Vikwazo vya uzalishaji wa viongozi wa kisiasa nchini

Muktasari:

  • Spika wa Bunge Job Ndugai alisema Bunge la 11 siyo Bunge la vijana kwa kuwa asilimia 80 ya wabunge wana umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea. Mbunge mdogo ana umri wa miaka 27 na mbunge mzee ana umri wa miaka 74.

Milango ya fursa za uongozi kwa vijana hususani wenye vipaji hapa nchini lilianza kuonekana kwa kasi mnamo miaka ya 2005.

Katika kipindi cha awamu ya Tano, vijana wamejaribu kuonyesha uwezo kupitia nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya mifumo rasmi bila kujali wamepitia mlango wa taasisi gani. Viongozi hao huzalishwa na taasisi za dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari, taasisi za elimu na vyama vya siasa.

Katika harakati za uzalishaji wa viongozi hao, Taasisi ya Uongozi na Mtazamo wenye Maudhui ya Soko Huria kwa vijana barani Afrika(ASFL) wiki iliyopita imekutanisha kundi la vijana 250 wanaotoka nchi za Nigeria, Uganda, Kenya, Afrika Kusini na mwenyeji Tanzania.

Msingi wa kongamano ulikuwa kwenye maeneo kadhaa hususani mbinu za uongozi wenye matokeo chanya kwa jamii. Ni awamu ya tatu tangu lilipoanzishwa Kongamano hilo mwaka 2016.

Vyama vikubwa vya siasa Chadema na CCM ambao walikuwa sehemu ya ushiriki wa kongamano hilo huzalisha viongozi wake katika mifumo tofauti na itikadi tofauti za kiuongozi.

Kwa mujibu wa CCM, viongozi vijana huandaliwa ngazi ya Shina hadi ngazi ya Taifa chini ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) wakati Bavicha huzalisha viongozi wake kupitia ngazi ya shule za msingi Chemchem, sekondari (Chaseso) na vyuo vikuu (Chaso).

Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bakari Mohamed anasema kikwazo katika uzalishaji wa viongozi nchini unaathiriwa na kukosekana kwa utamaduni wa kiraia, unaojenga mtazamo wa aina moja kitaifa.

“Challenge (changamoto) kubwa ni kukosekana kwa civil culture, kwa namna gani tunawajengea Imani ya pamoja, maadili ya msingi katika uongozi kwani kuna maadili ya msingi ambayo tunayahitaji kwenye msingi wa viongozi wetu bila kujali wanatokea NGOs, chama cha siasa, dini ,lazima kuwe na mambo ya msingi tunayokubaliana kama taifa,” anasema.

Profesa Bakari anasema katika miaka ya 2000, kulikuwa na mjadala wa kuandaa sera itakayosaidia itakayoanzisha elimu ya uraia, ikiwa na misingi ya utamaduni wa kiraia lakini ilikwama. “Vijana wanajifunza uongozi wanalelewa lakini umoja wa kitaifa utapungua, na kila upande utakuwa unazalisha viongozi kwa utaratibu wake tu,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji Kanda ya Afrika wa ASFL, Evans Exaud anasema hatua hiyo inachagizwa na uhitaji mkubwa wa vijana wengi barani, wanaotaka kuonyesha uwezo katika uongozi.

Evans anasema wanahitaji kujengeana maarifa mapya yatakayosaidia hususani katika utatuzi wa kero za wananchi kwa kutumia ubunifu na uwezo walionao.

Ushawishi katika uongozi

Kutokana na athari hizo, Mwanachama wa Taasisi ya Vijana ya Kimataifa(Yuna), Peter Mbando anasema wako vijana ambao wamekuwa wakiingia katika jukwaa la uongozi kwa kivuli cha fursa ya kujipatia ajira, na wengine wanaingia kutokana na hasira ya kutaka kuleta mabadiliko.

Mbando anayehamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu(SDG), upande wa vijana anasema; “Wapo vijana wanautazama uongozi kama fursa ya ajira, wanaona njia rahisi ni kupitia uongozi, lakini wako wanaoona mambo hayaendi kwa aina ya viongozi waliopo sasa Afrika ndiyo maana wanaamua kuingia ili kuleta mabadiliko kwa jamii,”anasema Mbando.

Kada wa CCM kutoka Umoja wa vijana, jijini Dar es Salaam , Elvira Cyprian(23), ambaye pia ni muhitimu wa shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora(UDSM) anasema vijana wanahitaji kuhoji maendeleo yenye tija na siyo ajira, akitamani fursa zifunguliwe zaidi kutokana na mapokezi mazuri ya vijana kwa jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, Patrick Ole Sosopi anasema wakati umefika kwa vijana kuanzisha tena mjadala wa kuwa na baraza la Taifa la Vijana nchini kutokana na changamoto ya tofauti ya mitazamo na itikadi katikati ya ujenzi wa Taifa moja.

Januari 2012, John Mnyika akiwa mbunge wa Ubungo kwa wakati huo aliwasilisha taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana.

Sehemu ya sita ya muswada huo ulikuwa unapendekeza kuanzishwa kwa Majukwaa ya Vijana katika ngazi ya Halmashauri, na Kamati za Vijana za Kata, Vijiji na Mitaa kwa madhumuni ya kuzishusha kwenye ngazi chini shughuli za vijana.

“Yaani tukae kama baraza la vijana Taifa, litakalokuwa na ujenzi wa dhana nzima ya uzalendo, kulea maadili ya uongozi na kujadili masuala kitaifa zaidi. uzalendo wa kuitumikia nchi na siyo uzalendo kwa serikali kwa sababu serikali itamaliza muda wake, Taifa litaendelea kuwapo,” anasema.