza aliyowaongoza Watanzania, Rais Magufuli anahitaji ukweli usiopinda.

Hapa niweke wazi kwamba utafiti ambao Rais Magufuli anaweza kuufanya kwa kutumia taasisi huru ya kimataifa, lengo lake si kushindana na ripoti ya Twaweza au kuhakiki majibu ambayo waliyatoa kuhusu kukubalika kwa Rais, bali kufanya tathmini ya mapokeo ya wananchi juu ya uongozi wake kwa nusu muhula.

Tena si lazima matokeo yatolewe kwenye vyombo habari, bali umuhimu wake ni kuyatumia kama stadi mpya katika ngwe ya pili ya muhula wake wa miaka mitano. Maana kujua unaowaongoza wanavyokubaliana na uongozi au makundi hasi na chanya dhidi ya utawala wako, hiyo ni nyenzo muhimu katika kuyahudumia makundi yote.

Mfano kutoka Marekani

Februari mwaka huu, Chama cha wanazuoni wa Sayansi ya Siasa Marekani (American Political Science Association), kilitoa utafiti wake wenye kumlinganisha Rais Donald Trump na watangulizi wake 44. Majibu yaliyotoka yalionyesha kwamba kukubalika kwa Trump kulikuwa chini kuliko wote waliomtangulia.

Kwa mujibu wa ripoti ya wanazuoni hao wa Marekani, Trump amewaongoza marais wanne walioshika nafasi tano za mwisho ambao ni Andrew Johnson, Franklin Pierce, William Harrison na James Buchanan. Aliwashinda mpaka waliokithiri kwa uvunjifu wa haki za binadamu.

Johnson, Pierce na Buchanan walitia fora kwa uvunjifu wa haki za binadamu kwa ubaguzi na ukandamizaji wa mtu mweusi pamoja jamii asilia ya Marekani, yaani Wahindi Wekundu. Wakati Harrison yeye ni Rais aliyetawala mwezi mmoja tu kabla kufikwa na mauti. Akiwa Rais aliyekaa muda mfupi zaidi ofisini, Harrison alijijengea sifa ya ujivuni, kiburi na kujiona anajua kuliko yeyote.

Mshangao mkubwa zaidi ni pale Trump aliposhindwa mpaka na Rais wa 37, Richard Nixon, ambaye alilazimishwa kujiuzulu urais mwaka 1974, baada ya Bunge la Marekani, Congress, kupitisha hoja ya kuanza mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, kutokana na kubainika kuhusika na kashfa ya Watergate.

Kashfa ya Watergate inahusu uvamizi wa timu ya kampeni ya Nixon (Republican), kwenye ofisi za kampeni za Urais za Chama cha Democratic, zilizokuwemo kwenye jengo la Watergate, Washington DC. Uvamizi huo ulilenga kuiba siri za kampeni za Democrats ili Nixon na Republican wazitumie kushinda uchaguzi mwaka 1972.

Kitendo cha Nixon kutajwa kushika nafasi ya 33 wakati Trump ni wa mwisho, ndicho ambacho kiliwashangaza wengi, kwamba wanazuoni wa Sayansi ya Siasa, wanamwona mtu ambaye alinusurika kidogo kushtakiwa kwa uhalifu akiwa Rais wa nchi, amekuwa bora kiuongozi kuliko Trump.

Utafiti huo uliratibiwa kwa kupitia tathmini ya kiutendaji kuanzia Rais wa Kwanza, George Washington mpaka Trump. Wanazuoni takriban 2,000 walitoa tathmini na kuwalinganisha mmoja baada ya mwingine kabla ya kufikia majibu waliyotoa.

Katika majibu hayo, Rais wa 16, Abraham Lincoln ameendelea kutajwa namba moja, Washington wa pili, namba tatu Franklin Roosevelt, nne Theodore Roosevelt na tano amekuwa Thomas Jefferson. Katika ripoti hiyo, wanazuoni hao walimuweka Rais wa 44, Barack Obama nafasi ya 10.

Nini Trump alishauriwa

Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, hupenda kusema kwamba utafiti hupingwa kwa utafiti. Kwamba ripoti inayopatikana kwa utafiti, haipaswi kujibiwa kwa majibu ya mtaani, isipokuwa inabidi kufanya utafiti mwingine ili kuujibu ule wa awali.

Hicho ndicho Trump alishauriwa, kwamba anapaswa kuifanyia tathmini ya wanazuoni wa Marekani kwa kutafuta wanazuoni wa siasa na wanahistoria wabobezi kutoka nje ya Marekani ambao wanaijua zaidi historia ya Marekani ili wampe tathmini ya uongozi wake kulinganisha na marais wengine waliotangulia.

