Viongozi wa michezo tambueni kuna kuibua vipaji

Muktasari:

  • Tatizo la visingizo ni kwamba vinatuondoa katika mtazamo wa ukweli wa tatizo na hivyo kuzuia maendeleo.

Ni kawaida yetu kutafuta visingizio. Huwa tunatafuta visingizio tunaposhindwa, kwa tabia zetu mbaya, kwa nia zetu mbaya, kwa kuwaumiza wengine, kwa kuwa wabinafsi na kwa makosa yetu. Hatutaki kukubali kuwa tuna ujinga, ni wabinafsi, wakatili!, wavivu, wasumbufu na mengi mengine ila tunaweka visingizio kibao.

Tatizo la visingizo ni kwamba vinatuondoa katika mtazamo wa ukweli wa tatizo na hivyo kuzuia maendeleo.

Kwa mfano, linapotokea kosa sehemu ya kazi tunatumia muda na nguvu kujadili nani wa kumlaumu badala ya kuendelea na shughuli zetu na kutafuta ufumbuzi wa kutatua tatizo lililotokea.

Watu tunaofuatilia masuala ya michezo tunafahamu kuwa tuna tatizo kubwa la maendeleo ya michezo nchini na limekuwa likishughulikiwa kwa visingizio vingi badala ya kutafuta ufumbuzi.

Tumekuwa tukiwatafuta watu wa kuwalaumu badala ya kutafuta njia za kuendeleza vipaji vilivyopo nchini.

Tanzania ni kati ya nchi zenye wachezaji wenye vipaji vya hali juu (katika soka) kuliko ilivyozoeleka kuwa nchi za Afrika Magharibi ndiyo zenye vipaji vingi vya wachezaji wa soka Afrika, ila ni kweli ni watawala wa soka la Afrika.

Zipo sababu zinazofanya nchi za Afrika Magharibi kuwa watawala wa soka la Afrika, sababu kuu ni kwamba nchi nyingi za Afrika Magharibi zilitawaliwa na Wafaransa, ambapo Wafaransa wana sera ya kusambaza utamaduni wao katika makoloni yao, hivyo wachezaji soka na watu wenye vipaji vingine walipata na hupata nafasi ya kwenda Ufaransa kwa urahisi. Pia, Ufaransa tangu zamani ilikuwa ikichukua wachezaji katika eneo hilo la Afrika Magharibi kwa ajili ya kuwatumia katika mashindano mbalimbali Ulaya.

Sababu nyingine kuu inayofanya soka la Afrika Magharibi kuwa juu ni mawakala.

Eneo hili la Afrika Magharibi linatolewa macho na mawakala wakubwa.

Hali hiyo haijatokea kwa kubahatisha, ni suala la motisha iliyopo katika eneo hilo, wachezaji wa Kusini mwa Afrika au Afrika Mashariki na Kati hawana motisha, kwa mfano wachezaji wa Afrika Kusini hawana nia ya kutaka kucheza soka Ulaya, wanalipwa mishahara mizuri.

Vilevile wachezaji wa Afrika Mashariki na Kati hupata wakati mgumu kucheza nje ya maeneo yao, pia wachezaji wa maeneo ya Kaskazini mwa Afrika na Kusini mwa Afrika huona aibu kwenda kucheza soka nje ya maeneo yao.

Sababu nyingine ni kuwa klabu za nchi za Afrika Magharibi nyingi zinamilikiwa na mtu binafsi ambaye hutegemea kuendesha klabu kwa kuuza wachezaji, ni tofauti na Tanzania ambapo makampuni binafsi yanadhamini klabu na soka la kulipwa lipo juu kidogo kwa nchi za Afrika Mashariki.

Sababu kubwa nyingine ni umasikini na mifumo mibovu!.

Umasikini upo sehemu zote za Afrika, lakini eneo la Afrika Magharibi lina umasikini na mifumo mibovu Zaidi ya kuendesha soka.

Katika sehemu nyingine za Afrika kuna umasikini, lakini ligi zinaendeshwa kwa utaratibu mzuri kiasi na malipo kwa wachezaji siyo mabaya.

Hali hiyo ya umasikini na mifumo mibovu ya kuendesha soka ndiyo inawafanya wachezaji wa Afrika Magharibi kutoka katika nchi zao na kwenda nchi yoyote Afrika, Marekani, Asia au Ulaya kucheza soka.

Ni wazi kuwa wachezaji wa nchi za Afrika Magharibi wana vipaji vya asili kama walivyo wachezaji wengine wa Afrika, ila wachezaji wa Afrika Magharibi wanaendelezwa kwa njia mbalimbali bila kutafuta visingizio.

Kinachokwamisha Afrika Mashariki ni ukata ambao uchumi wa mataifa mengi ya ukanda huo yanafanana, lakini vilevile wachezaji nao wana utayari hata wakiibuliwa?