Vijana wa siku hizi ni zao la wazee wa siku hizi

Muktasari:

  • Ulishawahi kukatiza mahali, kwa bahati ukapishana na mtu ambaye kwa namna zote ulijiridhisha kabisa kuwa akili zake haziko sawa kichwani. Yaani kwanza hayuko nadhifu, pili kichwani ana manywele yaliyojisokota na yaliyokosa matunzo, tatu amevalia nguo zilizochanika na nne anatembea akiokota chupa za maji za plastiki zilizokwishatumika na kutupwa barabarani na raia wasiojua maana ya ‘weka jiji safi’

Inawezekana tangu kuanza kwa dunia hakujawahi kutokea vijana wa hovyo kama tunaoishi nao enzi hizi, si wa kiume si wa kike, wote ni aina ya binadamu ambao wanakupa kibarua cha ziada kugundua kuwa unayepishana naye barabarani ama unayezungumza naye si mgonjwa wa akili.

Ulishawahi kukatiza mahali, kwa bahati ukapishana na mtu ambaye kwa namna zote ulijiridhisha kabisa kuwa akili zake haziko sawa kichwani. Yaani kwanza hayuko nadhifu, pili kichwani ana manywele yaliyojisokota na yaliyokosa matunzo, tatu amevalia nguo zilizochanika na nne anatembea akiokota chupa za maji za plastiki zilizokwishatumika na kutupwa barabarani na raia wasiojua maana ya ‘weka jiji safi’.

Kisha hatua mbili mbele ukakuta stoo kubwa inayonunua vyuma chakavu na makopo – halafu kabla hujasogeza mbele zaidi ukapishana na kijana mwingine ambaye anafanana karibu kila kitu na yule uliyepishana naye awali, yaani ana manywele yaliyojisokota na amevalia nguo ziliochanikachanika, isipokuwa huyu ni nadhifu na hajabeba chupa.

Akili ya kibinadamu inaweza kukusaidia katika hili, ukagundua kuwa kati ya wawili hawa mmoja yupo kazini na mwingine ndiyo anakwenda na fasheni lakini kwa jinsi wanavyorandana unaweza kusema kwamba huyu wa pili ambaye hajabeba machupa, ndiyo ametoka kuuza chupa zake katika ile stoo uliyoiona.

Ninachojaribu kukwambia ni kwamba tuna vijana wa ajabu kuliko vijana wa enzi zote zilizowahi kutokea nyuma; lakini hiyo haitavunja rekodi ya kwamba pia kwa sasa tuna wazee wa hovyo kuliko wazee wa enzi yeyote iliyowahi kutokea hapo awali– hao tunawaita wazee wa enzi hizi, mababu na mabibi.

Mababu wa enzi hizi wanajua kupigana vita na wavulana wa umri sawa na watoto wao kugombania wanawake kuliko wazee wa enzi zozote zile zilizowahi kuwepo. Wazee wanaongoza kwa kutumia pesa kuwavutia watoto wetu tuliowapeleka vyuoni kusoma kiasi kwamba watoto wanakengeuka na kusahau kabisa kilichowapelekea huko na kuwa wasichana wa siku hizi. Si wanasoma ili wapate kazi, wapate pesa, wazee wa siku hizi wamewarahisishia maisha,

Wakati mabibi nao ni kama wana ligi na mababu wa siku hizi, wenyewe wanakula sahani moja na mabinti katika kuhakikisha wanamiliki wavulana wadogo umri sawa na watoto wa kuwazaa.

Matokeo yake, asilimia kubwa ya vijana wa kiume wa siku hizi hakuna tena anayefanania na enzi zile za vijana kuingia mtaani na kupigika kweli kweli kwa sababu wanafahamu wao ni baba wa siku za mbeleni kwahiyo wanahitaji njuruku kuwa baba wa ukweli.

Vijana wa siku hizi wamekuwa magoigoi, mabibi wanawakomaza watoto wetu wa kiume na mababu wanawaharibu mabinti zetu – na ndiyo chimbuko la vijana wa siku hizi.