Vyuo vimejaa wanafunzi wanaosoma kwa mkumbo

Muktasari:

  • Idadi hiyo ya vijana inaashiria changamoto ya ukosefu wa ajira ambapo hadi mwaka 2017, Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 15 ya vijana nchini wanakabiliwa na tatizo hilo.

Kila mwaka kuna vijana wapatao 700,000 wanaoingia kwenye soko la ajira wakimaliza masomo kuanzia shule za msingi, hadi vyuo vikuu.

Idadi hiyo ya vijana inaashiria changamoto ya ukosefu wa ajira ambapo hadi mwaka 2017, Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 15 ya vijana nchini wanakabiliwa na tatizo hilo.

Swali kuu ni je, wameandaliwa kiasi gani kusomea kozi zinazochechemua vipaji vyao ili zirahisishe kuwapatia ajira?

Tatizo linaanza tangu wakati wa kuchagua kozi za kusomea, ambapo baadhi ya wanafunzi kwa kukosa uelewa huishia kuchaguliwa vyuo na wazazi wao. Wengine hufuata mkumbo na wachache hupata vyuo sahihi kwa taaluma wanazotaka.

Tanzania ina zaidi ya vyuo vikuu 30 na taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada, huku pia kukiwa na vyuo vya kati vya ufundi.

Hata hivyo, vyuo na taasisi nyingi hazijulikani na hivyo wanafunzi wengi kulundikana kwenye vyuo vichache hasa vya Serikali na kujikutaka wakikosa nafasi za masomo, huku vyuo vingine vikikosa wanafunzi wa kutosha.

Nini tatizo?

Kilichopo ni kuwa wanafunzi wengi hawana taarifa za kutosha, hivyo kujikuta wakifuata mikumbo ya marafiki zao na kujikuta wakikosa vyuo stahiki.

Hali hiyo huwafanya vijana wengi kushindwa kutimiza ndoto zao maishani. Wengine wamelazimika kusomea kozi ambazo hawakuzipenda na hivyo kujikuta wakishindwa kufanya kazi kwa ufanisi au wakifanya kazi tofauti na zile walizosomea.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki, anasema wanafunzi wengi wamejikuta kwenye kozi na baadaye kwenye ajira ambazo hazikuwa chaguo lao na hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

‘’ Mtu anataka kuwa mfamasia, anataka kuwa daktari au anataka kuwa mtu wa mafuta na gesi afanye nini? Hata wazazi hawajui wawapeleke wapi wanafunzi hao, wanachojua ni kutoa ada tu,’’ anasema.

INAENDELEA UK 18

INATOKA UK 17

Naye Benjamin Mohamed ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, anasema vijana wengi wameshindwa kutumia vipaji vyao, kwa sababu ya kukosa mwelekeo unaotakiwa katika maisha yao.

“Kuna vipaji vingi kutoka kwa vijana ambavyo havitumiki kwa sababu ya kutotambuliwa mpaka mtu anafariki. Kwa hiyo jamii inakosa mchango wa vijana,” anasema.

Mohammed anasema , ameshaandika vitabu vitatu vinavyoeleza fursa za vijana na jinsi zinazvyotumika kuondoa umasikini katika jamii.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu anasema: “Tumekuwa na tatizo la vijana wetu kufuata mkumbo, hawajui wanataka nini, matokeo yake wanasoma kozi ambazo wakimaliza, wanajikuta wanalundikana kwenye fani moja halafu wanalalamika hakuna ajira, wakati kuna kozi nyingine hazina wanafunzi lakini zina ajira nyingi,” anasema Lissu.

Taasisi yatoa mafunzo kwa wanafunzi

Kwa kutambua haja ya kuwa na wanafunzi wanaojitambua hasa katika kufanya uchaguzi wa masomo na fani, taasisi ya Global Education Link (GEL) hivi karibuni iliandaa mafunzo kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam yaliyohusu kuwapa ushauri wa jinsi ya kuchagua kozi zinazorandana na vipaji vyao.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi wa GEL, Abdul Malik Mollel anasema taasisi yake imeanzisha programu hiyo kwa wanfunzi wa shule za sekondari, ili kuwapa uelewa wa vyuo vilivyo na kozi wanazotarajia kusoma kwa malengo ya kupata ajira wanazotaka siku za usoni.

