VAR, teknolojia iliyochanganya wengi Russia

Muktasari:

  • Rais wa Fifa, Gianni Infantino anasema VAR imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanikisha kile kilichotarajiwa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya fainali za Kombe la Dunia, Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa), liliamua kutumia teknolojia ya kuwasaidia waamuzi (VAR) katika fainali za mwaka huu zilizoanza Juni 14 na kumalizika Julai 15.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino anasema VAR imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanikisha kile kilichotarajiwa.

Hata hivyo, kauli yake ni tofauti na mtazamo wa mashabiki na wadau mbalimbali wa soka. Kwa mtazamo wa wengi, VAR haikuwa mfumbuzi wa utata, badala yake malalamiko yalijitokeza kila mara ulipojitokea utata waamuzi hawakuyafanyia kazi kupitia VAR na kuamua vinginevyo.

VAR ilianza kuzua utata tangu mechi za hatua ya makundi mfano iliisaidia Ufaransa kushinda mchezo wake wa kwanza wa makundi dhidi ya Australia uliofanyika Juni 14, iliwazawadia bao la pili katika ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Croatia, Julai 15.

Kabla ya Ufaransa kupewa penalti yenye ukakasi iliyotokana na beki Ivan Perisic, kugongwa na mpira wakati akiruka kupiga kichwa, hata hivyo mwamuzi Nestor Pitana aliwapa Ufaransa penalti iliyofungwa na Antoine Griezmann na kuwapa uongozi wa mabao 2-1 hadi mapumziko.

Katika kipindi chote cha fainali hizo wachezaji, makocha, wachambuzi wa soka na wadau wengine wanadai teknolojia hiyo haikuwa suluhisho la utata.

Kocha wa Korea Kusini, Shin Tae-yong, anakumbuka jinsi teknolojia hiyo ‘VAR’ ilivyowanyonga walipocheza na Sweden na kumfanya mwamuzi Joel Aguilar kutoa penelti katika mechi hiyo waliyopigwa bao 1-0.

Kocha wa Australia hajasahau namna Antoine Griezmann, alivyofunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na uamuzi wa teknolojia hiyo na Ufaransa ilishinda mabao 2-1.

Gwiji la soka na nahodha wa zamani wa Argentina, Diego Maradona, anasema teknolojia hiyo ni nzuri lakini anadhani inatumiwa pale tu timu moja inapotaka kubebwa na kinyume cha hivyo mwamuzi wa kati anatoa uamuzi anaotaka.

Maradona ameshauri teknolojia hiyo iboreshwe kwa kuwaweka wasimamizi wasioegemea upande wowote ikibidi watu wasiokuwa na uhusiano au ushabiki wa namna yoyote na timu mbili zinazocheza.

Nguli huyo ameitaka Fifa kuboresha usimamizi wa VAR, akisema haitakuwa na maana endapo itaendelea kuongeza matatizo badala ya kupunguza malalamiko ya timu kuonewa na baadhi ya waamuzi.

Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea aliyekuwa nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba anasema kwa mtazamo wake VAR imesaidia kuwalinda washambuliaji ambao waamuzi hawakusaidia vya kutosha wanapocheza madhambi.