Utamu wa Viti Maalumu na ugumu kuwania ubunge majimboni

Muktasari:

  • Makundi haya yote mbali na uwakilishi wa wananchi bungeni, kila moja lina malengo maalumu na Viti Maalumu vinalenga kutoa fursa kwa wanawake kushiriki katika siasa.

Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kama ilivyo kwa Baraza la Wawakilishi na mabaraza ya madiwani kuna wawakilishi wa aina mbalimbali – Wapo wale wa kuchaguliwa, kuteuliwa na wale wa viti maalumu.

Makundi haya yote mbali na uwakilishi wa wananchi bungeni, kila moja lina malengo maalumu na Viti Maalumu vinalenga kutoa fursa kwa wanawake kushiriki katika siasa.

Katika jamii zetu zilizojaa mfumo dume, ilikuwa ni vigumu kwa wanawake kujipenyeza katika siasa kutokana na ama kukandamizwa au kukosa ukwasi unaohitajika kufikia hatua hiyo.

Baada ya mijadala mbalimbali ya kidunia kuhusu usawa wa jinsia na baadaye kupitishwa matamko kadhaa ya kitaifa na kimataifa ya kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo hivyo – mfano tamko la nchi za jumuiya ya maendeleo nchi za kusini mwa Afrika (SADC) kuingiza asilimia 30 ya wanawake katika vyombo vya maamuzi au ile kaulimbiu ya awamu ya nne ya 50 kwa 50, umuhimu wa viti maalumu ulizidi kuongezeka nchini.

Hata hivyo, viti hivyo maalumu vimekuwa ni mjadala mzito na wa muda mrefu kuhusu ama nafasi hizo ziendelee kuwapo, zifutwe au ziwe za muda tu.

Hoja inayobeba mjadala huo inaweza kuwa na lengo zuri la kuwapa wanawake fursa ya kuingia majimboni kushindania nafasi za uwakilishi kama ilivyo kwa wanaume. Wengine wanasema nafasi hizo zinawadhalilisha wanawake na kuonekana za kupewa kwa hisani.

Hata hivyo, wanaojenga hoja hizo ama wanasahau au wanaacha kuzingatia mazingira ya nchi na mfumo wa uongozi katika jamii.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Viti Maalumu ni muhimu kuwapo, lakini visiwe vya kudumu kama ambavyo baadhi ya wanawake wamechukulia, viwe na ukomo na baada ya hapo wanawake waliowahi kuvipata waende wakagombee majimboni.

Hawa wanapendekeza kuwa licha ya kuwapo faida lukuki za viti maalumu, walioteuliwa wawe na ukomo wa vipindi viwili kisha waende majimboni.

Kwa vipindi hivyo, wanasema wanawake hao watakuwa wamepata ujasiri, uzoefu na rasilimali fedha za kuwawezesha kusimama majimboni kugombea ubunge na kushinda.

INAENDELEA UK 20

INATOKA UK 17

Hapa wanatoa mfano wa mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Ester Bulaya wa Bunda Mjini ambao baada ya kupata uzoefu katika viti maalumu walihamia majimboni na kushinda.

Ni kutokana hatua hiyo, wanasiasa na wachambuzi wa masuala hayo waliozungumza na Mwananchi wanasema kukaa zaidi ya vipindi viwili katika viti maalumu ni kubweteka.

“Wakiondoka baada ya vipindi viwili wanawapa nafasi wengine, kukaa zaidi ni kubweteka,” anasema mwanasiasa mkongwe Njelu Kasaka.

Kasaka aliyepata kuwa mbunge na naibu waziri katika awamu ya pili anasema kuwa viti maalumu vilianzishwa kama njia ya kuwasaidia wanawake wengi waingie kwenye siasa kwa sababu mila na tamaduni hazikuwa zikiwapa nafasi hiyo.

Anasema lengo lilikuwa ni kwamba wanawake hao wazoee na baadaye wapiganie wenyewe majimboni, hivyo kukaa kwa mihula zaidi ya miwili si sahihi.

“Huko Ulaya, kama si Sweden ni Norway, kuna wanawake wengi bungeni kuliko wanaume, lakini siyo viti maalumu. Hao waligombea majimboni na wakashinda,” anasema.

Faida za Viti Maalumu

Kasaka anazitaja faida za kuwapo viti maalumu hapa nchini kuwa ni kuwaondolea wanawake aibu kwa sababu wengi wao barani Afrika wana aibu na inakuwa ngumu kwao kusimama mbele za watu kwenye majukwaa ya siasa na kunadi sera zao.

Anasema kupitia mikutano ya kisiasa wanayokwenda wanawake ikiwamo ya kampeni kwa wenzao, wanakuwa wanapata uzoefu na kuwa rahisi kwao kufanya kile wanachokiona.

Anaitaja faida nyingine kuwa ni kupata uelewa wa vitu vingi vinavyohusu nchi na Serikali kwa ujumla wawapo bungeni.

Mbunge huyo wa zamani wa Chunya, anasema kwa kuwa wabunge hao wa viti maalumu wanalipwa mshahara na posho mbalimbali kwa kipindi wanapokuwa wabunge na baadaye kiinua mgongo, fedha hizo zinawasaidia kujikimu kwenye kampeni, hivyo watakuwa wamepata faida nyingi ambazo wanawake wengine hawana.

