Utamtambuaje mpenzi mwenye tabia za kidikteta?

Muktasari:

  • Tunasukumwa na upendo ulio ndani yetu ingawa tafiti zinaonyesha kwamba wengi siku hizi huingia katika uhusiano kwa sababu nyingine zaidi ya pendo.

Kama umewahi kuwa katika uhusiano wa mapenzi au una kiu ya kuingia utakubaliana na mimi kwamba nia na dhumuni la kuingia ni kupendana.

Tunasukumwa na upendo ulio ndani yetu ingawa tafiti zinaonyesha kwamba wengi siku hizi huingia katika uhusiano kwa sababu nyingine zaidi ya pendo.

Hatuingii kwenye penzi kwa nia ya kutawalana, hatutegemei kumuona mtumwa na mtwana kati ya wapenzi wawili, hatutegemei kumuona muoneaji na muonewa, mtawala na mtawaliwa.

Ingawa haya yanatokea sana katika uhusiano na wewe ni shahidi hata kama hakuna wanaojua kuwa hili linakutokea katika uhusiano wako kwa sababu picha mnayoionyesha nje ni kama vile kila kitu kiko shwari, kumbe ndani ya mioyo yenu mmoja anajua kuwa anadhulumiwa haki yake ya kusema, kupendekeza kitu, kuchagua kitu na kuelekeza jambo.

Yamkini anayekufanyia hivi wala hajui kuwa anakuumiza na kwamba bado kidogo tu penzi lako kwake litakufa kwa kukosa pumzi kwa namna alivyokuminya.

Hapa nataka nikusaidie kukupa baadhi ya tabia unazoweza kuziona kwa mpenzi wako mara kwa mara ili ufahamu kuwa kiu yake ni kukutawala kimyakimya au hata waziwazi.

Kiu yangu ni kwamba kwa kuzijua tabia hizi anayemfanyia mpenziwe ajijue na kufahamu kuwa hatendi vyema na anahatarisha penzi lao, na anayefanyiwa pia ajue asili ya kinachomsibu ili wote kwa pamoja wajaribu kutafuta mbinu za kurejesha hali bora zaidi.

Angalizo. Haimaanishi mara tu utakapoona tabia moja kati ya hizi basi mpenzi wako anakutawala au ni dikteta, ila pale unapoona kujirudiarudia na kukomaa kwa tabia mojawapo au mjumuisho wa tabia hizi basi kuwa macho kwa sababu hali hizi zinapozidi ni ngumu kuvumilika.

Tabia.

Mara kwa mara mkienda kwenye migahawa au mitoko inatokea kuwa pale anapotaka mketi ndipo mtakakoketi hata kama wewe umeona sehemu nyingine nzuri zaidi labda kwa sababu ya upepo au mwanga au mandhari, lakini kwa sababu tu alishapendekeza sehemu basi utalazimika kufuata matakwa ya kile anachotaka.

Hata kama atagundua kuwa pale alipopachagua sio pazuri kama ulipochagua wewe, bado atang’ang’ania mketi pale alipopaona na kutoa sababu tele za kupakataa pale ulipopachagua.

Kila mara mnapokutana na marafiki labda iwe kwenye mitoko, maeneo ya ibada, mikutano, harusini na kwingineko ambapo mko pamoja, pale anapotaka wewe uwajue rafiki zake atakuita kwa ujasiri ndani yake akijua huwezi kukataa na atataka rafiki zake wakujue bila kujali uko kwenye hisia gani muda au siku hiyo.

Sasa ikifika siku au wakati ambao wewe unatamani umtambulishe kwa rafiki zako unaanza kuona anakunja sura anaonyesha kutotaka kusumbuliwa, kama ameketi basi hatanyanyuka ilimradi tu kukuonyesha kwa vitendo kuwa hayuko tayari kuwekwa upenuni eti ili tu ajulikane kwa marafiki zako wewe.

Mwisho unajikuta unaenda peke yako na kuwasalimia rafiki zako na kutafuta vijimaneno vya kuonyesha ama mpenzi wako anaumwa, hajisikii vizuri au kabanwa na jukumu fulani ila ukweli ni kwamba moyoni mwako unahisi kudhulumiwa na kuumia kwa sababu ulitamani msimame pamoja, mtabasamu pamoja.

Ukweli ni kwamba maumivu haya hayaelezeki na wala hawezi kuyajua na yakilimbikizana yana madhara makubwa baadaye.

Inapofika wakati mnaongelea mambo yahusuyo ndugu zenu, atataka ujihusishe na mambo ya ndugu zake na yamkini kukulaumu pale unapoonyesha kujiweka mbali na masuala ya ndugu zake, atataka muende kwenye sherehe zote za kwao, misiba, mtembelee wagonjwa, shida na raha za kwao zote utazijua hata kama nyingine ulitamani kutokuwepo.

Sasa inapofika masuala ya ndugu zako mikiki inaanza, mara yuko ‘bize’ na hili au lile, mara anaumwa, safari za kikazi,uchovu usiopimika. Ukija kuangalia unakuta kila kukiwa na kitu upande wenu unajihusisha mwenyewe.Kwa haya utajua kwamba huyu mtu ni ‘dikteta wa mapenzi’.

Itaendelea..