Ushauri uliotolewa ulijengwa na ukweli kwamba ndani ya Marekani kuna mgawanyiko mkubwa. Tabaka la wasomi halimkubali Trump, kwa kumwona ni mtu aliyeingia ofisini bila kuwa na uwezo wa kumudu kazi ya urais wa taifa hilo kubwa ulimwenguni. Hivyo, inaaminika kuwa si rahisi Trump apate alama nyingi za kuungwa mkono na wasomi.

Zaidi, Marekani yote kwa sasa, kila mwenye kufuatilia siasa na uongozi wa nchi unavyokwenda, ama anamuunga mkono Trump au kinyume chake. Katika hali hiyo inakuwa sababu ya kuamini kwamba utafiti au tathmini yoyote itakayofanywa na Wamarekani, itabeba hisia.

Kwa maana hiyo, wanaweza kutafiti Wamarekani na kutoa majibu ama kumkandamiza au kumtukuza kutokana na hisia. Ndiyo maana ushauri mkubwa zaidi umetolewa kuwaelekea watu wa nje ya Marekani, kwa kuamini kwamba watatoa majibu ya kweli pasipo kuchanganywa na hisia.

Ushauri kwa Trump umekwenda pia kwenye kukamilika kwa nusu muhula wa kipindi chake cha uongozi. Januari 20 mwakani, Trump atakuwa anatimiza miaka miwili ofisini tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Marekani. Hivyo, ameshauriwa kuajiri taasisi ya nje ya Marekani kutathmini mapokeo ya Wamarekani kwa uongozi wake.

Hicho ndicho nashauri kwa Rais Magufuli. Siyo kutaka kulinganisha urais wake dhidi ya watangulizi wake, bali kupata ukweli pasipo hisia za kisiasa juu ya namna ambavyo Watanzania wanauelewa uongozi wake. Je, aendelee hivyohivyo au yapo maeneo ya kufanyia mabadiliko? Majibu ya utafiti yatampa mwanga.

Ushauri kwa wabunge

Rais Magufuli anapotimiza nusu muhula, maana yake na wabunge nao tayari wameshatimiza nusu ya kipindi chao cha miaka mitano tangu walipochaguliwa Oktoba 25, 2015 kisha kuapishwa mwezi mmoja baadaye, yaani Novemba 2015. Hivyo, wabunge nao wanatakiwa kufanya tathmini.

Mbunge huwezi kuendelea kujiamini ni mwakilishi wa wapigakura kwenye jimbo lako wakati hujui hisia zao kwako tangu walipokuchagua. Inawezekana tayari ulishavunja matarajio yao, kwa hiyo unaendelea kuwa mbunge kwa sababu hawana kitu kingine cha kufanya ili kukuondoa.

Katika hali ya namna hiyo, maana yake endapo uchaguzi utafanyika leo hutachaguliwa. Mbunge akifanya utafiti, itamsaidia kuelewa nafasi yake kwa wapigakura wa jimbo lake kwenye nusu ya kwanza ya muhula wake, na atapata picha ni uelekeo gani wa kuufuata katika nusu iliyobaki.

Mbunge si lazima kufanya utafiti kwa kutumia taasisi ya kimataifa. Kwanza ni vigumu kumudu gharama. Hivyo, inawezekana kutumia taasisi za ndani au vijana wasomi ambao watamsaidia mbunge kujua nini ambacho wananchi wanakiwaza juu yake. Hiyo inaenda pamoja na kufahamu hisia za makundi na sababu zake.

Wabunge wanapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Ukichaguliwa leo, unasubiri mpaka miaka mitano ndipo unarudi kwenye uchaguzi pasipo kujua nafasi yako kwa hao wapigakura unaowaomba ridhaa nyingine ya kuwawakilisha. Hii imesababisha wabunge wengi kushindwa, licha ya kutumia nguvu kubwa kwenye uchaguzi.

Kama mbunge anakuwa amefanya utafiti mapema na kujua nafasi yake kwa wapigakura kuwa hakubaliki, hawezi kutumia nguvu kubwa yenye kuweza kumgharimu pia kiuchumi, wakati ameshatambua hali halisi. Ukishajua hukubaliki, utakaa pembeni mapema kuliko kungoja mshutuko wa kwenye sanduku la kupigia kura.

Orodha ya wabunge ambao walishindwa bila kutarajia na kuacha mshangao mkubwa ni wengi. Hata kwenye urais, aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh alishindwa na Adama Barrow kwa mshituko. Matarajio yalikuwa Jammeh angeshinda kwa urahisi, ikawa tofauti. Rais Magufuli aitishe utafiti huru umsaidie. Wabunge pia wafanye utafiti majimboni kwako. Nusu muhula imeshakamilika.