Anasema mahitaji hayo yamejitokeza baada ya kuona wanafunzi wengi wanafaulu mitihani wa kidato cha sita, lakini wanakosa nafasi vyuoni kwa kutokuwa na uelewa wa sifa zinazotakiwa na vyuo vilivyopo.

“Wanafunzi wengi mara nyingi wanakuwa na matamanio makubwa ambayo wakati mwingine hayatekelezeki kwa sababu hawana uelewa wa sifa zinazotakiwa vyuoni, hivyo kujikuta wakisoma kozi wasizotaka au kukosa kabisa kozi zitakazowafikisha kwenye ajira za ndoto zao,” anasema na kuongeza:

“Kwa mfano, leo tumewaita wanafunzi wanaochukua mchepuo wa Kemia, Jiografia na Biolojia na wale wa Fizikia, Kemia na Baiolojia. Wote wanataka kusomea udaktari, lakini ukiwauliza sifa zinazotakiwa hawajui, matokeo yake wanakwama wakati wa kuomba nafasi vyuoni.”

Anasema mafunzo hayo yanalenga kuwapa mwangaza wanafunzi wa kozi wanazosomea kulingana na ndoto walizonazo katika ajira kwa kutumia wataalamu wa saikolojia na kozi za kisayansi zilizomo katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Alisema program hiyo imeanzia Dar es Salaam kisha itaendelea mikoani siku za usoni na mafunzo yanatolewa bure.

Mbali na kuwapa ushauri, Mollel pia anasema amekuwa akitoa ushauri kwa wanafunzi na wazazi wanaotaka watoto wao wakasomee vyuo vya nje.

Mkuu wa Operesheni wa taasisi hiyo, Regina Lema anasema wanawaunganisha wanafunzi na vyuo vya nje na baada ya hapo mzazi au mlezi atapata taarifa zote za maendeleo ya mwanafunzi.

“Baadhi ya wanafunzi wanakwenda kusoma nje ya nchi bila kuwa na taarifa za kutosha matokeo yake wanafunzi wanajiingiza kwenye makundi ya uovu na kupoteza malengo yaliyowapeleka kusoma.

“Kwa hiyo sisi tutahakikisha chuo anachokwenda mwanafunzi ni sahihi na tunawasiliana na walimu mara kwa mara ili kujua maendeleo yake,” anasema Regina.

Anasema mbali ya kuwatafutia vyuo vya nje wanafunzi, wanawasaidia pia katika masuala ya uhamiaji ikiwa pamoja kupata pasi za kusafiria na viza.

“Kuna faida kubwa ya kusoma nje ya nchi, kwanza unajifunza mambo mengi yanayoendelea duniani ikiwa pamoja na tamaduni za watu na kazi. Ukiwa huko pia unaweza kutembelea nchi nyingi zaidi. Kwa mfano, kama unasomea China, unaweza kutembelea Hong Kong, Singapore, Malaysia na nyingine za karibu kwa gharama nafuu,” anasema.

Wasemavyo wanafunzi

Baadhi ya wanafunzi wamezungumzia mafunzo hayo na kusema yameamsha ari ya kujisomea zaidi ili watimize ndoto zao.

Christopher Liyegwa anayesoma kidatio cha sita katika Shule ya Sekondari Pugu, anasema amejifunza jinsi ya kutumia ndoto zake na kuzisimamia maishani mwake.

“Nimejifunza jinsi ya kutumia muda, kujiamini na kuishi na watu ili nifikie malengo katika maisha. Mimi natamani kuwa daktari, nimejipanga na ninasimamia ndoto yangu,” anaeleza.

Naye, Magdalena Richard anayesoma kidato cha sita shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa, anasema mafunzo hayo yamechochea ndoto yake ya kuwa mhandisi wa umeme.

“Kwanza nimejifunza jinsi ya kutambua ndoto yangu, mikakati yangu katika hiyo ndoto na kuishikilia ndoto hiyo. Je, watu wananionaje katika hiyo ndoto, na jinsi ya kutunza muda na kujiamini ukiwa mbele ya watu. Nijiulize nataka kuwa nani? Binafsi napenda kuwa mhandisi wa umeme, kwa hiyo najitahidi shuleni ili niifikie,” anasema Magdalena