Mbunge huyo anazungumzia mahitaji ya fedha katika uchaguzi, akisema utaratibu na utamaduni wa hapa nchini unawaumiza wanasiasa kwa kuhitaji kuwa na fedha nyingi.

“Hapa nchini ni tofauti na ninaweza kusema tumepindua mambo. Katika nchi nyingine watu wanaokuunga mkono ndiyo wanaopaswa kukuchangia kwenye kampeni. Lakini hapa kwetu anayegombea ndiyo anajigharamia yeye, na kuwagharamia wanaomuunga mkono na ndiyo maana wakati mwingine inatafsiriwa kama rushwa, ila ni muhimu kujipanga kwa ajili ya hilo wakati wa kugombea jimboni,” anasisitiza Kasaka.

Hoja ya viti maalumu kuwa siyo ya kudumu inaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk George Shumbusho ambaye anasema kuwa ni vizuri wakakaa mihula miwili na kupisha wengine.

Profesa Shumbusho anazitaja faida ambazo zinapatikana kwenye nafasi hiyo adhimu, kuwa ni kujifunza mbinu za ushindi kupitia wabunge wa kuchaguliwa kwa kuhudhuria mikutano yao.

“Pia, viti maalumu vinavutia wanawake wengine kujiunga katika siasa. Visingekuwapo, wanawake wachache sana wangejitokeza kuwania nafasi za kisiasa,” anasema Profesa Shumbusho.

Ingawa hajasema kama kuna haja ya kukaa muda mrefu au mfupi katika nafasi hiyo, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maida Abdallah anasema nafasi hiyo ina umuhimu na inamjenga mwanasiasa mwanamke.

Anasema ukiache mbunge wa jimbo ambaye anafanya kazi katike eneo dogo, mbunge wa viti maalumu anafanya kazi katika eneo pana hivyo ni rahisi kumfikia kila mwananchi na kutambua kero zake.

Anasema mbunge siyo rahisi kutekeleza kila kitu, hivyo wa viti maalumu wanapita na kuongeza nguvu katika kupigania maendeleo, mfano kuhusu suala la maji, umeme na mambo mengine yanayowasumbua wananchi katika eneo husika.

Ndiyo maana mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya anasema kuwa viti maalumu vinampa mbunge nafasi ya kufanya kazi na kujenga uaminifu kwa wananchi.

Anasema nafasi hiyo humwandaa mwanamke kwenda kwenye siasa za ushindani na ushawishi kwa wananchi, kutokana na kujifunza kutoka kwa wengine.

“Waliopitia viti maalumu wameonyesha ukomavu na wamekuwa wakifanya vizuri kwenye harakati zao, kama vile mimi, Halima Mdee, Esther Matiko, Suzan Kiwanga, Pauline Gekuru hivyo vinajenga sana,” anasema Bulaya.

Bulaya anasema ukianza kwenye nafasi hiyo na ukafanya vizuri hata suala la kampeni wakati utakapoamua kugombea jimboni halitakuwa mzigo kwako.

Anasema mara nyingi ukifanya kazi wananchi wenyewe ndiyo wanakupendekeza uwe mbunge wao, hivyo watakuunga mkono ikiwamo kukuwezesha kifedha katika suala zima la kampeni.

“Mimi sikuwa nimesema nataka kugombea ubunge Bunda Mjini, wananchi wenyewe walinipendekeza na wakaniunga mkono. Kuna wakati walikuwa wanajaza mafuta kwenye gari kwa ajili ya kampeni,” Bulaya anaelezea uzoefu wake.

Anasema si vibaya mbunge wa viti maalumu kujipanga kuwania jimbo mapema, kwa sababu akikaa bungeni muda mfupi atakuwa ameshapata uzoefu na kujifunza mengi.

“Wabunge wa viti maalumu wakitumia vema nafasi ya wao kuwa bungeni, kuhudhuria mikutano watajifunza vitu vingi katika muda mchache, hivyo si vibaya kama watajipanga kuwania majimbo, ingawa inategemea na muhusika mwenyewe.

“Kwangu mimi kupiga kazi ni muhimu sana. Wapo chuoni wafanyakazi kwanza ili wafaulu mtihani ulio mbele yao,” anasema Bulaya.

Hoja wa mbunge wa viti maalumu kukaa si zaidi ya vipindi viwili, inaungwa mkono na wengi akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda.

Mwakagenda anasema ni bora kukaa kwa miaka 10 na kusonga mbele kuwapa nafasi wengine wanaotamani kuingia bungeni kupitia mfumo huo.

Anasema wapo waliokaa kwa miaka 20 na kujaribu kugombea wakakosa kwa sababu ya ukosefu wa fedha na mfumo dume, ila ni vema wanaotaka kusonga mbele wakajipanga mapema.

“Nafasi ya viti maalumu inawasaidia wanasiasa wanawake kupata uzoefu, kupata uhusiano na watu mbalimbali, kutafuta wafadhili na kujua vitu vingi vinavyoihusu jamii na taifa kwa ujumla, kwa sababu wao hufanya kazi katika eneo pana zaidi,” anasema Mwakagenda.